Wiki iliyopita utakumbuka nilianza kuandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari hapo juu. Nimefanya hivyo kwakuwa, wapo watu wengi ambao wanaachwa na wapenzi wao lakini wanafanya mambo ambayo wenyewe wanadhani yatawasaidia kuwapa amani moyoni mwao, kumbe wanazidi kujitesa.
Wiki hii nitamalizia baadhi ya mambo ambayo unatakiwa kuyaepuka pale unapopigwa kibuti na mpenzi wako uliyetokea kumpenda.
Kudhani ni mwanaume tofauti
Kama huyo uliyempenda kakutosa, amini utampata mwingine ambaye huenda akawa mzuri zaidi na mwenye mapenzi ya dhati kwako kuliko huyo wa awali.
Hutakiwi kumuwaza sana na ukiona anakujia akilini mwako, jiulize tu kwamba kwani yeye ni nani hasa? Ana tofauti gani na wanaume wengine ambao wanatamani kuwa nawe?
Usimfuatefuate
Ni lazima utajisikia hali fulani utakapokuwa unaonana na mpenzi wako wa zamani ambaye ulikuwa ukimpenda. Kwa maana hiyo jaribu kuepuka kuonana naye mara kwa mara ili kujiondoshea maumivu.
Wapo ambao wameachwa lakini bado wanaendelea kuwafuatilia wapenzi wao, kuwapigia simu na kuwatumia sms tena wakati wa usiku. Ya nini kujipa presha za bure? Mbaya zaidi eti asipopokea au kujibu meseji zako unaumia, hivi ‘inahuu?’ Mimi nadhani kaamua kukuacha na wewe jaribu kumpotezea.
Usikumbuke mazuri yake, kumbuka mabaya yake
Wapo wengi wameachwa na wapenzi wao lakini maisha yao bado yameendelea kuwa mazuri na ya furaha. Walichokifanya ni kujaribu kusahau yale mazuri waliokuwa wakifanyiwa na wapenzi wao na kuyakumbuka mabaya waliyokuwa wanatendewa.
Utakapokuwa unayakumbuka yale mazuri aliyokutendea lazima utakuwa unaumia na matokeo yake kutamani kurudiana naye wakati tayari kishakutoa katika moyo wake.
Usimgeuze adui yako wala rafiki
Hata kama kakuumiza vipi, huwezi jua sababu ya yeye kukuacha kwani kila kinachotokea hapa ulimwenguni kimepangwa na Mungu. Hivyo basi, kama ulikuwa unamheshimu endelea kumheshimu, msalimie pale unapoonana naye na hata pale atakapokuwa anahitaji msaada wako, msaidie kama unavyowasaidia watu wengine.
Lakini katika hili usije ukakubali kujenga mazingira ya yeye kukuchukulia kama rafiki. Kumbuka kwa waliotokea kuwa wapenzi na wakaachana hawawezi kuwa marafiki bali itakuwa ni unafiki. Hata hivyo, kama utamfanya mpenzi wako wa zamani rafiki unaweza kuutibua uhusiano wako mpya.
Hii ni kwa sababu, wanaotaka kukutamkia kuwa wanakupenda wanaweza kushindwa kufanya hivyo kwa kuhisi bado uko na yule wa zamani. Lakini pia hata utakapokuwa umempata mpenzi mpya, hataamini kuwa nyie mmebaki marafiki tu bali anaweza kuhisi siku moja moja mnakumbushia enzi zenu. Kikubwa usimfanye rafiki wala adui.
Kufuatilia maisha yake ya kimapenzi
Wapo ambao wameachwa lakini bado wanaendelea kufuatilia maisha ya kimapenzi ya wapenzi wao wa zamani. Yanini kutaka kujua kwamba saa hivi yuko na nani?Ukijua itakusaidia nini? Muache aendelee na maisha yake.
Ndugu zangu, mpaka kufikia hapo naomba niweke kituo. Kikubwa ni kwamba, unapoachwa na mtu jaribu kuishi maisha yako. Ndiyo! Kwanini ukubali mtu akuharibie maisha yako? Usikubali kabisa kushindwa kula, kufanya kazi zako vizuri, kuchanganyikiwa kisaikolojia eti kwa sababu mpenzi wako uliyempenda kakuacha.
No comments:
Post a Comment