Friday, June 28, 2013

Msingi imara ndiyo tiba ya matatizo yenu.


NAAM tumekutana tena kwenye kona hii ya mahaba. Kama kawaida ndani ya uhusiano kuna maudhi yaliyofikia hatua ya kukosa uelewano ndani.
Nitakuwa si muungwana kwa kutotanguliza salamu, mimi ni mzima wa afya njema, sijui wewe mwenzangu?
Nimepata maswali mengi juu ya matatizo ndani ya ndoa au uhusiano.

Ni matatizo gani hayo?
Kukosekana amani ndani ya nyumba zetu, heshima na upendo kutoweka huku ikiwa haijulikani nani baba, nani mama wote mmekuwa kambale kina mmoja ana sharubu.

Katika swali la msingi la ndugu yangu linatokana na tabia za mkewe kujiamulia mambo bila woga kama anajimiliki mwenyewe.
Yupo na mkewe muda mrefu sasa na wana watoto wawili ambao ni wadogo, ila kama isingekuwa hivyo angekuwa ameishamuacha muda mrefu. Kikubwa alikuwa akiomba msaada wa ushauri ili aepukane na dhahama za mkewe.

Nina imani wote swali mmelisoma, naamini ukipewa nafasi ya kushauri ungeanzia kwenye tatizo. Lakini kwangu mimi huwa sijibu tatizo bali chanzo cha tatizo ili mwingine yasimkute kama yaliyomkuta mwenzetu.
Hebu sasa tuangalie tatizo hilo linatokana na nini?
Kama nilivyoanza na kichwa cha habari kuwa msingi imara ndiyo tiba sahihi ya matatizo yenu.

Ni msingi gani?
Nina imani ni swali lililo akilini mwako.
Siku zote nyumba iliyo bora, ni ile yenye msingi imara ambao ndiyo unaobeba nyumba nzima atakayodumu daima dawamu.
Hata katika kitu chochote kama mapenzi au biashara msingi imara ndiyo unaoendesha kitu imara. Leo nazungumzia uhusiano wetu ndani ya nyumba kati ya mke na mume.

Hili ni tatizo linalotafuna uhusiano wetu:
Kuna tatizo moja ambalo huenda watu huwa hatulioni mwanzo tunapoanzisha uhusiano wetu, tatizo hili ni udhaifu wa mtu kushindwa kuwa kiongozi wa nyumba kutokana na baadhi ya vitu akiamini akivikemea huenda akaharibu uhusiano wao.

Mara nyingi mwanzo wa mapenzi wanaume wengi huwa dhaifu kwa wake zao kutokana na uchanga wa ndoa zao, huku wakitaka kuonyesha mapenzi kwa wenza wao. Hata linapotokea jambo la kuudhi au kwenda kinyume hawawakanyi, bali hulikemea kwa kubembeleza huku ikionesha wazi mtendaji anaweza kuamua mwenyewe iwe kuendelea kutenda au kuacha.

Unapoyafumbia macho makosa madogo madogo na kuamini ipo siku utayakataza, ni sawa na kuuacha ufa uliouona kwenye nyumba yako, jinsi unavyouacha ndivyo unavyokua.

Ukija kushtuka na kuanza kulikemea kwa nguvu, hapo lazima mwenzako ataona unamuonea kwa vile kitu kile alikuwa akikifanya kwa muda mrefu pengine miaka sita iliyopita, ulikuwa ukitazama tu na yeye kujiona yupo sawa japo akili yake inamsuta kwenda kinyume.

Hapa ndipo tunapata jibu la ndugu yetu kuwa ugonjwa aliuacha kipindi kirefu mpaka umekomaa. La muhimu ni kujenga msingi imara toka mwanzo wa uhusiano kwa kukemea yote kwa nguvu zote bila kuangalia umbile wala sura.

Kama mkeo ana tabia hizo bado hujachelewa, mweke chini na kukemea mabo yote anayotenda kinyume. Kama hataki kusikia, ni wazi si mwenzako katika safari ya maisha, uamuzi unao mwenyewe kuangalia kama kuwa naye ni faida au hasara kwako. Kama ni faida endelea naye kama ni hasara jibu unalo mwenyewe.

Mwanamke aliyetoka katika familia inayojua ndoa ni nini, ni msikivu kwa kila atakachoelezwa na mwenzake kwa faida ya ndoa yake. Ni mwenye tabia za kike za upole na usikivu, kumuheshimu mumewe na kuacha asichokipenda.

Hakuna sifa ya kushindana kila kitu na mumeo kwa kupaza sauti, mwanamke mwenye silika la kike huwa hapazi sauti juu, ni mwenye aibu.

No comments: