Friday, November 5, 2010

Hajui ukipatacho, haelewi thamani yake ndiyo maana anakwambia hakufai.

Nimekuwa nikilieleza hili mara kwa mara kwamba mapenzi yanapoangaliwa kila upande, unakuja kupata jibu kwamba hakuna uhusiano uliokamilika. Muhimu kwako ni kumkubali mwenzi wako kama alivyo na kumpa heshima yake ya asimilia mia moja.

Kumkubali ni kutambua ujazo wake moyoni mwako. Hapa nikiwa na maana kwamba wewe mwenyewe unakuwa umejiridhisha kuwa unampenda kwa alama zote, hivyo umeamua kufanya naye maisha.

Uvumilivu unahitajika kwa kila mmoja, lakini busara iliyo wazi ni kwamba hutakiwi kuishi kwa kutazama makosa ya mwenzi wako. Mwisho wa siku naye ni binadamu, kwahiyo unaishi na kiumbe chenye damu na moyo, siyo malaika.

Unashauriwa kumtambua mwenzi wako kwa jinsi alivyo na kujua jinsi ya kurekebisha kasoro zake. Uwe wa kwanza kujua udhaifu wake na kumkosoa kwa vipimo, siyo kwa sababu Mungu amekujalia mdomo na sauti ndiyo kila siku upayuke.

Una kila sababu ya kuzungumza na kutaka ushauri kuhusu mwandani wako lakini siyo nidhamu ‘kumvua nguo’. Hapa napitisha hoja kuwa kutoa kipaumbele kwa mwenzi wako ni sehemu ya nidhamu ya kimapenzi.

Wiki iliyopita nilikuonesha mifano. Unatakiwa ujiridhisha mwenyewe kuwa pamoja na kasoro zake bado anastahili kupewa hifadhi ya moyo wako. Lakini kuna huyo anayekuambia uachane naye. Je, unampa nafasi gani?

Jibu unalo, lakini kwangu nikikushauri kitaalamu kama muongozo ni kuwa unatakiwa uangalie moyo wako unakupa jibu gani kuliko kusikiliza rafiki anachosema. Ujazo wake kwenye moyo wako haujui na hatambui ni kiasi gani utaathirika ukimkosa.

Je, rafiki anakuja na hoja au ngonjera? Anaponda badala ya kukupa njia ya kufanya. “Ooh, achana naye, kwanza yule malaya sana atakuua.” Somo hili likupe sababu ya kuwaona marafiki wenye uelewa wa hisia kwa sababu utakapokosa usingizi usiku kwa sababu ya mawazo hatakuwepo.

Kama mwenzi wako hafai au anafaa, jibu lipo ndani ya kuta za moyo wako. Ndiyo maana linapokuja suala la kupokea ushauri wa kimapenzi, unatakiwa umuone mtu ambaye ana sifa ya kutoa ushauri. Tafuta washauri na siyo wapondaji.

Unaweza kuwaazima masikio marafiki zako, wakampaka mwenzi wako badala ya kukupa ufumbuzi wa kile kinachokusumbua. Mwisho ukaona yao ni mazuri halafu kwa hasira ukafikia uamuzi wa kuachana naye, utajuta baadaye. Itakutesa zaidi baada ya kubaini kuwa mmoja wa waliokuwa wanamponda ndiye kamchukua.

MJALI MWENZI WAKO KULIKO CHOCHOTE
Hiyo ni nidhamu kuu. Hapo unashauriwa kitaalamu kuwa mwenzi wako kama mtu ‘spesho’ zaidi wa maisha yako, unapaswa kwenda naye kwa maewaleno. Kusikilizana na kupeana muongozo wa kila siku katika maisha.

Fikiria kuwa una marafiki wengi, ndugu na jamaa mlioshibana lakini mwishoni unapotaka kulala, hurejea nyumbani na kujifunika shuka moja na mwenzi wako. Bila shaka unaona ni kwa namna gani huyo anashikilia kipengele nyeti cha maisha yako.

Dunia katika pointi ya maradhi, hususan Ukimwi na magonjwa mengine ya ngono, ni yeye ndiye anayeweza kukuweka huru. Damu yako ikawa salama, kwani kinyume chake asipokuwa makini, anaweza kuchetuka, akachetukia maradhi, mwisho wa siku akakuletea gonjwa uhangaike nalo.

Kwa maana hiyo ni mlinzi wa maisha yako. Unalala fofofo karibu yake na mpo wawili tu chumbani, ukiamka hujikuti na jeraha lolote. Usipomjali mtu wa namna hiyo unataka thamani yake ukampe nani?

Kuna kundi la watu huwatanguliza marafiki kuliko wenzi wao. Yaani katika pande mbili, mwenzi wako anasema hili, halafu wewe unasikiliza neno la rafiki kwanza. Hilo ni kosa kubwa ambalo ni rahisi kuyeshusha upendo.

Ni bora unapoona mwenzi wako anaongea kitu ambacho unaona hakifai, utumie muda wako kumuweka sawa na akuelewe. Usithubutu kufanya kinyume chake kama hakuelwi. Mwisho kabisa, ukiona mwenzio ana wasiwasi, jiepushe na hicho anachokihofia au mfanye aondoe mashaka.

Mwenzi wako anahisi kuna mtu unatoka naye kimapenzi. Fahamu kuwa hilo linamtesa moyoni, huwezi kujua kaambiwa na wangapi mpaka akaja kukuuliza. Zifanye fikra zake ziwe huru kwa kumuelewesha mpaka aelewe au jiepushe na huyo mtu.

Itaendelea wiki ijayo…

No comments: