Saturday, September 25, 2010

Unatamani kumuacha? Chukua muongozo huu

Ni wiki nyingine tunakutana katika kona yetu. Mada ni ile ile ambayo tulianza nayo wiki iliyopita.
Nilieleza kwamba inawezekana ikaonekana ni jambo geni, Luqman kutoa somo la kuachanisha wapenzi lakini tukisimama kwenye ukweli tutajua kuwa haya mambo yapo.

Tamu imekuwa ikigeuka shubiri. Matarajio ya wengi yamekuwa yakishindwa kutimia. Uliyedhani anaweza kuwa mwenzi bora wa maisha yako hadi kufa, keshokutwa unaweza kubaini kwamba umedandia mti ambao siyo.

Uvumilivu ni pointi ya kwanza lakini inawezekana umevumilia muda mrefu na hajabadilika. Tutatakiwa kuamini katika kufundisha, pengine umemfundisha bila kuona mabadiliko. Siku zote mapenzi ni kupendana, kuheshimiana, kila mmoja atunze hisia za mwenzake kinyume chake ni kichocheo cha kuachana.

Hata hivyo, ibaki kichwani kuwa inauma mno kuachana na mtu uliyempenda, hivyo unapoamua inakubidi uwe na dhamira kutoka moyoni kwamba umechoshwa naye, halafu fuata dondoo zinazofuata;

WEKA SABABU ZAKO MEZANI!
Unapotaka kumbwaga rafiki yako au mpenzi wako ambaye hujampa ahadi yoyote ya kuishi naye katika ndoa, anza mchakato kwa kuweka bayana sababu zinazokufanya utake kuachana naye. Hakikisha kuwa sababu unazoziweka ni zile ambazo mpenzi wako huyo hatapata namna ya kuzipinga.

Zitengeneze sababu hizo kwa kuzingatia mtazamo wako mwenyewe, na si kwa mtazamo wa mpenzi au rafiki yako huyo, ili hatimaye kusiwe na sababu ya mwenzako huyo kudhani atajirekebisha ili aweze kuendelea kuwa na wewe.

Namna hii utakuwa unayaangalia zaidi maslahi yako mwenyewe na iwapo utalazimika kumweleza mwenzako ni kwa nini unataka kumaliza uhusiano wako na yeye, sababu zako hazitaonekana kama shambulio kwake yeye mwenyewe wala tabia yake.

USITHUBUTU KUWASILIANA NAYE!
Utakapaokuwa umeweka wazi sababu zako na kuziamini, weka mkakati kuwa hutaanzisha tena mawasiliano na mwenzako. Jiwekee msimamo kuwa hutampigia simu, wala kumtumia ujumbe wa simu, wala baruapepe na kadhalika, ila utajibu tu yeye atakapoanzisha.

Unapomwalika mtu au kumpigia simu au kumtumia ujumbe ni kama unamtia moyo na kumfanya aamini kuwa unampenda na kumjali. Kama mhusika ni mtu mwenye fahamu atashtuka kuwa jitihada zote anafanya yeye na wewe uko kimya. Akitafakari atagundua kuwa hauko naye tena.

KATAA ANAPOKUITWA
Iwapo kweli umedhamiria kumaliza uhusiano wako na mwenzako, jaribu kukataa mialiko anayokupa, mathalani kwa ajili ya chakula cha pamoja cha mchana. Pia kama atasema atakufanyia jambo fulani, kataa kiaina.

Fanya vivyo hivyo kwa matukio yote ya kijamii. Kataaa mialiko kwa njia ambayo hatakushtukia haraka kuwa humhitaji tena, bali aje kushtuka baadaye atakapojumlisha matukio.

Katika hatua za awali, hii itamaanisha kuwa utakosa kwenye matukio fulani ambayo wewe mwenyewe ungependelea kuyahudhuria, lakini huna la kufanya, maana umeazimia kumaliza uhusiano wako na mpenzi au rafiki yako.

Unapotaka kupeleka ujumbe kwa mpenzi wako kuwa hayuko tena moyoni mwako, lazima tu ujitoleee kupata hasara katika baadhi ya mambo. Kumbuka kuwa huhitaji tena uhusiano wako na mwenzako.

MUWEKEE MAPOZI
Kuna wakati ambapo rafiki au mpenzi wako atafanya au kusema jambo na wewe utatakiwa kuonesha mwitikio. Kama umeshadhamiria kuachana naye, onesha mwitikio wa shingo upande.

Kama mhusika atabaini jinsi ulivyoitikia shingo upande, utakuwa umepeleka ujumbe maridhawa, kwamba huna tena furaha na uhusiano wenu na kwamba unahisi ni wakati muafaka wa kumaliza mambo.

Kuna mazingira ambayo hutaepuka kumwitikia mpenzi au rafiki unayetaka kumpiga chini. Kwa sababu hiyo, ndiyo maana unapaswa kumwitikia lakini katika hali ambayo inaonesha kana kwamba huna habari naye sana.

Unapomwitikia mpenzi wako kwa shingo upande, unamwonesha kuwa si tena kipaumbele kwako, jambo ambalo litamfanya yeye mwenyewe kuona kuwa ni wakati muafaka wa kupunguza moto wake kwako.

KAA NAYE MBALI
Kama umekuwa na mazoea ya kuwa karibu na mpenzi wako kama ilivyo kawaida, anza kujenga mazingira ya kujitenga naye mnapokuwa mbele za watu, ili aweze kuhisi mabadiliko katika mwenendo wako.

Haina maana kuwa usizungumze naye kaa naye karibu na uzungumze naye kama kawaida, lakini majibu yako yawe ya mkato. Pia usikae karibu naye sana, maana namna hiyo utalazimika kuzungumza naye na kukaribisha lugha yake ya matendo.

Lakini kama itawezekana, jishughulishe zaidi kuzungumza na watu wengine ili kwa kiasi Fulani huyo mwenzako aweze kuona kuwa hukumpa kipaumbele cha kwanza.

Itaendelea wiki ijayo

No comments: