Sunday, December 30, 2012

Unavutia lakini hupati mpenzi wa kweli, tatizo ni nini?

NIANZE kwa kuwakumbusha kwamba bado kidogo sana kile kilio chenu kifikie tamati, ni juu ya ujio wa kitabu changu kipya kilichokusanya mada nyingi pamoja na Love Messages zenye tiba ya penzi linaloanza kupoteza mwelekeo.

Kinahusu msichana mmoja mrembo (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 29, lakini aliyeteswa na mapenzi sana. Watu mbalimbali walitoa ushauri na maoni yao, wengine wakaomba wawe wachumba. Mh! Haya bwana, ninachokifanya ni kuchapa baadhi ya sms kisha mwenyewe ataamua la kufanya. Hebu tuone sms za wasomaji kumi tu...

Msomaji wa kwanza: Bibie hii ndiyo hali ya dunia, kumbuka kuna msemo unasema, hakuna kizuri kinachokosa kasoro. Steven Mhehe, Zanzibar.

Msomaji wa pili: Huyo binti kuna mahala anakosea, uzuri alionao kama wanavyosema hautoshi, inawezekana si mnyenyekevu katika uhusiano, anakosa lugha ya mapenzi n.k. Ajaribu kuangalia maeneo hayo. Bunge Nyamonge, Ukonga Dar.

Msomaji wa tatu: Anko Jose, mimi naitwa Deo wa Dar, naomba namba ya huyo dada wa Tanga, nataka kuzungumza naye.
Msomaji wa nne: Niilichojifunza hapo ni kwamba watu wapeane mapenzi baada ya ndoa na siyo kabla. Omary Juma, Igogo, Mwanza.

Msomaji wa tano: Nimejifunza kwamba, si mwanaume utakayemuona anaweza kuwa na mapenzi ya kweli, pia tusipende kujirahisha kwa wanaume, kwa sababu mwanaume akishakufunua na kujua ulivyo, imepita. Nawashauri wasichana wenzangu tuwe na msimamo. (Hajataja jina lake).

Msomaji wa sita: Huyo dada wa Tanga anaonekana kuwa na matatizo kama yangu, mimi ni mwanaume msomi wa Chuo Kikuu, nina miaka 39. Nimeachana na mke wangu wa ndoa kwa matatizo. Niunganishe na huyo dada tunaweza kufarijiana! Mpe namba yangu, nitamweleza nilipo.
Msomaji wa saba: Pole sana dada zetu mlio wazuri kupindukia, kwani wanaume wengi huwa waoga kuwa katika uhusiano na watu wazuri, wakihofu kuachwa. Ninachoweza kusema ni kwamba sisi wanaume ndiyo wabaya wa kuwachezea watoto wa watu na mwisho wanaonekana kama malaya tu!

Msomaji wa nane: Naitwa Ngosha kikazi nipo Arusha, lakini wikiendi hii nipo hapa Dar. Mimi ni Mkristo, miaka 27, nimezaliwa Bugando. Naomba namba ya huyo dada, kama yupo tayari kufunga ndoa.

Msomaji wa tisa: Wanawake wengi hutumia uzuri wao kwa kufikiri kuwa kila mwanaume anayemtaka kimapenzi humpenda kwa ajili ya uzuri alionao, matokeo yake humtumia kimapenzi na kumuacha. Anachotakiwa kufanya huyo dada ni kwamba, hakuna mwanamke mwenye matatizo katika suala zima la mapenzi, kwani hayo mambo ni ya kujifunza hata kama hujui. Afahamu kwamba wanaume wote aliowahi kukutana nao, hawakumpenda bali walimtamani, awe makini sana wakati wa kuanzisha uhusiano mpya na mwanaume mwingine na asitumie uzuri wake kuwa kigezo cha kupendwa na kila mwanaume.

Zuhura M., Dar es Salaam.
Msomaji wa kumi: Tunajifunza kwamba, uzuri si kigezo cha tabia, maana unaweza kuwa mzuri lakini ukawa mbovu wa tabia. Timilai Shemalamba, Tanga.

KUTOKA KWA SHALUWA
Ushauri wa wote niliochapa meseji zao, nimeuacha kama ulivyo na msomaji wangu huyo ana uamuzi wa kuamua nini cha kufanya.

Aidha, kuna ambao mmeomba namba zake, kwakuwa sina mamlaka ya kutoa namba za mtu, nimechapa namba za waombaji ili kama dada huyo akiridhia mwenyewe atakutafuta. Haya twende moja kwa moja kwenye funzo linaloonekana hapo.

Tunaona moja kwa moja makosa ya kuruhusu mwanaume aujue mwili wa mpenzi wake mapema. Suala la uaminifu huanzia mbali rafiki zangu, ukionekana huna msimamo, rahisi kudanganyika, tafsiri yake inakuwa kwamba unaweza kuwa hivyo kwa wanaume wengi zaidi.

Nani anapenda kuwa na mwanamke wa kuchangia? Nani anapenda kuwa na mwanamke anayedanganyika kirahisi? Utadanganyika na wangapi? Wanaume wanapenda kuona unakuwa mgumu kuruhusu mwili wako kuchezewa! Ndiyo wengi wanajisifu wakiwa kwenye ndoa zao.

Ndiyo maana utasikia mwanaume akijisifu kwa mkewe: “Mke wangu ulikuwa mgumu sana, lakini nilitumia kila njia kukupata...” au “Ah! Ulinisumbua sana mke wangu, lakini nashukuru nimekupata.” Kwanini yote haya? Kwa sababu anahisi yupo na mwanamke thabiti, mwenye msimamo na asiyeyumbishwa.

Sina shaka umepata kitu kipya kichwani mwako. Naomba niwaache, hadi wiki ijayo tena nitakapokuja na mada nyingine.

No comments: