Wanawake wengi walioolewa wako katika hali ya kukandamizwa kimawazo na waume zao, asilimia 27 kati yao wanatajwa kuwa na hamu kuondokana na ukandamizaji na kupata usawa lakini hawafanyi hivyo kwa kuogopa kupoteza wenza wao. Asilimia 51 wanatajwa kupigania haki huku wengine wakitajwa kutofahamu haki zao na maana ya usawa.
Licha ya idadi ya wanawake wataka haki kwenye ndoa kuongozeka katika siku za hivi karibuni, ushahidi unaonesha kuwa harakati za wanawake kupata usawa kwa waume zao zimekuwa zikikwama.
Pamoja na mambo mengi uelewa kuhusu jinsi ya kutafuta na kupata usawa ni jambo linalochangia wengi wao kuishi katika maisha ya kukandamizwa. Zifuatazo ni kanuni 22 za kumuwezesha mwanamke kupata haki au usawa kwa mumewe bila migogoro mikubwa.
KANUNI YA KWANZA
Jambo la kwanza kwa mwanamke kufahamu ni kwamba anapotafuta haki yake hatafuti ushindi bali suluhisho la tatizo. Hivyo anapoona mumewe hamfanyii haki, anamuonea na kwamba angependa kupewa haki kama mke ni lazima aweke dira hii ili ipunguze munkari wake pale atakapokutana na kikwazo cha kutosikilizwa.
KANUNI YA PILI
Tatizo kubwa la watu wengi wanapokuwa wanatafuta usawa hufikiri mambo yao na kuingia kwenye akili za wenza wao na kuchambua wanachowaza. “Amenifanyia hivi bila shaka atakuwa anatafuta sababu za kuniacha” Usifikirie tatizo kwa muono wako na kudhani aliyelifanya hivyo alilenga unachowaza, mara nyingi huwa sivyo. Waza kufuatana na msingi wa tatizo na si mawazo unayojitungia kichwani mwako.
KANUNI YA TATU
Wanachokosea wanawake wengi kwenye safari yao ya kutafuta usawa kwa waume zao ni kukusanya makosa, kuyatunza bila kuyatafutia ufumbuzi. Likitokea kosa jipya huamsha na yale ya zamani na kuyalalamikia kwa wakati mmoja. Kufanya hivyo huongeza mzozo na kamwe hakutoi nafasi ya kupewa haki kwa vile wanaume hawako tayari kutoa haki kwa makosa 30 kwa wakati mmoja. Inashauriwa likitokea tatizo litatuliwe kwa wakati huo na lisahaulike.
KANUNI YA NNE
Mazungumzo ya kudai usawa lazima yaambatane na lugha laini, zenye kushirikishana na kuwekana wazi. Mfano. “Mume wangu una tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani na hutaki nikuulize, hivi siku ukipata matatizo nitajuaje? Naomba uwe unaniambia kama utachelewa, au wewe unaonaje?” Kauli hii ni rahisi kumfanya mwanaume afikirie kutoa haki kuliko ikiambatana na ukali.
KANUNI YA TANO
Unapodai haki usiongee kupita kiasi mpaka povu likutoke, ukishaweka wazi lengo lako hitimisha kwa kumshukuru mwenza wako kwa kukusikiliza. Wanaume wengi hawapendi kusikiliza wenza wao kwa muda mrefu kwani hujiona kama wanachoshwa, wanatawaliwa au kukosewa adabu. “Nimekusikia mbona unaongea sana...au una jingine?” Wengi huhoji hivi pale mwanamke anapochukua muda mwingi kuzungumzia tatizo.
KANUNI YA SITA
Linapokuja suala la tuhuma za kusaliti penzi au kosa lolote haifai kuhukumu bila kumsikiliza mtuhumiwa. Linapotokea tatizo mpe nafasi mumeo ajitetee, sikiliza utetezi wake na uhoji kupitia maelezo yake. Hata mahakama hutoa nafasi kwa watuhumiwa kujitetea kabla ya kuwahukumu.
KANUNI YA SABA
Kabla hujang’ang’ania kutafuta usawa lazima wewe mwenyewe uwe muumini wa usawa, isiwe unamlazimisha mwenzako akupe haki wakati wewe humpi haki kama mume. Uhai wa usawa ni wa pande mbili.
Itaendelea wiki ijayo...
Je, ungependa kujifunza zaidi kuhusu elimu hii ya mapenzi? Andaa shilingi 3,000 zitakazokuwezesha kupata kitabu cha TITANIC kilichoheheni elimu ya mapenzi, meseji na chombezo mbili nzuri za kusisimua VUVUZELA KITANDANI na MSHAURI WA MAPENZI. Kitakuwa mtaani hivi karibuni usikikose!
No comments:
Post a Comment