Monday, October 25, 2010

Sauti inavyoweza kuamsha au kuondoa hisia za mapenzi

Wataalamu wa masuala ya uhusiano wa kimapenzi wanaamini ndani ya sauti kuna nguvu ya mapenzi ambayo mtu akiitumia anaweza kuamsha hisia za mwenzake na kuongeza chumvi ya huba katika penzi lake.

Hii haijalishi awe mwanamke au mwanaume. Watafiti mbalimbali kwenye karne ya 14 -18 walibaini uwezo wa sauti katika kutuliza au kuusumbua ubongo na hivyo kuanzisha mafundisho juu ya umuhimu wa sauti.

Katika hali ya kawaida, sehemu yenye kelele huleta wasiwasi mwilini ambao baadaye humfanya mtu aonekane mchovu au akumbwe na mshtuko wa moyo. Kambi nyingi za kijasusi duniani kelele ni sehemu ya mateso kwa mtuhumiwa, washukiwa wengi hufungiwa kwenye vyumba vidogo na hatimaye kusumbuliwa na milio mikali ambayo huwakera na kujikuta wakitoa siri za matukio yao mabaya.

Lakini sauti hizo hizo zikiwa tulivu huvutia, ndiyo maana sehemu za starehe hasa hoteli za kitalii, mbuga za wanyama hupambwa na sauti za ndege au milio ya taratibu ya vinubi, muziki na hata ngoma. Haya ndiyo maajabu ya sauti mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku.

Natambua kuna aina nyingi za sauti zenye kukera na kuvutia, lakini leo najikita kwenye sauti zetu sisi kama binaadamu katika kukuza au kubomoa uhusiano wetu wa kimapenzi. Kama nilivyosema sauti kali inakera na tulivu inafariji.

Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo cha Albright, Pennsylvannia nchini Marekani umebaini kuwepo kwa hisia kali za mapenzi kwenye sauti tulivu. Katika ripoti yake iliyotolewa na mtafiti Susan Hughes ilielezwa kwamba wanaume na wanawake huvutiwa na sauti tulivu kwenye mawasiliano yao.

Nanukuu maneno ya Susan: “Wakati mwanamke anaposhusha sauti yake mithili ya mtu anayenong’oneza, mwili wa mwanaume husisimka zaidi na kunasa hisia za mapenzi, tofauti na anapoongea kwa sauti ya juu.” Jambo hili si la kupuuza bali ni muhimu katika kukuza mapenzi.

Wapenzi wengi wamekuwa hawafahamu umuhimu wa sauti tulivu kwenye mapenzi, si ajabu ukamkuta mwanamke anaongea na mumewe au mpenzi wake kama yuko baa, sauti kali utadhani wanagombana.

Hili ni tatizo la kimapenzi kusema kweli. Tunashauri unapokuwa na mpenzi wako hata kama wewe ni ‘kinega’ au baunsa mtaani shusha kidogo sauti ili kumletea mwenzako msisimko.

Katika kumalizia somo hili, naomba nitoe jaribio kwa wapenzi, litakaloweza kulifanya somo hili kuaminika. Kwanza- Wapenzi wanaoishi pamoja waitane na kuketi au kulala pamoja, halafu kila mmoja azingatie utulivu wa sauti yake katika mawasiliano. Baada ya hapo waanze kuzungumzia mapenzi yao kwa muda usiopungua dakika 20 yatakayotokea waniambie.

PILI –Wanaoishi mbalimbali, wao wachukue picha za wenza wao au wavute taswira kwa muda fulani kisha waanze kuzungumza kutumia simu zao kwa sauti tulivu muda wa dakika 20, nao waniambie matokeo yake.

Baada ya hapo siku ya pili warudie mazungumzo yao lakini kwa kutumia sauti za juu kama watu wanaobwatuka. Matokeo yake waniambie pia. Naamini tutakuwa tumejifunza umuhimu wa kutumia sauti za chini tunapokuwa kwenye mawasiliano ya kimapenzi.

Nashauri wapenzi wajifunze kutumia sauti tulivu za kimapenzi wanapozungumza na wenza wao, waache kuongea kwa sauti kali, zenye kukera na wapunguze kelele zisizokuwa za msingi hasa wanapokuwa faragha.

Kama unapenda mafundisho haya, jipatie kitabu cha TITANIC No3 kwa wauza magezeti kote nchini kwa shilingi 3,000 tu. Humo utapata mada, meseji za mapenzi pamoja na chombezo mbili zilizotikisa wasomaji, VUVUZELA KITANDANI na MSHAURI WA MAPENZI.

No comments: