Friday, February 25, 2011

Mbunge wa Arusha mjini atembelea viwawa njiro...

Mbunge wa Arusha mjini Hon.Godbless Lema jumapili hiliyopita alitembelea parokia yetu kuangalia maendeleo ya vijana katika parokia yetu na kukutana na mwenyekiti wa viwawa njiro na viongozi wengine tulijadili mipango mbalimbali ya kimaendeleo ya parokia yetu na kijimbo.Mbunge wa wa arusha mjini nampongeza sana kwa moyo wake wa kujitoa.

Facebook, simu za mkononi zinavyoumiza watu katika mapenzi.

TUPO kwenye muktadha wetu unaosema: “Facebook, simu za mkononi zinavyoumiza watu kwenye mapenzi.”
Somo hili ni zuri, ndiyo maana baada ya kutoa sehemu ya kwanza, kwenye toleo la Jumatatu wiki hii, nilipata simu na meseji nyingi kupindukia.

Nasema ahsante kwa pongezi na naomba uambatane na mimi, ili tuendelee kutoka pale tulipoishia. Wiki iliyopita, nilitoa mifano kadhaa iliyopo nyuma ya migogoro ya simu za mkononi.

Hata hivyo, nimeona mada hii niichambue katika maeneo mawili. Wiki hii niendelee na somo la simu, halafu likiisha nitaanza na Facebook.

Niliandika jinsi watu wanavyotengana au wanandoa kukosa suluhu kwa sababu ya simu. Namna baadhi yetu tunavyokosa uhuru na amani na kuishia kuwapiga marufuku wenzi wetu wasishike ‘viselula’ vyetu, tukihofia siri zetu kugundulika.

Na tatu ‘niliwabonda’ wale wataalamu wa ‘kusevu’ namba za wenzi wao wa pembeni kwa majina tofauti, wanaume kuandika ya kiume na wanawake kuweka ya kike. Haya ni mapenzi ya mashaka.

‘Ki ukweli’ simu za mkononi ni utandawazi uliojaa chembechembe nyingi za sumu katika uhusiano wa kimapenzi na hii imetokana na watu wengi, kukosa ustaarabu na kuzitumia kuwasaliti wenzao
Hata hivyo, dhamira ya mada hii ni kukuandikia mbinu kadhaa zitakazokufanya wewe uishi na amani, bila kuzichukia simu kama dada yangu, Jasmin Mdanzi wa Nyakato, Mwanza ambaye sms yake niliiandika wiki iliyopita.

Pamoja na mbinu hizo, ningependa nikufahamishe kuwa haya nitakayoyaandika kama wewe utashindwa kuyafanyia kazi inavyotakiwa, hakuna kinachoweza kufanyika.

Mosi, wewe na mpenzi wako mnapaswa kuwa na uelewa mkubwa, kwa kutambua ukweli. Pili ni kuacha papara, mambo ya kusikia simu ya mpenzi wako inaita, unairukia na kutaka kujua anayepiga au aliyetuma ujumbe, vimepitwa na wakati.

ANGALIZO; Inawezekana akawa hana tabia ya kucheza mechi za nje, lakini wivu wako wa kupitiliza ndiyo unaomfanya ashindwe kuwa huru. Hata Zainab ambaye ni dada yake ofisini, anamuandika Zidane kwa sababu ukikuta jina la kike hauwezi kumuelewa hata akuambiaje.

Hujawahi kuona, mtu anamuelewesha kuwa fulani ni dada yake ambaye hushirikiana kwa ukaribu ofisini, lakini mama nyumbani haelewi, hapo matokeo yake ni jamaa ‘kumsevu’ Ramla kama Ronaldo.

Pointi ni hizi zifuatazo, naamini ukizisoma kwa herufi katika kila mstari, utapata kile kitu ambacho binafsi nimekikusudia, pia utaweza kuondoa migogoro isiyo na ulazima.

KUJIAMINI!
Inawezekana wewe ni muaminifu katika mapenzi yako, lakini tabia yako ya kujishtukia mara kwa mara kila anapokuomba simu, inamfanya aanze kuwa na mashaka juu yako.

Anajiuliza, kwanini haupendi ashike simu yako? Elewa kuwa jibu atakalolipata hapo ni kuwa kuna mchezo mchafu unaomchezea, na unaufanya kupitia simu ndiyo maana unailinda kama nguo ya ndani ambayo huivua wakati wa kuoga tu.
Wasilia na nico trac kama una mada ya kupost na nzuri 0716276000 or 0755451999

Dalili 10 za mwanaume anayekupenda.

ANAVYOTAZAMA
Mwanasaikolojia Zick Rubin kutoka Chuo cha Havard nchini Marekani aliwahi kusema kwamba watu wanaopendana hutumia asilimia 75 kutazamana kuliko wasiopendana, ambao kiwango chao ni asilimia 30-50.

Hii ina maana kwamba mwanaume anapotumia muda wake mwingi kumtazama msichana na kugeuka taratibu kuangalia vitu vingine kama mtu asiyependa kuacha kumwangalia, ujue anampenda.

MIPANGO
Mwanaume anayekupenda atakushirikisha kwenye mipango yake hasa ya muda mrefu. Mfano akitaka kununua kiwanja, kujenga nyumba atakuambia na pengine kutaka mchango wako wa hali na mali katika kulifanikisha hilo. Ukiona mwanaume anakuficha mambo yake, tambua kuwa huyo ana walakini kwenye penzi la dhati na la muda mrefu.

ATAONESHA HUZUNI
Katika maisha ya mapenzi kuna wakati wa kuhuzunika. Mwanaume mwenye upendo wa dhati atashirikiana nawe wakati wa huzuni na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa unapata furaha.

ATAKUAMINI
Dalili nyingine ya kupendwa na mwanaume ni kuaminiwa kwenye maisha kwa ujumla. Yaani mwanaume anayekupenda hatakuficha kitu, mfano pesa zake, atakupa uhuru kwenye simu yake na kukuamini katika usimamizi wa miradi yake.

ATAKUPA NAFASI
Ninapozungumzia nafasi nina maana atakukaribisha kwake bila hofu na kukupa nafasi ya kuingia na kutoka bila mipaka, atakupa nafasi ya kuweka vitu vyako kwenye kabati na kuruhusu nguo, picha na vitu vyako kuonekana wakati wote chumbani kwake.

UTAKUWA MWANAFAMILIA
Mwanaume aliyefikia chaguo la mwisho kwa mwanamke humshirikisha mpenzi wake kwenye masuala yake ya kifamilia, mfano atamwalika kwenye vikao vya harusi, kipaimara, atatoa nafasi ya kuambatana naye kuona wagonjwa, kusalimia ndugu na atakuwa huru kukutambulisha kwao.

ATAZUNGUMZA NAWE KUHUSU WATOTO
Kwa kuwa wanaume wengi hufikiria kuwa na familia, mwanaume anayekupenda atazungumza nawe mipango ya kupata watoto kwa kuwa atakuwa amekuchagua wewe kuwa mama wa wanaye na atapenda mazungumzo hayo.

ATAKUSAIDIA
Kwa kuwa kukwama ni sehemu ya maisha yetu, mwanaume anayekupenda atakuwa tayari kukusaidia unapokwama. Kila mara atahakikisha kuwa unakuwa na mafanikio na yeye atakuwa tayari kukupunguzia usumbufu wa maisha, kwa kukufuata kazini, kukusaidia baadhi ya mambo na hata ya nyumbani.

ATAJITOLEA
Ninaposema kujitolea ninamaanisha atakuwa tayari kufanya mambo yako na kuyaweka yake nyuma. Kwa mfano akiwa anapenda mpira na siku hiyo kuna mechi, lakini muda huo ukamwambia akufuate kwa mjomba wako atakuwa tayari kuacha furaha yake na kukujali wewe. Huyu ni mwanaume anayekupenda kwa dhati.

ATAAMBATANA NAWE
Wapenzi wengi wasiokuwa na mapenzi ya dhati huona aibu kuambatana na wapenzi wao kwenye mikusanyiko ya watu, lakini mwanaume anayekupenda atafurahia kutoka moyoni kuongozana nawe kwenye halaiki ya watu na kufurahia uwepo wako bila kuona aibu.

Mada hii inaishia hapa, hebu jiulize mwanadada, huyo uliyenaye anakufanyia haya, kama sivyo kwa kiwango kikubwa utakuwa na kazi ya kuhakiki penzi lako na pengine kujenga misingi mipya ya uhusiano wenu kabla haujavunjika.
   
                             

Sunday, February 20, 2011

Unapotokea kumpenda mtu aliye na mpenzi wake, fanya haya!


Tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuonana tena wiki hii tukiwa wazima. Lakini pia tumshukuru kwa kutuletea kitu kinachoitwa mapenzi.

Mapenzi yamekuwa yakichukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku na yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa furaha kwa kila mtu.

Kama huamini, angalia wale waliotokea kupenda na wao wakapendwa, utabaini nyuso zao zimetawaliwa na furaha isiyo na kifani. Lakini mapenzi hayo hayo yamekuwa ni chanzo cha vilio kwa baadhi ya watu.

Mpenzi msomaji wangu, kupenda hakuna macho! Moyo ukishapenda hausikii la kuambiwa. Katika hili ndiyo maana unaweza kumuona mwanaume kazimika kwa demu ambaye hawaendani kabisa lakini moyo wake ndiyo umeshapenda.

Ilishawahi kutokea msichana akampenda kijana mmoja ambaye ni fukara kupita maelezo. Yeye akawa ndiyo anamhudumia kwa kila kitu. Akamfanyia mpango wa ajira na mwisho wake wakafunga ndoa.

Sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na amani. Wamegeuka mfano wa kuigwa kwa jinsi wanavyopendana lakini huko nyuma msichana huyo alikuwa akichekwa kwa kutoa penzi kwa mwanaume asiye na mbele wala nyuma.

Hayo ndiyo mapenzi jamani! Lakini pia katika kufurukuta kumtafuta mpenzi wa kuwa naye maishani, mwanaume anaweza kujikuta unaangukia kwa demu ambaye tayari ana mpenzi wake.

Moyo wako unakuambia yeye ndiye mtu sahihi katika maisha yako lakini tayari ana mtu wake, unafanyaje?

Utapambana kuhakikisha unapata kile ambacho moyo wako umekipenda au utakubaliana na ukweli kwamba huwezi kuwa naye kwa kuwa ana mtu wake? Inapofikia hatua hiyo unaweza kujikuta upo njia panda hasa pale ambapo huyo mwenye mtu wake naye anaonesha kuwa na chembechembe za mapenzi kwako.
Kuna mambo kadhaa ya kukusaidia kukabiliana na hali hii.

Chunguza
Tumia muda wako mwingi kuchunguza juu ya uhusiano wake. Uhusiano wao umesimama na wanaonekana ni watu wenye ‘future’? Nasema hivyo kwa sababu, yawezekana uhusiano wa huyo uliyetokea kumpenda ni wa kuzuga tu na huenda wewe ndiye mwenye ‘future’ naye. Ndiyo maana nikasema chunguza uhusiano wake kwanza.

Usitafute uadui
Baada ya kuchunguza, ukibaini kwamba uhusiano wao hauko ‘siriasi’, vuta subira, lolote linaweza kutokea na likaufurahisha moyo wako. Lakini kama utaona ni watu walio siriasi na wanaelekea kuoana, usitafute uadui bure, kaa pembeni.

Una nafasi kwake?
Sawa umetokea kumpenda msichana aliye na mtu wake, umeshawahi kujiuliza kama una nafasi ndani ya moyo wake? Anaonesha dalili fulani za kukupenda kama unavyompenda na ni mtu anayeonesha kukumisi anapokuwa mbali na wewe? Utakapobaini una nafasi kwake, uamuzi wa kumpotezea hautakuwa na nafasi.

Ni rahisi kubadili uamuzi wake?
Unadhani huyo uliyetokea kumpenda anaweza kubadili maamuzi ya kumuacha huyo aliyenaye kama kweli hawana ‘future’? Utagundua hilo kwa kuongea naye na kumsikia kama anaweza kufanya maamuzi hayo ili awe na wewe.

Pingana na moyo wako
Ifike wakati upingane na moyo wako. Unajua moyo wako kukuambia kuwa unataka kuwa na uhusiano na demu ambaye tayari ana mpenzi wake wakati mwingine utakuwa unakupotosha.

Kwa hiyo ukiona vipi, pingana nao. Acha kumng’ang’ania msichana mwenye mpenzi wake licha ya ukweli kwamba, huenda wewe ndiye mwenye nafasi ya kuwa mume wake na siyo huyo aliye naye.

Urafiki ni poa?
Umempenda sana na hauko tayari kumkosa katika maisha yako lakini imetokea kwamba tayari yuko na mtu na umebaini huna nafasi kwake kabisa? Usiumie, omba angalau urafiki. Siyo urafiki wa kivile sana ila angalau pale unapotaka kusikia sauti yake kwa kumsalimia tu, upate nafasi hiyo.

Usiumie, yupo mwingine
Haina haja ya kujitafutia vidonda vya tumbo bure kwa kuwa tu umebaini uliyetokea kumpenda tayari ana mtu. Chukulia ni hali ya kawaida, mademu wazuri ambao wanaishi singo wapo kibao huko mtaani, ni suala la wewe kutulia tu. Amini yupo mwingine ambaye atayafanya maisha yako yawe ya furaha.

Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba, unapotokea kumpenda mtu fulani, pambana kuhakikisha unampata kwa sababu ukimkosa maisha yako yanaweza kuwa gizani. Ila pale utakapoona uwezekano wa kuwa naye haupo, usilazimishe ndugu yangu. Kumbuka haya ni maisha tu!


Friday, January 14, 2011

Kama una moyo mdogo, usitake kujua historia ya mpenzi wako...

NAAM kama ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba, ili kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku ambayo yametawaliwa na mapenzi kwa asilimia kubwa.


Leo nataka tuzungumzie kitu kimoja kuhusiana na jinsi mtu anavyopokea historia ya nyuma ya mwenzake, pale mnapokuwa mmeanzisha uhusiano mpya kila mmoja wenu alikuwa tayari amekwishauanza kwingine.
Ni vizuri kila mmoja kuwa muwazi kwa mwenzake pale anapotaka kujua historia ya nyuma ambayo itamuondoa hofu kwa kujua nini mwenzake alifanya nyuma. Hii husaidia kukufanya usishangae ukijua kitu cha mwenzako ambacho tayari aliishakueleza kama kitajitokeza mbele.
Lakini hapa kuna kitu kimoja ambacho ni muhimu sana watu kujua, kitu hiki humfanya mtu kupoteza imani ya mwenzake pengine kujuta kwa nini alikubali kuwa mwenza wake. Japo katika maisha yetu ya kila siku, kila mtu anatakiwa kuitunza rekodi yake kabla ya kuanzisha uhusiano.
Na hii imekuwa ikiwaelemea sana wanawake pale wanapokuwa wamekutana na wanaume zaidi ya mmoja, akili ya mwanaume atajua wewe ni malaya, Lakini ni tofauti na mwanaume hata akitoa historia yake kuwa alikuwa na wanawake watano bado kwa mwanamke haimsumbui moyoni bali humlinda kwa muda ule aliokuwa nao.
Ila atakuwa na wivu sana kwa kuamini wewe ni mzuri kila mwanamke anakutaka. Nia yangu ni kuelezea uwezo wa mtu kupokea historia ya mwenzake, kama una moyo mdogo si vizuri kutaka kujua historia ya mpenzi wako hasa wanaume ambao huenda ukaelezwa mtu fulani ambaye unamfahamu hata ukimuona moyo unakupasuka japo mpenzio amekuhakikishia hayupo naye tena.
Historia ina faida gani?
Faida ya historia kwa wapendanao ni kuondoa uchafu ambao pengine kama ungeusikia siku za mbele ungekuumiza moyo wako. Na pengine hata kujilaumu kwa nini hukuujua mapema. Faida nyingine ni kumjua mwenzako kiundani pengine ndugu yako wa toka nitoke ambaye mlipotezana mkiwa wadogo.
Unapotaka historia ya mwenzako hakikisha moyo wako jasiri na kuwa tayari kusamehe hata yale yatakaoumiza moyo wako. Na baada ya kupokea historia ni nafasi yako ya kujenga hatua nyingine kwani siku zote mwisho wa penzi la zamani ni mwanzo wa penzi jipya.
Pia pengine mwenzako kabla ya uhusiano wenu ana mtoto lakini amefanya siri kwa wewe kuamini hana motto mwisho wa siku unajua. Lazima moyo utakuuma na kuamini mwenzako si mkweli.
Katika maisha ya leo kina mtu ana makosa yake ambayo yanarekebishika, kama historia ya mwenzako ni mbaya au amekukosesha amani. Tumia makosa yake kujenga penzi imara kwani siku zote mwenye akili timamu hujifunza kutokana na makosa yake.

Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

Monday, December 6, 2010

Ya kuzingatia unapokutana kwa mara ya kwanza na mpenzi wako!

Ni matumaini yangu kwamba muwazima bukheri wa afya na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku. Wiki iliyopita nilizungumzia umuhimu wa wale walio katika uhusiano kufanya kila wanaloweza kuhakikisha hawaachani kirahisi labda ziwepo sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao.

Mada ya wiki hii ni maalum kwa wale wanaoanzisha uhusiano mpya au wale wanaoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa mara ya kwanza.

Yawezekana ukawa ‘umemtokea’ mtu na kumueleza kwamba unampenda na kwa bahati nzuri jibu likawa zuri kwa yeye kukukubalia ombi lako.
Kuna ile siku ya kwanza ambayo mnapanga mkutane ili muweze kuzungumza mambo kadha wa kadha kuhusu uhusiano wenu.

Siku ambayo mnakutana kwa mara ya kwanza ni siku muhimu sana kwenu, ni siku ambayo kila mmoja anatakiwa kuwa makini. Achilia mbali hayo, yapo mambo unayotakiwa kuyazingatia ili kuifanya siku hiyo iweze kuwa ya kihistoria.

Haya ndiyo ambayo leo hii nimedhamiria kuwaandikia angalau kwa ufupi nikiamini kwamba, yatakuwa ni yenye manufaa kwenu.

Mazungumzo yenu
Huyu mpenzi wako ndiyo mnakutana kwa mara ya kwanza, jitahidi sana mazungumzo yako yawe ya kumfanya ahisi amempata mtu sahihi katika maisha yake. Kuwa makini na kila neno na kila sentensi inayotoka kinywani mwako.

Usijioneshe kwamba wewe ni mzungumzaji sana wala mkimya sana. Kuwa katikati kwa sababu, kuongea sana au kuwa mkimya sana ni tatizo linaloweza kuuyumbisha uhusiano wenu kwa siku za mwanzo.

Zungumzia mambo yanayogusa maisha yenu na siyo kuhusu watu wengine. Andaa mada kichwani mwako ambazo ungependa mzizungumzie mtakapokutana.

Itakuwa ni kitu cha ajabu sana endapo utaanza kuuliza ‘Hivi ulishakuwa na uhusiano na watu wangapi mpaka sasa?’ Swali hilo si la msingi sana kuliuliza kwa siku hiyo kwani linaweza kuyumbisha pia uamuzi uliouchukua wa kumkubali. Dadisi mambo ya msingi tu na mengine yapotezee.

Utoke vipi?
Suala la kuchagua nguo za kuvaa pale unapokwenda kukutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza si la kupuuza. Wapo watakaosema suala la mavazi halina umuhimu bali mapenzi hutoka moyoni, ni sawa lakini kuvaa kwako pia kunaweza kumfanya mpenzi wako avutiwe nawe zaidi.

Sisemi kwamba kama hauna nguo na viatu vizuri ukaazime, hapana! Chagua katika hizo hizo ulizonazo zile ambazo unaamini kabisa zitaongeza upendo kutoka kwake.

Pia vaa kulingana na wakati na sehemu mnayokwenda. Kama ulisoma moja ya makala zangu nilizowahi kuandika huko nyuma yenye kichwa cha habari kisemacho “Uvae vipi unapokwenda wapi, utakuwa unafahamu unachotakiwa kufanya.

Aidha, kama ni mwanamke usijirembe kupitiliza, jipulize manukato yasiyoweza kumkera mpenzi wako tena iwe kwa mbali sana. Kwa kifupi muonekano wako uwe ‘simpo’.

Muende wapi?
Maeneo ambayo mara nyingi sana wapenzi hupenda kukutana ni ufukweni, hotelini, baa au sehemu nyingine ambazo ni za kijamii. Epuka kutaka kukutana na mpenzi wako kwa mara ya kwanza gesti.
Nasema hivyo kwakuwa, kama wewe ni mwanaume mpenzi wako atafikiria kwamba lengo lako si kuanzisha uhusiano ‘siriasi’ bali una lako jambo.

Hata kama atakuja kwakuwa anakupenda lakini yawezekana akaanza kujenga picha tofauti na wewe na anaweza kukosa uhuru mtakapokuwa pamoja.
Hivyo, chagua sehemu ambayo mtakaa huku kila mmoja akijisikia huru bila kujenga mawazo tofauti kwa mwenzake.

Usiri na usalama wa eneo mnalokutana
Kikubwa cha kuangalia katika sehemu ambayo mnatarajia kukutana kwa mara ya kwanza ni ile ambayo mtaongea mambo yenu bila watu wengine kusikia wala kuwavuruga. Kama ni ufukweni, nendeni sehemu ya peke yenu lakini pia ambayo ni salama.

Msiende sehemu ambayo unahisi mpenzi wako anaweza kushindwa kuwa huru kutokana na watu kujazana au sehemu ambayo inatishia usalama wenu. Angalieni sehemu nyingine.

Kwa leo jamani ni hayo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

Friday, November 26, 2010

Mambo kumi yanayohitaji umakini kwenye mapenzi......

Watu wengi wamekuwa wakiyachukulia mapenzi kama kitu cha zawadi, ambacho mhusika hatakiwi kutazama ubora wake, kitu ambacho si sahihi.

Kwenye mapenzi kuna mambo kumi ya msingi ambayo yanataka umakini mkubwa katika kuyatenda, la sivyo madhara yanaweza kuwa makubwa. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:

1. KUCHAGUA- Tunapokuwa na hisia za mapenzi lazima umakini uwepo kwenye kuchagua. Ifahamike kuwa katika ulimwengu huu tunaoishi tuna wanaume na wanawake wengi hivyo jukumu letu kubwa litakuwa ni kuchagua mmoja wa kutufaa, kwa kuangalia kama ana sifa tunazohitaji.

2. KUKUBALI- Watu wengi siku hizi wamekuwa wepesi mno kukubali kutii hisia zao. Utakuta mtu anashawishika kimapenzi mpaka anachanganyikiwa kisa katumiwa ujumbe kwenye facebook au amepigiwa simu na kusikia sauti nzuri. Mapenzi ya kweli hayataki tabia hiyo, lazima tuwe makini tusikubali kujiingiza kwenye mapenzi kwa pupa.

3. KUJITAMBULISHA- Nyakati hizi wapenzi wamekuwa wepesi mno kuutambulisha uhusiano wao kwenye jamii. Utakuta msichana amefahamiana na mvulana wiki moja iliyopita, cha ajabu atawaambia watu wote: “Mimi mchumba wangu ni fulani.”
Tabia hii inaonesha mtu si makini, kwani kwenye mapenzi kuna suala la kujiridhisha kwanza na chaguo, kabla hujamtambulisha mwenza wako, vinginevyo utatambulisha wanawake wengi kwenu hadi wazazi watakupuuza.

4. KUBADILI DINI- Licha ya kwamba haikatazwi mtu kubadili dini ili aolewe/aoe, lakini ni vyema kila mtu akafahamu kuwa suala hili linahitaji umakini sana kulifikia.

Upo ushahidi wa kutosha unaoonesha kuwa mtazamo wa familia hutofautiana sana pale mmoja wao anapoamua kubadili dini kwa lengo la kuoa au kuolewa.

Hii ina maana kwamba kabla ya kufikia hatua hiyo ni vyema mtu akafikiria kwa kina, asije akabadili dini leo halafu kesho akajikuta mume aliyekuwa anampapatikia si lolote kwake. Hali hii itakuwa imemletea matatizo makubwa kwenye familia yake na hata ndani ya nafsi yake mwenyewe.

5. KUZAA- Kuna watu si makini kabisa kwenye suala la kuamua azae na nani na kwa faida gani? Utakuta baba ana watoto kumi, lakini kila mmoja na mama yake. Hili si jambo jema, hata kama umempenda mwanaume fulani jiulize kwanza ni sahihi kwako kuzaa naye?
6. KUGAWA MALI- Wapenzi wengi wamejikuta kwenye majuto makubwa baada ya kuamua kwa pupa kuwagawia sehemu ya mali wapenzi wao.

Utasikia mwanzo tu wa uhusiano jamaa anamwambia mpenzi wake: “Nimeamua kiwanja cha Mbezi niandike jina lako na duka la Mchungwani litakuwa lako. Haya ni makosa.
7. KUAMINI-Wapenzi msiwe wepesi sana kuwaamini wenzenu, jambo la imani linahitaji muda kulifikia. Isitokee kwa haraka ukamuamini mpenzi wako na kuweka wazi kila kitu zikiwemo namba za siri za benki. Umakini unahitajika sana.

8. KUELEZA UKWELI- Ingawa mapenzi yanataka ukweli lakini kuuendea ni jambo linalohitaji umakini. Haitakuwa busara kumwambia mpenzi wako kuwa uliwahi kubakwa na watu kumi miaka miwili iliyopita, au ulishafungwa kwa ujambazi. Yote hayo lazima yatazamwe kwanza ili kuchuja faida na hasara zake kwa mwenzako.

9. KURUDIANA- Katika mapenzi kuna wakati mnaweza kutengana kwa sababu mbalimbali. Hali hii inapotokea wahusika wasirudiane bila kujichunguza na kuwa na maamuzi ya msingi, vinginevyo wanaweza kujikuta wakijutia uamuzi wa kurudia ‘matapishi’ yao.

10. KUACHANA- Mnapokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na ikatokea hali ya kuhitilafiana katika hili na lile, haifai kukimbilia kuachana.

Upo ushahidi kuwa wengi kati ya walioachana hujutia uamuzi wao. Ni vyema kabla ya kufika huko kila mtu akajiuliza mara mbili kama atakuwa sahihi kuachana na mwenza wake.Mimi NICOLAUS TRAC NAMPENDA MY LOVE SITAMUACHA KAMWE.

Mapenzi ni afya, ni kila kitu lakini yana kanuni zake!....NICOLAUS TRAC

Haihitaji papara kuamua kuhusu mwenzi wa maisha yako. Kuna fahari ya macho na kinachogusa mtima. Usimuone barabarani ni mzuri, ukakurupuka. Unatakiwa ujadiliane na moyo wako halafu mpate jibu linalokubalika.

Kupata mwenzi wa maisha ni sawa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tofauti na ile ya Zanzibar au Kenya, hii inahusisha maridhiano kati ya macho na moyo. Macho yanaona na kuvutiwa, moyo unaguswa.

Kwa mantiki hiyo, ni kosa kujiaminisha kwamba unapenda ikiwa moyo wako haujakubali. Lakini haiwezekani moyo ukapenda ikiwa macho yamekataa. Macho yanaona, ubongo unatafsiri halafu moyo unapokea.

Umemkubali kwa jinsi alivyo, hapo ni sawa. Lakini unatakiwa kujiuliza maswali mengine 50 kuhusu yeye, halafu upate majibu ambayo yanaridhiwa na kila upande. Usifanye chaguo ambalo litaufanya moyo wako usinyae.

ONYO: Kamwe usiruhusu moyo wako usinyae kwa sababu hiyo ni sawa na ugonjwa hatari. Moyo unaposhindwa kufanya kazi yake barabara, hutema sumu ndani kwa ndani ambayo inaweza kukusababishia matatizo makubwa nap engine kukua haraka. Kuwa makini.

Maswali ya kujiuliza ni haya;
KABISA NIMEMRIDHIA?
Hapa kuna maana kuwa tayari umemkubali lakini jiulize tena na tena kuhusu yeye. Kama kuna shaka ndani yake usilazimishe, badala yake pitisha uamuzi mmoja pale ambapo umeona majibu yanakuja chanya kila ulipojiuliza.
NIPO TAYARI?

Binadamu hajakamilika, pengine kuna mambo yanayomzunguka mwenzi wako. Watu wa pembeni wanazungumza, lakini pia si ajabu ikawa kuna vikwazo vya kifamilia. Swali hili linachukua nafasi katika eneo hilo.

Jiulize kama upo tayari kukabiliana na presha za watu na ndugu ilimradi uhakikishe unambakiza kwenye himaya yako. Isitokee ukasema upo tayari leo lakini baada ya muda ukamfanya mwenzako ajute.

Jiridhishe leo kwa faida ya maisha yenu kwa jumla. U-tayari wako uwe na maana kuwa hata miaka 10 ijayo, utamtetea popote kwamba ulilolisimamia leo, utaendelea nalo kila siku mpaka Mungu atakapoamua kutumia mamlaka yake kuwatenganisha.

SITAMCHOKA?
Usithubutu kupenda kwa fahari ya jicho la leo. Nimekutaka ujadiliane na moyo wako kwa sababu kuna vitu vingi vya kujiridhisha kabla ya kuamua kuzama moja kwa moja. Ikiwa kuna dalili kwamba ipo siku utamchoka usithubutu kumpotezea muda.

Mwenzi wa maisha ina maana ni mtu wa furaha yako kwa maisha yako yote. Kwamba yeye atakuwa sehemu ya maisha yako. Hivyo, huyo hatakiwi kuchokwa bali anastahili hifadhi ya kudumu moyoni kuliko mwingine.

Mtu ambaye unaweza kumchoka mbele ya safari utamjua tu kwa kujiuliza. Ikiwa kuna penzi la kweli, hakika utaona ni kiasi gani linavyomea. Hutakuwa na shaka ya aina yoyote juu yake na utakubali kwamba furaha anayokupa leo, haitabadilika.

Kuna penzi la usanii, kama hilo ndilo linalokuongoza basi ni vema ujitenge. Nina maana kuwa endapo humpendi kutoka moyoni ila unamdanganya, jitenge haraka kwa sababu mbele utamchoka, utamsumbua na utamsaliti.
VIPI MAUDHI YAKE?

Mpenzi wako ni binadamu siyo malaika. Hivyo ndivyo na wewe ulivyo. Nyoye ni viumbe dhaifu, kwahiyo kila mmoja ana upungufu wake lakini kwako ni vizuri ukajiuliza endapo maudhi yake unaweza kuyavumilia.

Ni kosa kubwa kufukia mashimo kwa yale yanayokukwaza kwa mwenzi wako. Amua leo, ikiwa unaona kila kitu kinawezeka, kwamba pamoja na kasoro zake lakini anavumilika na upo tayari kufanya naye maisha, basi nenda mbele zaidi.

Ruhusu moyo wako uamue katika maudhi yanayokusumbua kutoka kwa mwenzi wako. Moyo wako upime kwamba ubora wake upo juu kuliko kasoro zinazokutibua. Hapo unangoja nini tena? Mng’ang’anie huyo huyo, ukitaka asiye na kasoro utasubiri sana.
NAWEZA KUONGOZANA NAYE?

Hili siyo swali la kudharau hata kidogo. Kuna watu wengi wapo kwenye ndoa lakini hata siku moja huwezi kuona wameongozana na wenzi wao. Kuna vitu vingi vinawasibu, angalia nawe yasije yakakukuta kwenye safari yako.

Akuridhishe kwa muonekano wake, kwahiyo uwe na imani kuwa hata ukiongozana naye barabarani utakuwa ni mwenye kujiamini. Hapa kuna la kujifunza zaidi. Hakuna maana kuwa utashindwa kuongozana naye kwa sababu ni mbaya, la hasha!

Inawezekana mwenzi wako ni mzuri sana, kwahiyo mkiongozana watu huwashangaa. Pia, mwenzi wako anaweza kuwa na umbo kubwa, mnene, hivyo macho ya watu barabarani yanaweza kukufanya ukajiona mnyonge.
Itaendelea wiki ijayo

Sunday, November 14, 2010

Maumivu ya kuachana wakati bado mnapendana unayajua?

Ni jambo la kumshukuru Mungu kutukutanisha tena kupitia safu hii ambayo lengo lake kuu ni kuelimishana na kukumbushana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Wiki iliyopita nilizungumzia mada iliyokuwa inawagusa moja kwa moja wanawake na suala la kujirahisi kwa wanaume. Nilieleza namna ambavyo miili yao ina thamani kubwa kuliko wanavyofikiri.

Hivyo basi, wanaume ambao wanatakiwa kupata fursa ya kuichezea miili yao wawe wale ambao wamewapenda kwa dhati na mioyo yao imeridhia. Wasifanye hivyo kwa tamaa ya pesa ama kitu kingine.

Baada ya kugusia kidogo mada hiyo ya wiki iliyopita, leo nizungumzie jambo moja ambalo limekuwa likiniumiza sana na kujiuliza kwanini huwa linatokea. Wakati najaribu kupitiapitia mtandao, niliona waraka wa barua pepe ambayo dada mmoja alikuwa akimtumia mpenzi wake wa zamani. Naomba niuandike hapa chini kama ulivyo kabla ya kuendelea.

Kwako John, nilikupenda sana mpenzi wangu, nawe ulionesha mapenzi ya dhati kwangu lakini kwa kile kilichotokea ambacho siwezi kukiandika hapa, tuliachana wakati bado nakupenda. Wakati mwingine nahisi sikustahili kukuacha lakini hilo linakuja akilini mwangu nikiwa tayari nimefanya uamuzi.

Kurudi kwako tena nahisi hutanikubalia, nabaki nalia. Nakutakia maisha mema lakini jua nimekuacha wakati nakupenda.
Ni mimi Janeth.

Janeth anaumia kwa uamuzi aliochukua wa kuachana na mpenzi wake wakati bado walikuwa wanapendana. Yawezekana alifanya hivyo kutokana na hasira ama kasoro ambazo alizibaini kwa mpenzi wake. Labda nilizungumzie hili la kasoro za wapenzi wetu kama chanzo cha wengi kuachana wakati bado wanapendana.

Tuelewe kwamba, kila binadamu ana kasoro huku zikitofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Kama ni mfuatiliaji mzuri wa safu hii utakumbuka niliwahi kuandika makala inayosema kuwa, tuvumiliane hasa tunapobaini kuwa wapenzi tulio nao wana kasoro fulani.

Wakati nikiandika hivyo, leo nalazimika kulizungumzia hili la namna ya kukabiliana na kasoro za wapenzi wetu kutokana na ushauri alioomba mmoja wa wasomaji wangu.

“Naitwa Rehema, nina mpenzi wangu ambaye tunapendana sana lakini miongoni mwa vitu ambavyo vinatufanya tusilifurahie penzi letu ni kasoro za kiuanaume alizo nazo. Ananipa kila ninachokitaka lakini tunapokuwa faragha mambo hayaendi.

“Imefika wakati amekuwa akitoa machozi na kunieleza kuwa, tatizo lake la kimaumbile (jogoo kutoamka) analishangaa kwani humjia anapokutana na mimi tu. Mwenyewe anadai aliyemfanyia mchezo huo ni mpenzi wake wa zamani. Nampenda lakini kasoro hiyo aliyo nayo mpenzi wangu inaniweka njia panda.”

Wapo watu wengi walio katika uhusiano usiokuwa na furaha kutokana na kasoro ndogo ndogo ama kubwa walizonazo wapenzi wao. Katika hili kwanza lazima tujue kwamba, hakuna binadamu aliyekamilika!

Leo hii unaweza kumuacha mpenzi wako kutokana na kutokuridhisha katika tendo la ndoa tu lakini ukaingia kwenye uhusiano na mtu mwingine ambaye yeye ni ‘mzuri’ faragha ila ni mlevi na mkorofi.

Ndiyo maana siku zote tumekuwa tukitakiwa kuzifanyia tathmini kasoro walizonazo wapenzi wetu kabla ya kuchukua hatua ya kuwaacha au uamuzi mwingine usiofaa.

Tufahamu kwamba, mapenzi ndiyo yanayotangulia, moyo wako unapompenda fulani hauangalii kasoro alizo nazo kwasababu moyo wenyewe unajua kuwa, kasoro alizonazo mtu haziuzuii kupenda.

Ndiyo maana leo hii unamkuta mwanamke yuko katika uhusiano na mwanaume mkorofi kupita maelezo lakini mwanamke huyo anakueleza kuwa, hawezi kumuacha kwakuwa moyo wake umependa. Anachokifanya ni kumvumilia ili kutokwenda kinyume na matakwa ya moyo wake.

Kwa mfano, mpenzi wako hayajui mapenzi! Hiyo ni kasoro kubwa ambayo wapenzi wengi wamekuwa wakiilalamikia. Mara ooh! Mpenzi wangu hayajui mambo, ni goigoi awapo uwanjani. Mara ooh! Mpenzi wangu akienda mzunguko mmoja tu hoi.

Sawa! Hayo ni mambo yanayokukwaza lakini ndiyo uchukue hatua ya kumuacha kweli? Sidhani kama utakuwa ni uamuzi sahihi na wale wanaowaacha wapenzi wao eti kwasababu wana kasoro fulani wanadhihirisha kutokuwa na mapenzi ya dhati.
Kasoro za wapenzi wetu haziwezi kuwa sababu sahihi za kuwaacha, kama moyo wako umempenda huyo uliye naye na yeye akaonesha kukupenda, kasoro alizo nazo zichukulie kama changamoto kwako.

Tambua kwamba unaweza kubahatika kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hana kasoro kubwa za kukukwaza lakini akawa hana mapenzi ya kweli, matokeo yake akawa mtu wa kukuliza kila siku.

Cha msingi, unapokuwa katika uhusiano na mtu kwa muda fulani ni lazima utabaini kasoro alizo nazo lakini na yeye pia atakuwa amekusoma na kukujua vizuri. Kama kweli mnapendana, mnachotakiwa kufanya ni kuangalia njia sahihi za kukabiliana na kasoro zenu. Zifanyieni kazi, rekebishaneni, yatafutieni ufumbuzi matatizo yenu ili mwisho kasoro hizo zisije zikawafanya mkaachana wakati bado mnapendana kwani inauma sana.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena hapa wiki ijayo.

Tuesday, November 9, 2010

Hajui ukipatacho, haelewi thamani yake ndiyo maana anakwambia hakufai- 3

Ni mada ambayo inajenga zaidi kujiamini kwa kila mtu kwa mwenzi wake. Kutanguliza nafsi yako ni kitu muhimu mno. Tupo katika sehemu ya tatu na ndiyo ya mwisho.
Naamini katika Kitchen Party lakini sikubaliani na dhana kuwa ili mwanamke awe bora kwenye mapenzi au ndoa yake ni vema apitie katika mafundisho ya namna hiyo.

Inahitaji busara za kufikiria na kuamua. Kutambua wewe mwenyewe unahitaji nini kisha upime na kile ambacho unaambiwa. Hata kumhudumia mwenzi wako chumbani ufundishwe?
Mapenzi si taaluma kwamba kuna tabaka la watu fulani ambalo limefuzu. Kila mtu anaweza, kwahiyo unaweza pia. Muhimu ni kujitambua, kung’amua maeneo yako hatarishi na kujiweka wazi.

Kuna ugumu gani kumueleza mwenzi wako kuwa eneo hili na lile ndiyo muafaka? Unadhani anaweza kuja malaika kutoka mbinguni wa kutii kiu yako? Ni wewe na yeye, ndiyo maana mpo ‘spesho’.

Mwanaume kwenda Bag Party, sipingi lakini ni utamaduni ambao hauna matunda mema. Kinachoweza kukupa uhakika wa kumudu penzi lako ni kuamini katika kile kinachokuunganisha na mwenzi wako.

Unatakiwa ujue sababu ya wewe kuwa na mwenzako kabla ya mwingine yeyote. Faida zake zifike kwake. Kasoro mnarekebishana wawili, tena katika eneo ambalo hukutani na mtu mwingine yeyote. Mapenzi yana maana kubwa!

Ni katika hilo, ndiyo maana ya kutoa pointi kwamba hupaswi kuamini katika maneno ya watu ili kuchukua uamuzi hasi au chanya kuhusu mwandani wako. Kila kitu kipo ndani yako, hakuna mtu wa nje anayejua zaidi.

Inaposemwa sikitiko la mahaba linashinda msiba, maana yake ni kuwa ukifiwa utalia na wengi lakini maumivu ya moyo yanayotokana na mapenzi, yatakuuma peke yako. Hayupo atakayelia kilio cha kweli pamoja na wewe.

Hatatokea mtu ambaye anaweza kuhisi kile ambacho kinakutoa machozi. Tunakataa utengano lakini hoja ya msingi hapa ni kuwa tafsi ya mapenzi ni kitu chenye ubaguzi, kwamba “ni sisi wawili tu, kwa ajili yetu, furaha yetu na kila kinachotuhusu!”

MWENZI WAKO NI NAMBA MOJA
Haihitaji kufuzu elimu ya chekechea kujua hili. Hata yule ambaye hajapita kabisa shule anafahamu kwamba binadamu anavyoishi, kila kipindi anajikuta anapoteza marafiki na kupata wengine.

Inalazimishwa na hali halisi ya maisha. Unaposoma makala haya, mwisho wa aya hii fumba macho ukumbuke ni marafiki wangapi ambao ulikuwa nao, ukashibana nao mpaka ukadhani wao ni sehemu ya maisha yako?

Bila shaka ni wengi, baada ya hapo jiulize swali lingine, wote hao wapo wapi? Unakuja kugundua kwamba kuna baadhi hata hujui walipo katika huu mgongo wa ardhi.Mmekwishapotezana, kila mtu anaangalia ustaarabu wake.

Kwa mwenzi wa maisha yako, mtaishi mpaka kufa. Mtaambata kila mahali kwa sababu maisha yako hayakamilishi tafsiri yake bila uwepo wake, kwa maana hiyo hupaswi kudanganyika kwa hoja dhaifu za kukuchonganisha naye.

USIACHE MBACHAO KWA MSALA UPITAO
Nilikujengea hoja yenye mantiki kwamba kila hatua kuna aina ya marafiki unawapoteza na kupata wapya. Hii inamaana kuwa hutakiwi kuwadharau lakini usiwape nafasi kuzidi hata ile ambayo wewe humpa mwandani wako.

Nina mfano wa mtu aliyekuwa anateswa mno na marafiki wa mke wake. Jamaa kila siku anaonya kuhusu aina fulani ya watu lakini mke hasikii. Ndiyo kwanza maneno yanaingia sikio la kulia kabla hayajafika sikio la kushoto yanapotea.

Mume akawa analalamika kuwa anazidiwa nguvu na marafiki wa mwenzi wake, kwamba hana kitu chochote cha kuamua endapo marafiki wa mke wake watasema chochote. Sikitiko la mume mwisho likampa shinikizo la damu! Mapenzi yanatesa!

Mume akalalamika kuwa akimkataza mke wake kutoka, wakija marafiki wataondoka naye hata kama itakuwa ni usiku. Wakati mwingine wanatoa maneno ya kuudhi, “achana naye, kwani mwanaume peke yake!”

Ni kosa kubwa kwa sababu wanaopotosha ni watu wa kupita. Mume au mke ndani ya nyumba upo naye leo na kwa uweza wa Mungu, ni kifo ndicho kitakachowatenganisha. Huyo mpigadebe hajui kinachokutuliza kwake.

Hii ni kwa mume na mke, kwani wapo wanaume wengi hawajui kutunza hisia za wenzi wao. Wamelemaa kwa hulka za mfumo dume, matokeo yake wanaharibu. Usisikilize ya watu, mwache akushauri lakini si kukupangia maisha.

Tafuta watu wanaojua kutoa ushauri wa kitaalamu na si kudandia kila mtu. Wengine hawajui tafsiri ya kuumizwa na mapenzi, kwahiyo si ajabu akakwambia umuache! Kumbuka kwamba utakapokuwa unalia, moyo unauma, machozi yanatoka, unakosa usingizi hatokuwepo. Ni maisha yako!

Friday, November 5, 2010

Hajui ukipatacho, haelewi thamani yake ndiyo maana anakwambia hakufai.

Nimekuwa nikilieleza hili mara kwa mara kwamba mapenzi yanapoangaliwa kila upande, unakuja kupata jibu kwamba hakuna uhusiano uliokamilika. Muhimu kwako ni kumkubali mwenzi wako kama alivyo na kumpa heshima yake ya asimilia mia moja.

Kumkubali ni kutambua ujazo wake moyoni mwako. Hapa nikiwa na maana kwamba wewe mwenyewe unakuwa umejiridhisha kuwa unampenda kwa alama zote, hivyo umeamua kufanya naye maisha.

Uvumilivu unahitajika kwa kila mmoja, lakini busara iliyo wazi ni kwamba hutakiwi kuishi kwa kutazama makosa ya mwenzi wako. Mwisho wa siku naye ni binadamu, kwahiyo unaishi na kiumbe chenye damu na moyo, siyo malaika.

Unashauriwa kumtambua mwenzi wako kwa jinsi alivyo na kujua jinsi ya kurekebisha kasoro zake. Uwe wa kwanza kujua udhaifu wake na kumkosoa kwa vipimo, siyo kwa sababu Mungu amekujalia mdomo na sauti ndiyo kila siku upayuke.

Una kila sababu ya kuzungumza na kutaka ushauri kuhusu mwandani wako lakini siyo nidhamu ‘kumvua nguo’. Hapa napitisha hoja kuwa kutoa kipaumbele kwa mwenzi wako ni sehemu ya nidhamu ya kimapenzi.

Wiki iliyopita nilikuonesha mifano. Unatakiwa ujiridhisha mwenyewe kuwa pamoja na kasoro zake bado anastahili kupewa hifadhi ya moyo wako. Lakini kuna huyo anayekuambia uachane naye. Je, unampa nafasi gani?

Jibu unalo, lakini kwangu nikikushauri kitaalamu kama muongozo ni kuwa unatakiwa uangalie moyo wako unakupa jibu gani kuliko kusikiliza rafiki anachosema. Ujazo wake kwenye moyo wako haujui na hatambui ni kiasi gani utaathirika ukimkosa.

Je, rafiki anakuja na hoja au ngonjera? Anaponda badala ya kukupa njia ya kufanya. “Ooh, achana naye, kwanza yule malaya sana atakuua.” Somo hili likupe sababu ya kuwaona marafiki wenye uelewa wa hisia kwa sababu utakapokosa usingizi usiku kwa sababu ya mawazo hatakuwepo.

Kama mwenzi wako hafai au anafaa, jibu lipo ndani ya kuta za moyo wako. Ndiyo maana linapokuja suala la kupokea ushauri wa kimapenzi, unatakiwa umuone mtu ambaye ana sifa ya kutoa ushauri. Tafuta washauri na siyo wapondaji.

Unaweza kuwaazima masikio marafiki zako, wakampaka mwenzi wako badala ya kukupa ufumbuzi wa kile kinachokusumbua. Mwisho ukaona yao ni mazuri halafu kwa hasira ukafikia uamuzi wa kuachana naye, utajuta baadaye. Itakutesa zaidi baada ya kubaini kuwa mmoja wa waliokuwa wanamponda ndiye kamchukua.

MJALI MWENZI WAKO KULIKO CHOCHOTE
Hiyo ni nidhamu kuu. Hapo unashauriwa kitaalamu kuwa mwenzi wako kama mtu ‘spesho’ zaidi wa maisha yako, unapaswa kwenda naye kwa maewaleno. Kusikilizana na kupeana muongozo wa kila siku katika maisha.

Fikiria kuwa una marafiki wengi, ndugu na jamaa mlioshibana lakini mwishoni unapotaka kulala, hurejea nyumbani na kujifunika shuka moja na mwenzi wako. Bila shaka unaona ni kwa namna gani huyo anashikilia kipengele nyeti cha maisha yako.

Dunia katika pointi ya maradhi, hususan Ukimwi na magonjwa mengine ya ngono, ni yeye ndiye anayeweza kukuweka huru. Damu yako ikawa salama, kwani kinyume chake asipokuwa makini, anaweza kuchetuka, akachetukia maradhi, mwisho wa siku akakuletea gonjwa uhangaike nalo.

Kwa maana hiyo ni mlinzi wa maisha yako. Unalala fofofo karibu yake na mpo wawili tu chumbani, ukiamka hujikuti na jeraha lolote. Usipomjali mtu wa namna hiyo unataka thamani yake ukampe nani?

Kuna kundi la watu huwatanguliza marafiki kuliko wenzi wao. Yaani katika pande mbili, mwenzi wako anasema hili, halafu wewe unasikiliza neno la rafiki kwanza. Hilo ni kosa kubwa ambalo ni rahisi kuyeshusha upendo.

Ni bora unapoona mwenzi wako anaongea kitu ambacho unaona hakifai, utumie muda wako kumuweka sawa na akuelewe. Usithubutu kufanya kinyume chake kama hakuelwi. Mwisho kabisa, ukiona mwenzio ana wasiwasi, jiepushe na hicho anachokihofia au mfanye aondoe mashaka.

Mwenzi wako anahisi kuna mtu unatoka naye kimapenzi. Fahamu kuwa hilo linamtesa moyoni, huwezi kujua kaambiwa na wangapi mpaka akaja kukuuliza. Zifanye fikra zake ziwe huru kwa kumuelewesha mpaka aelewe au jiepushe na huyo mtu.

Itaendelea wiki ijayo…

Usijirahisi, penzi na mwili wako vina thamani kubwa.

Tumshukuru Mungu kwa kutukutanisha tena kupitia safu hii nikiamini kwamba kwa rehema zake umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.

Wiki hii mpenzi msomaji nataka kuzungumzia mada ambayo inawagusa wanawake wasiojiheshimu, wanaopenda kujirahisi kwa kila mwanaume bila kujua kuwa mapenzi na miili yao vina thamani kubwa.

Sote ni mashahidi kwamba huko mtaani wapo wanawake ambao kwa kweli wanawadhalilisha wenzao, wamekuwa ni wa kuchukuliwa na kila mwanaume anayewatongoza. Kwa kifupi hawawezi kusema ‘no’, wanachokiangalia ni pesa tu.

Hali hii imewafanya wanaume wenye nazo kuwatumia kadri wanavyotaka. Unawakuta wale vijana wanaojiita ‘mapedeshee’ leo yuko na huyu na anamfanya anavyotaka na kesho yuko na mwingine, ndivyo wanavyoishi. Hii ni hatari sana lakini ninachotaka kuzungumzia leo ni kwa wale wanawake wanaoshindwa kukabiliana na usumbufu wanaoupata kutoka kwa wanaume wakware.

Kwa tathmini yangu, kila mwanamke ni mzuri na kila mwanamke anapendwa lakini tujue kwamba, nafasi ya kupenda kwa upendo ule wa dhati inakwenda kwa mtu mmoja tu.

Cha ajabu unamkuta msichana yuko na mpenzi wake lakini bado macho yake yako juu juu. Si mtu wa kutulia na mtu mmoja na kwa wengine hata hiyo nafasi ya mtu mmoja hawaitoi.

Yaani wao ndiyo wale wanaoitwa ‘cha wote’, kila mwanaume akiwa na pesa zake anapewa nafasi ya kuumiliki mwili kwa muda. Inafika wakati najiuliza wanaofanya hivyo wanaijua thamani ya miili yao? Nadhani hawajui kwani kama wangekuwa wanajua wasingekuwa tayari kumvulia nguo kila mwanaume kwani madhara yake ni makubwa.

Linapokuja suala la madhara anayoweza kuyapata mwanamke anayejirahisi kwa wanaume, magonjwa yanachukua nafasi kubwa. Kuchanganya wapenzi kunaweza kukuweka katika mazingira mazuri ya kuambukizwa magonjwa yanayoweza kuyaathiri maisha yako kwa kiasi kikubwa.

Achilia mbali hilo, unapokuwa ni mtu wa kujirahisi kwa wanaume hata heshima yako katika jamii unayoishi inapungua. Hakuna atakayekuheshimu na itafika wakati hata wanaume ambao umewapa penzi watakuona siyo hasa pale ambapo watakutana wanaume wawili ambao wote umetembea nao. Watakuona hujatulia, na ni malaya.

Lakini pia naomba niseme kwamba, thamani ya mwili wako ni kubwa. Ifike wakati mwanaume unayediriki kumpa uhuru katika mwili wako awe ni yule uliyempenda kwa dhati na si kwa tamaa ya pesa au kitu kingine.

Wapo wanawake ambao kila wanakopita licha ya kuwa wamevaa nguo wanaonekana wako uchi. Hii ni kwa sababu, idadi kubwa ya wanaume wanawajua walivyo kuanzia kwenye nywele hadi kwenye kucha. Kujirahisi kwao ndiko kumewafanya wafikie hatua hiyo.
Nini cha kujifunza hapa?

Uvumilivu
Hili ni kwa wale ambao bado hawajabahatika kuwapata wapenzi wenye mapenzi ya dhati kwao. Yawezekana wanakutongoza wanaume wengi kila mmoja akidai anakupenda lakini kwa uelewa wako ukabaini ni ‘wasanii’ wanaotaka kukuchezea kisha kukuacha.

Kama uko katika hali hiyo, kuwa mvumilivu amini ipo siku utampata yule ambaye atakupenda kwa dhati na kukipata kile ambacho umekikosa kwa muda mrefu.

Uaminifu
Uko na mpenzi wako na anakupa unachokitaka, tulia! Yawezekana kuna wanaume ambao wanajua kabisa uko na mpenzi lakini bado wanakuchomekea. Usikubali wakurubuni kama kweli uliyenaye unampenda. Kamwe usiwachekee, wape maneno ambayo hata kesho hawatathubutu kukuambia maneno ya kijinga.

Thamani yako
Wanawake wengi wanaojirahisi wanaonekana hawajui thamani yao. Hawaoni madhara ya kujiachia kwa kila mwanaume anayewatokea. Huu ni ulimbukeni kwani mwanamke ana heshima kubwa kiasi kwamba mwili wake si wa kuguswa hovyo, achilia mbali kuchezewa. Lakini wengi hawako hivyo, wanashikwa sehemu zao nyeti na wanaume wanachekelea, yaani kwao ni poa tu. Ukiwa hivyo jua unajidhalilisha.

Kujiheshimu
Mwanamke kamili ni yule anayejiheshimu na kuwaheshimu wengine. Ukijaribu kufanya uchunguzi utabaini kuwa, asilimia kubwa ya wanawake wanaojiheshimu hata usumbufu kutoka kwa wanaume wakware siyo mkubwa. Wanaume wanaogopa kuwatongoza na wale wanaodiriki kufanya hivyo ni wale wasiojali. Jiheshimu na uuheshimu mwili wako. Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo.

Wednesday, October 27, 2010

MJUE WMENZI WAKO VEMA....

Mjue mwenzi wako vema kuepusha migogoro
Na NICO TRAC.

WATU wametofautiana tabia kutokana na sababu mbalimbali, zilizo kubwa ni malezi tuliyopata baada ya kuzaliwa hadi umri walionao pia kutoka kwenye asili zetu, kwa maana ya wazazi wetu nk.

Ilivyo ni kuwa wakati tunazaliwa, ni kama tulikuwa kaseti tupu, ambayo baadaye ilikuwa na kazi kubwa ya kurekodi kila kilichokuwa kikipita au kufanyika mbele yetu.

Hata hivyo haijalishi umezaliwa familia yenye tabia gani, au wewe sasa una tabia zinazokera au kufurahisha kiasi gani, jambo la msingi sana kwako ni kujichunguza, kisha kuchukua hatua, kuachana na tabia zenye kukera.

Ili kujua kama mwenendo wa tabia zako unakera au kufurahisha, ni rahisi, muulize mwenzi wako, kama anafurahia mwenendo wa tabia zako au kuna mambo yanakwenda kinyume.

Katika maisha ni jambo la msingi sana kujifahamu ulivyo.

Kinyume na hili ni vigumu sana kuwa na maendeleo au maelewano na watu wanaokuzunguka. Nilikuwa nafuatilia maendeleo ya watu duniani, niliona asilimia kubwa ya watu ambao wamekuwa na maisha mazuri ya furaha ni wale ambao wamekuwa 'social'...wenye kujichanganya na kucheka na watu.

Ni kweli kuna tofauti kubwa ya tabia za watu, kwa mfano watu wanaofahamika kama Melancolin, hawa kimsingi wanafahamika kuwa ni wenye uwezo mkubwa kiakili.

Watu wa aina hii kwa kawaida huwa hawana maneno mengi, wana moyo wa huruma hasa kuwasaidia wale ambao wanakuwa katika matatizo na kwa ujumla wana huruma wala hawapendi kuona wengine wakionewa.

Katika uhusiano, watu wa aina hii huhitaji kuwa na watu wenye tabia tofauti na huwa na uwezo wa kuishi nao vizuri. Hata hivyo baadhi ya watu hawa wana tatizo la kutojiamini au kutochangamkia kufanya mambo makubwa, kwa imani kuwa yote yatawezekana kesho.

Shida iliyo kwa watu wa aina hii ni wepesi wa kukata tamaa. Na zaidi ya yote wanapenda sana kutiwa moyo. Pia wanasifika kwa uwezo wao wa uvumilivu na kwa ujumla wanaeleweka kuwa ni kundi la watu wenye busara na hekima nyingi.

Watu wa aina hii huwa wanahesabu upendo wa dhati kwa kufanyiwa sio yale wanayoambiwa.

Je, mwenzi wako ni mtu wa aina gani? Ni suala la msingi sana kama nilivyosema, kupata muda wa kumuelewa kwa kina mwenzi wako na kuchukua hatua. Ni kuwa hata kama mwenzi wako ana hali gani kitabia, kinachohitajika ni kwa wawili kukaa pamoja na kuelezana ukweli wa vile inavyotakiwa iwe.

Katika maisha kuna kundi la watu wengine, liitwalo 'flagmetic', hawa wanafahamika kwa uwezo wao mkubwa wa kutosifia mambo ya wenzao. Watu wa aina hii wanapenda sana kuzungumza jambo baada ya kutafiti kwa kina, ndio kusema kuwa katika mazungumzo yao, mara nyingi utakuwa yametawaliwa na mifano au tafiti za hapa na pale.

Inaamini kuwa watu wenye kundi hili, ndio wenye uwezo mkubwa katika suala zima la upelelezi, hii ni kwa sababu tu ya uwezo wao mkubwa wa kupenda kufanya jambo fulani baada ya kutafiti kwa kina, ingawa kwa mwonekano wanaweza kuonekana kana kwamba ni watu wasio na uwezo mkubwa katika kufanya mambo.

Jambo jingine la kufahamu kuhusu watu hawa ni kuwa si wepesi wa kuamini watu wengine. Hata kama kwa mfano yuko na mume au mkewe, si rahisi kumuamini kwa asilimia mia, ndio maana utaona labda wengine wanawaficha wenzi wao akaunti za benki walizonazo nk, ni kwa sababu tu wameumbwa hivyo.

Wanasifika kwa kupokea, lakini ni wazito kutoa. Je, mwenzi wako yukoje? Angalia, tafiti kwa kina alivyo, kisha jua alivyo, hii itakusaidia kujua namna ya kuishi naye pasipo mikwaruzo.

Lakini zaidi ya yote, hawa ndugu, ni maarufu wa kusamehe hata kama utamtendea baya kiasi gani, ni kwa sababu tu kimsingi ni kuwa hawajali, yaani hata kama utamfanyia baya vipi, yeye si mwenye kujali.

Pia ni suala la msingi ni kufahamu wengi wa walio kwenye kundi hili, aaah suala la kukufokea hadharani, ni la kawaida, wala hawaoni kama ni kosa. Zaidi ya yote, hata kama utawasema vibaya kiasi gani, ni kama unajisumbua, kwa sababu hawaumizwi na maneno ya watu.

Lakini pia wanayo sifa nyingine, huenda ikawa ni nzuri, kwamba wana uwezo mkubwa wa kusuruhisha migogoro ya wengine, ingawa wao wanaweza kuwa na yao kwa ndani nk.

Maisha yao kwa ujumla yana ufanisi wa wastani, hii inatokana na wakati mwingine kusaidia wengine kupita kiasi hadi wanajikuta wanatoa siri ambazo pengine zingewasaidia wenyewe kuwa na maisha bora yaliyojaa mafanikio.

Ndio nasema msingi wa kukufanya uwe na maelewano mazuri na watu, ni kujuana tabia na kujua kumbe watu wametofautiana na kama mwenzi wangu yuko hivi na vile, ninachotakiwa kufanya ni hiki na kile ili maendeleo na maelewano ya kweli yaweze kupatikana.

Kuna kundi la watu wengine wanaitwa Sanguine, hawa wanasifa sana kwa ucheshi. Ni wazuri kwa kazi za mapokezi...eeeh kuna wengine hata ukisalimiana naye tu, tayari anacheka, anatabasamu nk, kana kwamba labda tayari mlishawahi kuonana naye miaka mingi iliyopita, ingawa yaweza kuwa ndio mara yenu ya kwanza kukutana.

Ni maarufu wa kuongea, yaani yuko tayari kunyimwa chakula, mruhusu aongee na watu. Ni muhimu kulifahamu mapema hili. Itasaidia kuepusha migogoro nk.

Monday, October 25, 2010

Sauti inavyoweza kuamsha au kuondoa hisia za mapenzi

Wataalamu wa masuala ya uhusiano wa kimapenzi wanaamini ndani ya sauti kuna nguvu ya mapenzi ambayo mtu akiitumia anaweza kuamsha hisia za mwenzake na kuongeza chumvi ya huba katika penzi lake.

Hii haijalishi awe mwanamke au mwanaume. Watafiti mbalimbali kwenye karne ya 14 -18 walibaini uwezo wa sauti katika kutuliza au kuusumbua ubongo na hivyo kuanzisha mafundisho juu ya umuhimu wa sauti.

Katika hali ya kawaida, sehemu yenye kelele huleta wasiwasi mwilini ambao baadaye humfanya mtu aonekane mchovu au akumbwe na mshtuko wa moyo. Kambi nyingi za kijasusi duniani kelele ni sehemu ya mateso kwa mtuhumiwa, washukiwa wengi hufungiwa kwenye vyumba vidogo na hatimaye kusumbuliwa na milio mikali ambayo huwakera na kujikuta wakitoa siri za matukio yao mabaya.

Lakini sauti hizo hizo zikiwa tulivu huvutia, ndiyo maana sehemu za starehe hasa hoteli za kitalii, mbuga za wanyama hupambwa na sauti za ndege au milio ya taratibu ya vinubi, muziki na hata ngoma. Haya ndiyo maajabu ya sauti mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku.

Natambua kuna aina nyingi za sauti zenye kukera na kuvutia, lakini leo najikita kwenye sauti zetu sisi kama binaadamu katika kukuza au kubomoa uhusiano wetu wa kimapenzi. Kama nilivyosema sauti kali inakera na tulivu inafariji.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo cha Albright, Pennsylvannia nchini Marekani umebaini kuwepo kwa hisia kali za mapenzi kwenye sauti tulivu. Katika ripoti yake iliyotolewa na mtafiti Susan Hughes ilielezwa kwamba wanaume na wanawake huvutiwa na sauti tulivu kwenye mawasiliano yao.

Nanukuu maneno ya Susan: “Wakati mwanamke anaposhusha sauti yake mithili ya mtu anayenong’oneza, mwili wa mwanaume husisimka zaidi na kunasa hisia za mapenzi, tofauti na anapoongea kwa sauti ya juu.” Jambo hili si la kupuuza bali ni muhimu katika kukuza mapenzi.

Wapenzi wengi wamekuwa hawafahamu umuhimu wa sauti tulivu kwenye mapenzi, si ajabu ukamkuta mwanamke anaongea na mumewe au mpenzi wake kama yuko baa, sauti kali utadhani wanagombana.

Hili ni tatizo la kimapenzi kusema kweli. Tunashauri unapokuwa na mpenzi wako hata kama wewe ni ‘kinega’ au baunsa mtaani shusha kidogo sauti ili kumletea mwenzako msisimko.

Katika kumalizia somo hili, naomba nitoe jaribio kwa wapenzi, litakaloweza kulifanya somo hili kuaminika. Kwanza- Wapenzi wanaoishi pamoja waitane na kuketi au kulala pamoja, halafu kila mmoja azingatie utulivu wa sauti yake katika mawasiliano. Baada ya hapo waanze kuzungumzia mapenzi yao kwa muda usiopungua dakika 20 yatakayotokea waniambie.

PILI –Wanaoishi mbalimbali, wao wachukue picha za wenza wao au wavute taswira kwa muda fulani kisha waanze kuzungumza kutumia simu zao kwa sauti tulivu muda wa dakika 20, nao waniambie matokeo yake.

Baada ya hapo siku ya pili warudie mazungumzo yao lakini kwa kutumia sauti za juu kama watu wanaobwatuka. Matokeo yake waniambie pia. Naamini tutakuwa tumejifunza umuhimu wa kutumia sauti za chini tunapokuwa kwenye mawasiliano ya kimapenzi.

Nashauri wapenzi wajifunze kutumia sauti tulivu za kimapenzi wanapozungumza na wenza wao, waache kuongea kwa sauti kali, zenye kukera na wapunguze kelele zisizokuwa za msingi hasa wanapokuwa faragha.

Kama unapenda mafundisho haya, jipatie kitabu cha TITANIC No3 kwa wauza magezeti kote nchini kwa shilingi 3,000 tu. Humo utapata mada, meseji za mapenzi pamoja na chombezo mbili zilizotikisa wasomaji, VUVUZELA KITANDANI na MSHAURI WA MAPENZI.

Unapoumizwa na penzi zingatia haya

MU hali gani mabibi na mabwana kwa kukutana tena kwenye safu yetu ya kujuzana mawili matatu kuhusu maisha yetu ya kila siku. Japo leo nilikuwa nimeandaa mada nyingine.

Lakini wakati najiandaa kuandika alikuja rafiki yangu wa karibu ambaye aliniletea matatizo mengi kutoka kwa mzazi mwenzake, ambaye wamezaa watoto wawili na wanaishi pamoja kama mke na mume.

Moja ya matatizo hayo ambayo yamejaa kwenye baadhi ya nyumba tunazoishi kwa mwanamke kukosa heshima wala woga kwa kufanya mambo kwa kujiamulia kama vile anajimiliki mwenyewe.

Mwenza wake amekuwa si mkweli mwenye matukio yanayoonesha kukosekana kwa uaminifu katika uhusiano wao. Amekuwa akitoka bila ruhusa na kurudi akiwa amelewa na aulizwapo huwa mkali.

Kibaya zaidi kilichomtokea siku ya jumamosi baada ya kukorofishana mwanamke yule alimtumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu, kuwa mtoto mdogo wa mwaka mmoja siyo wake naye atafute wa kwake.

Nina imani hali hii imewakumba watu wengi ambao kila siku uendelea kuumia wakati wenzao wanaendelea kufurahia maisha. Matukio haya utokea wakati mwanamke anapokuwa na uhakika huna sauti kwake kwa kuonyesha udhaifu mbele yake.

Siwezi kuwa na upendeleo kwa kusema tabia hizi ni za wanawake peke yao, hata baadhi ya wanaume nao wapo wenye tabia hizi.

Kwa vile kona hii majibu yake huwa hayalengi upande mmoja, nilipenda nielezee kwa wote na kila mmoja asome kama ni yeye yamemkuta au yakitaka kukuta ufanyeje. Naanza kwa kusema ukiona vitu vyote hivi ujue ndani ya uhusiano au ndoa yako hakuna mapenzi bali kinachowaongoza ni mazoea. Na tatizo lilianza kama mzaha kwa kulifumbia macho kutokana na udhaifu mbele ya mwenzako kwa kuyaacha yote yaliyokwenda kinyume.

Nasema hivi kwa
maana gani?
Kila anayefuatilia kona hii atakubaliana na mada nilizozitoa kuhusu penzi la kweli na mnafiki wa mapenzi. Ila leo nataka niongezee kidogo ili tuelewe tupo wapi, tumetoka wapi na tunaelekea wapi katika mapenzi.

Utajiuliza inakuwaje mtu anakubali kufanyiwa hivi na kubakia kulalamika bila kuchukua hatua yoyote? Ukiona mtu au ukijiona upo hivi basi ujuwe wewe ni mtumwa wa mapenzi kwa kuongozwa na mapenzi na si wewe kuyaongoza.
Mtumwa wa mapenzi yukoje?

Mtumwa wa mapenzi ni yule anayependa kwa kumuona mpenzi wake ni mzuri na hawezi kumpenda mwingine kuliko yeye. Na hii utokea kwa kuamini kumpata ilikuwa ni bahati na wala si uwezo wako binafsi. Ukifikia hatua hii hata kumkanya kwa baya huwezi.

Watu wa aina hii huburuzwa na mapenzi kwa mpenzi wake kufanya jambo lolote bila woga kwa kuamini mpenzi wake anampenza kupindukia yaani ‘hageuzi’. Watu hawa huumia zaidi ya kung’olewa jino bila ganzi. Uamini wakiachwa ndiyo mwisho wao wa kupenda au kupendwa. Napenda kusema haya machache ili usiwe mtumwa wa mapenzi:

Kwanza: Unatakiwa wewe ndiye uwe dereva wa kuyaongoza mapenzi siyo yenyewe yakuongoze.
Pili: Unatakiwa uwe na maamuzi sahihi ya moyo wako hasa panapotokea kufanyiwa kosa la makusudi kwa kulikemea kwa nguvu zote.

Tatu: Usikubali mpenzi wako akuumize kwa sababu unampenda kwa vile mapenzi ni kupendana kufarijiana na si kuumizana au kutesana.

Nne: Angalia katika mapenzi yako nini kimezidi, faida au hasara, chukua kilichozidi.
Tano: Jiamini kuwa kupenda au kupendwa kwako si bahati
Sita: Muweke chini mpenzio na kumueleza matatizo yake ambayo yanakwenda kinyume na watu waliokubaliana kuishi pamoja, kama hata kuwa muelewa, tafuta usuluhisho kwa watu mbalimbali wenye busara na ikishindikana ni wajibu wako wa kulivunja penzi.

Hapa naomba nieleweke kulivunja penzi iwe suruhisho la mwisho kabisa kama hakutapatikana suruhu ya aina yoyote. Na kulivunja penzi hakikisha umekubaliana na moyo wako. Jiepushe na kumkumbuka aliyeachana naye ili asiendelee kukuumiza. Siku zote adui ya moyo yako hawezi kupata nafasi moyoni mwako.

Mwisho: Jipange vizuri kabla ya kuanzisha penzi jipya ili usirudie kosa la awali. Na mwisho kabisa napenda kuwakumbusha wanawake wazuri wote au wanaume wenye fedha kuwa wakati ukuta na hakuna marefu yasiyo na ncha. Samahani kwa kosa la makusudi ni unafiki, samahani siku zote ni uungwana lakini haipunguzi machungu.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

Friday, October 22, 2010

Usibabaike na kukuita kwake sweetie, honey, swali ni je, anakupenda?

Kwa nguvu zake Mwenyezi Mungu mimi ni mzima wa afya njema na ninaendelea vyema na majukumu yangu ya kila siku likiwemo hili la kukumbushana na kuelimishana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Kabla sijaenda mbali, katika mada hii ambayo naamini itawagusa wengi, ni vizuri kama tutajiuliza kwa pamoja maana ya mapenzi! Mapenzi humaanisha nini hasa? Je, ni usanii au ni tofauti na hivyo?

Katika hili, kila mmoja anaweza kuwa na maana yake lakini binafsi naweza kuyatafsiri mapenzi kama hisia ambazo zipo moyoni mwa mtu kwenda kwa mwingine. Hisia hizi ili ziweze kuwa mapenzi ni lazima ziwe na ukweli na za dhati huku moyo ukiwa na nafasi kubwa katika hilo.

Hii ndiyo maana ya haraka haraka ya mapenzi. Kwamba unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu uliyetokea kumpenda, hupaswi kuwa na mtu mwingine kwakuwa, kufanya hivyo ni kuunyima haki moyo wako.

Pamoja na ukweli huo juu ya mapenzi, lakini hivi sasa maana halisi ya mapenzi imepotoshwa kabisa, imebadilishwa huku kila mmoja akiyachukulia kama anavyoona yeye na kujiona yuko sahihi. Mapenzi ya siku hizi yamejaa usanii mtupu, hayana ukweli, kila siku ni maumivu juu ya maumivu. Kwanini watu wanaharibu maana halisi ya mapenzi?

Tunajua matatizo mengi yanaweza kutukumba iwapo tutakuwa siyo waaminifu kwa wale tuliowaeleza kwamba tunawapenda. Tunajua kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja ni kujitafutia matatizo ambayo mwisho wa siku tunaweza kujikuta tunajuta na kutoa machozi lakini bado tunaendelea kufanya hivyo.

Tunaelewa wazi inavyouma kusikia mpenzi wako ana mtu mwingine lakini sisi mbona tunawafanyia wenzetu hivyo? Hatuoni kwamba kwa kufanya hivyo tunakwenda kinyume kabisa na maana halisi ya mapenzi?

Unaweza kujifanya mjanja sana kwa kuunganisha wapenzi zaidi ya kumi huko gizani ukiamini huonekani na hakuna matatizo yoyote ambayo unaweza kuyapata, kumbe unajidanganya maana kuna siku utakuja kuumbuka kwa kuonekana kwako si muaminifu!

Ila sasa kitu ambacho kimekuwa kikinisikitisha ni pale mtu anapoona dalili za wazi wazi kwa mpenzi wake kwamba si muaminifu lakini bado anaendelea kumng’ang’ania eti kwa maelezo kwamba anampenda sana na hayuko tayari kumkosa katika maisha yake. Jamani inakuwaje mtu ameshabaini yuko ndani ya penzi la kitapeli lakini bado haambiwi wala hasikii?

Najua wapo walio katika penzi la kitapeli kwa kuhisi wanapendwa kutokana na kuitwa majina ya kimahaba lakini hawajui. Ila kuna hawa ambao kutokana na ulimbukeni wao wanajua kabisa wameingia ‘choo cha kike’ lakini hawataki kutoka.

Naomba niseme tu kwamba, wapo watu ambao utapeli ndiyo asili yao, yaani mapenzi yao wanayaendesha kiujanja ujanja. Ni walaghai ambao inafika wakati hujifanyisha kuwa wana mapenzi ya kweli lakini ukichunguza sana unakuta hamna kitu.

Ukiwa na bahati mbaya ya kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu wa aina hii ni vigumu sana kudumu naye na hata kama mtadumu, hamuwezi kufurahia maisha yenu.

Unamkuta mwanamke ni mwepesi sana kukuita majina mazuri ya kimapenzi kama vile sweetie, honey na mengineyo ya aina hii lakini ungebahatika kuingia kwenye moyo wake ungekutana na hali tofauti, yaani hakupendi kama unavyodhani. Hawa wapo wengi lakini ni vigumu sana kuwabaini.

Yaani wao kuwasaliti wapenzi wao ndiyo maisha yao ya kila siku lakini ngoja nikuulize wewe unayemsaliti mpenzi wako. Hivi unavyomfanyia mwenzako hivyo unadhani yeye hana moyo? Hivi hujui kuwa mwenzako anakupenda kwa mapenzi yake yote na amekuchagua wewe uwe wa kumpa furaha? Siku akijiua kwa sababu yako utakuwa katika hali gani? Hebu acha utapeli wako!

Kuwa muwazi, dhihirisha kile kilichomo moyoni mwako. Acha kujifanyisha, kama unampenda kiukweli mfanye mwenza wako aamini hivyo lakini kama humpendi basi mwache huru atafute mwingine mwenye msimamo na uendelee na maisha yako.

Saturday, October 9, 2010

Kupendwa ni bahati, usikubali muachane kirahisi

Jamani tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kutukutanisha tena kupitia safu hii namba moja kwa kuandika makala nzito zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Wiki iliyopita nilizungumzia jinsi unavyoweza kukabiliana na hali ya mpenzi wako kuhisi humpendi au unamsaliti wakati kiukweli hisia zake ni potofu.

Wiki hii nitazungumzia umuhimu wa wapenzi kuhakikisha kila mmoja anachukua nafasi yake kulilinda penzi lao na kulifanya lidumu milele. Nimelazimika kuandika makala haya kutokana na ukweli kwamba, wapo watu waliojaaliwa kupendwa lakini ukiwaangalia hawaoneshi kujali wala kuchukulia kupendwa huko kama bahati kwao.

Nasema ni bahati kwasababu, huko mtaani wapo watu ambao wanaishi maisha yasiyokuwa na furaha kwasababu hawajapata watu wa kuwaita honey, sweetie na majina mengine ya namna hiyo.

Hawana furaha kwakuwa, hawajawapata watu wa kuwabembeleza wanapokuwa katika huzuni, watu wa kuwajali na kuwapa furaha. Ni jambo linalowaumiza wengi sana na ndio maana tunaona kasi ya wanawake kutongoza wanaume inaongezeka tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Sasa hebu jiulize wewe ambaye umebahatika kuwa na mtu anayeonesha kukupenda kwa dhati, unafanya nini kuhakikisha hakuachi? Si suala la kuchukulia juu juu kwa sababu madhara yake katika maisha yako ni makubwa tofauti na vile unavyofikiria.

Waweza kutoonesha kujali leo kwa sababu wapo watu wanaokusumbua wakidai wanakupenda lakini je, una uhakika kwamba wanachokuambia ni kweli? Si kwamba wanakutamani tu? Uliye naye kama kweli unampenda ndiye wa kumng’ang’ania kwa kumjali, kumthamini na kumuonesha upendo wa hali ya juu.

Wengine wasikufanye ukapunguza mapenzi yako kwa mpenzi wako kwasababu ikitokea siku akaamua kukuacha unaweza kujikuta unajuta na kuona bora hata ungeendelea kuwa naye huyo uliyekuwa unamchukulia poa.

Mnatofautiana katika hili na lile? Hiyo ni kawaida katika maisha ya kimapenzi, kikubwa ni kufanya jitihada za kuondoa tofauti zenu haraka kwa kuombana msamaha kila mnapokoseana kisha kuendelea na safari yenu ya mapenzi.

Hata kama mpenzi wako kakukosea, usichukue uamuzi wa haraka, mpe nafasi ya kujiangalia, naamini akigundua kakukosea atakuomba msamaha na wewe usijisikie vibaya kumsamehe.

Akijenga katabia ka’ kukukosea kila mara akitarajia kukuomba msamaha na kusamehewa, mfikirie upya na kuona kama unaweza kuendelea kumvumilia lakini mara nyingi mtu anayekukosea kila wakati penzi lake linakuwa la mashaka.

Hakupi ulichokitarajia? Unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi kuna kitu unachokitarajia kutoka kwa huyo uliyempenda. Wakati mwingine waweza kukosa baadhi ya vitu kutoka kwake lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kumfanyia makusudi ili muachane.

Yeye kama binadamu ana mapungufu, anachokupatia jaribu kuridhika nacho hasa kama anaonesha kukupenda kwa dhati, mengine yatakuja kwa baraka za Mungu.

Yote haya najaribu kuyasema kwasababu kupendwa ni bahati na ukibahatika kuwa kwenye uhusiano unaokufanya angalau ukawa na furaha katika maisha yako, usikubali mambo madogo madogo yakawatenganisha. Uvumilivu uchukue nafasi yake lakini pia kusameheana iwe sehemu ya maisha yenu ya kila siku.

Wazungu wanasema, “Something is better than nothing’ wakimaanisha kwamba, kitu kidogo ulichonacho ni bora kuliko kutokuwa na kitu kabisa. Wewe umebahatika kuingia katika uhusiano kama sio katika ndoa kabisa.

Naamini utakuwa na tofauti kubwa sana na yule ambaye anajitongozesha lakini watu wanampotezea na kama atafanikiwa basi anaweza kujikuta anachezewa kisha anaachwa.

Kumkosa mpenzi kwakweli inauma na inaweza kuyatingisha maisha yako. Lakini sasa kama wewe ni miongoni mwa wale wanaotamani kuwa na wapenzi lakini mpaka sasa hawajabahatika, huna sababu ya kutoa machozi yako. Amini siku itafika na yawezekana utakayempata atakuwa ndiye mwenza wako wa maisha.

Naombeni kwa leo niishie hapo, unachotakiwa kukiingiza katika akili yako leo kupitia makala haya ni kuhakikisha huachani na mpenzi wako uliyempenda kirahisi. Na kama unaona hana nafasi katika moyo wako, msipotezeane muda! .