Wednesday, October 27, 2010

MJUE WMENZI WAKO VEMA....

Mjue mwenzi wako vema kuepusha migogoro
Na NICO TRAC.

WATU wametofautiana tabia kutokana na sababu mbalimbali, zilizo kubwa ni malezi tuliyopata baada ya kuzaliwa hadi umri walionao pia kutoka kwenye asili zetu, kwa maana ya wazazi wetu nk.

Ilivyo ni kuwa wakati tunazaliwa, ni kama tulikuwa kaseti tupu, ambayo baadaye ilikuwa na kazi kubwa ya kurekodi kila kilichokuwa kikipita au kufanyika mbele yetu.

Hata hivyo haijalishi umezaliwa familia yenye tabia gani, au wewe sasa una tabia zinazokera au kufurahisha kiasi gani, jambo la msingi sana kwako ni kujichunguza, kisha kuchukua hatua, kuachana na tabia zenye kukera.

Ili kujua kama mwenendo wa tabia zako unakera au kufurahisha, ni rahisi, muulize mwenzi wako, kama anafurahia mwenendo wa tabia zako au kuna mambo yanakwenda kinyume.

Katika maisha ni jambo la msingi sana kujifahamu ulivyo.

Kinyume na hili ni vigumu sana kuwa na maendeleo au maelewano na watu wanaokuzunguka. Nilikuwa nafuatilia maendeleo ya watu duniani, niliona asilimia kubwa ya watu ambao wamekuwa na maisha mazuri ya furaha ni wale ambao wamekuwa 'social'...wenye kujichanganya na kucheka na watu.

Ni kweli kuna tofauti kubwa ya tabia za watu, kwa mfano watu wanaofahamika kama Melancolin, hawa kimsingi wanafahamika kuwa ni wenye uwezo mkubwa kiakili.

Watu wa aina hii kwa kawaida huwa hawana maneno mengi, wana moyo wa huruma hasa kuwasaidia wale ambao wanakuwa katika matatizo na kwa ujumla wana huruma wala hawapendi kuona wengine wakionewa.

Katika uhusiano, watu wa aina hii huhitaji kuwa na watu wenye tabia tofauti na huwa na uwezo wa kuishi nao vizuri. Hata hivyo baadhi ya watu hawa wana tatizo la kutojiamini au kutochangamkia kufanya mambo makubwa, kwa imani kuwa yote yatawezekana kesho.

Shida iliyo kwa watu wa aina hii ni wepesi wa kukata tamaa. Na zaidi ya yote wanapenda sana kutiwa moyo. Pia wanasifika kwa uwezo wao wa uvumilivu na kwa ujumla wanaeleweka kuwa ni kundi la watu wenye busara na hekima nyingi.

Watu wa aina hii huwa wanahesabu upendo wa dhati kwa kufanyiwa sio yale wanayoambiwa.

Je, mwenzi wako ni mtu wa aina gani? Ni suala la msingi sana kama nilivyosema, kupata muda wa kumuelewa kwa kina mwenzi wako na kuchukua hatua. Ni kuwa hata kama mwenzi wako ana hali gani kitabia, kinachohitajika ni kwa wawili kukaa pamoja na kuelezana ukweli wa vile inavyotakiwa iwe.

Katika maisha kuna kundi la watu wengine, liitwalo 'flagmetic', hawa wanafahamika kwa uwezo wao mkubwa wa kutosifia mambo ya wenzao. Watu wa aina hii wanapenda sana kuzungumza jambo baada ya kutafiti kwa kina, ndio kusema kuwa katika mazungumzo yao, mara nyingi utakuwa yametawaliwa na mifano au tafiti za hapa na pale.

Inaamini kuwa watu wenye kundi hili, ndio wenye uwezo mkubwa katika suala zima la upelelezi, hii ni kwa sababu tu ya uwezo wao mkubwa wa kupenda kufanya jambo fulani baada ya kutafiti kwa kina, ingawa kwa mwonekano wanaweza kuonekana kana kwamba ni watu wasio na uwezo mkubwa katika kufanya mambo.

Jambo jingine la kufahamu kuhusu watu hawa ni kuwa si wepesi wa kuamini watu wengine. Hata kama kwa mfano yuko na mume au mkewe, si rahisi kumuamini kwa asilimia mia, ndio maana utaona labda wengine wanawaficha wenzi wao akaunti za benki walizonazo nk, ni kwa sababu tu wameumbwa hivyo.

Wanasifika kwa kupokea, lakini ni wazito kutoa. Je, mwenzi wako yukoje? Angalia, tafiti kwa kina alivyo, kisha jua alivyo, hii itakusaidia kujua namna ya kuishi naye pasipo mikwaruzo.

Lakini zaidi ya yote, hawa ndugu, ni maarufu wa kusamehe hata kama utamtendea baya kiasi gani, ni kwa sababu tu kimsingi ni kuwa hawajali, yaani hata kama utamfanyia baya vipi, yeye si mwenye kujali.

Pia ni suala la msingi ni kufahamu wengi wa walio kwenye kundi hili, aaah suala la kukufokea hadharani, ni la kawaida, wala hawaoni kama ni kosa. Zaidi ya yote, hata kama utawasema vibaya kiasi gani, ni kama unajisumbua, kwa sababu hawaumizwi na maneno ya watu.

Lakini pia wanayo sifa nyingine, huenda ikawa ni nzuri, kwamba wana uwezo mkubwa wa kusuruhisha migogoro ya wengine, ingawa wao wanaweza kuwa na yao kwa ndani nk.

Maisha yao kwa ujumla yana ufanisi wa wastani, hii inatokana na wakati mwingine kusaidia wengine kupita kiasi hadi wanajikuta wanatoa siri ambazo pengine zingewasaidia wenyewe kuwa na maisha bora yaliyojaa mafanikio.

Ndio nasema msingi wa kukufanya uwe na maelewano mazuri na watu, ni kujuana tabia na kujua kumbe watu wametofautiana na kama mwenzi wangu yuko hivi na vile, ninachotakiwa kufanya ni hiki na kile ili maendeleo na maelewano ya kweli yaweze kupatikana.

Kuna kundi la watu wengine wanaitwa Sanguine, hawa wanasifa sana kwa ucheshi. Ni wazuri kwa kazi za mapokezi...eeeh kuna wengine hata ukisalimiana naye tu, tayari anacheka, anatabasamu nk, kana kwamba labda tayari mlishawahi kuonana naye miaka mingi iliyopita, ingawa yaweza kuwa ndio mara yenu ya kwanza kukutana.

Ni maarufu wa kuongea, yaani yuko tayari kunyimwa chakula, mruhusu aongee na watu. Ni muhimu kulifahamu mapema hili. Itasaidia kuepusha migogoro nk.

No comments: