Friday, November 5, 2010

Usijirahisi, penzi na mwili wako vina thamani kubwa.

Tumshukuru Mungu kwa kutukutanisha tena kupitia safu hii nikiamini kwamba kwa rehema zake umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.

Wiki hii mpenzi msomaji nataka kuzungumzia mada ambayo inawagusa wanawake wasiojiheshimu, wanaopenda kujirahisi kwa kila mwanaume bila kujua kuwa mapenzi na miili yao vina thamani kubwa.

Sote ni mashahidi kwamba huko mtaani wapo wanawake ambao kwa kweli wanawadhalilisha wenzao, wamekuwa ni wa kuchukuliwa na kila mwanaume anayewatongoza. Kwa kifupi hawawezi kusema ‘no’, wanachokiangalia ni pesa tu.

Hali hii imewafanya wanaume wenye nazo kuwatumia kadri wanavyotaka. Unawakuta wale vijana wanaojiita ‘mapedeshee’ leo yuko na huyu na anamfanya anavyotaka na kesho yuko na mwingine, ndivyo wanavyoishi. Hii ni hatari sana lakini ninachotaka kuzungumzia leo ni kwa wale wanawake wanaoshindwa kukabiliana na usumbufu wanaoupata kutoka kwa wanaume wakware.

Kwa tathmini yangu, kila mwanamke ni mzuri na kila mwanamke anapendwa lakini tujue kwamba, nafasi ya kupenda kwa upendo ule wa dhati inakwenda kwa mtu mmoja tu.

Cha ajabu unamkuta msichana yuko na mpenzi wake lakini bado macho yake yako juu juu. Si mtu wa kutulia na mtu mmoja na kwa wengine hata hiyo nafasi ya mtu mmoja hawaitoi.

Yaani wao ndiyo wale wanaoitwa ‘cha wote’, kila mwanaume akiwa na pesa zake anapewa nafasi ya kuumiliki mwili kwa muda. Inafika wakati najiuliza wanaofanya hivyo wanaijua thamani ya miili yao? Nadhani hawajui kwani kama wangekuwa wanajua wasingekuwa tayari kumvulia nguo kila mwanaume kwani madhara yake ni makubwa.

Linapokuja suala la madhara anayoweza kuyapata mwanamke anayejirahisi kwa wanaume, magonjwa yanachukua nafasi kubwa. Kuchanganya wapenzi kunaweza kukuweka katika mazingira mazuri ya kuambukizwa magonjwa yanayoweza kuyaathiri maisha yako kwa kiasi kikubwa.

Achilia mbali hilo, unapokuwa ni mtu wa kujirahisi kwa wanaume hata heshima yako katika jamii unayoishi inapungua. Hakuna atakayekuheshimu na itafika wakati hata wanaume ambao umewapa penzi watakuona siyo hasa pale ambapo watakutana wanaume wawili ambao wote umetembea nao. Watakuona hujatulia, na ni malaya.

Lakini pia naomba niseme kwamba, thamani ya mwili wako ni kubwa. Ifike wakati mwanaume unayediriki kumpa uhuru katika mwili wako awe ni yule uliyempenda kwa dhati na si kwa tamaa ya pesa au kitu kingine.

Wapo wanawake ambao kila wanakopita licha ya kuwa wamevaa nguo wanaonekana wako uchi. Hii ni kwa sababu, idadi kubwa ya wanaume wanawajua walivyo kuanzia kwenye nywele hadi kwenye kucha. Kujirahisi kwao ndiko kumewafanya wafikie hatua hiyo.
Nini cha kujifunza hapa?

Uvumilivu
Hili ni kwa wale ambao bado hawajabahatika kuwapata wapenzi wenye mapenzi ya dhati kwao. Yawezekana wanakutongoza wanaume wengi kila mmoja akidai anakupenda lakini kwa uelewa wako ukabaini ni ‘wasanii’ wanaotaka kukuchezea kisha kukuacha.

Kama uko katika hali hiyo, kuwa mvumilivu amini ipo siku utampata yule ambaye atakupenda kwa dhati na kukipata kile ambacho umekikosa kwa muda mrefu.

Uaminifu
Uko na mpenzi wako na anakupa unachokitaka, tulia! Yawezekana kuna wanaume ambao wanajua kabisa uko na mpenzi lakini bado wanakuchomekea. Usikubali wakurubuni kama kweli uliyenaye unampenda. Kamwe usiwachekee, wape maneno ambayo hata kesho hawatathubutu kukuambia maneno ya kijinga.

Thamani yako
Wanawake wengi wanaojirahisi wanaonekana hawajui thamani yao. Hawaoni madhara ya kujiachia kwa kila mwanaume anayewatokea. Huu ni ulimbukeni kwani mwanamke ana heshima kubwa kiasi kwamba mwili wake si wa kuguswa hovyo, achilia mbali kuchezewa. Lakini wengi hawako hivyo, wanashikwa sehemu zao nyeti na wanaume wanachekelea, yaani kwao ni poa tu. Ukiwa hivyo jua unajidhalilisha.

Kujiheshimu
Mwanamke kamili ni yule anayejiheshimu na kuwaheshimu wengine. Ukijaribu kufanya uchunguzi utabaini kuwa, asilimia kubwa ya wanawake wanaojiheshimu hata usumbufu kutoka kwa wanaume wakware siyo mkubwa. Wanaume wanaogopa kuwatongoza na wale wanaodiriki kufanya hivyo ni wale wasiojali. Jiheshimu na uuheshimu mwili wako. Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo.

No comments: