Friday, October 22, 2010

Usibabaike na kukuita kwake sweetie, honey, swali ni je, anakupenda?

Kwa nguvu zake Mwenyezi Mungu mimi ni mzima wa afya njema na ninaendelea vyema na majukumu yangu ya kila siku likiwemo hili la kukumbushana na kuelimishana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Kabla sijaenda mbali, katika mada hii ambayo naamini itawagusa wengi, ni vizuri kama tutajiuliza kwa pamoja maana ya mapenzi! Mapenzi humaanisha nini hasa? Je, ni usanii au ni tofauti na hivyo?

Katika hili, kila mmoja anaweza kuwa na maana yake lakini binafsi naweza kuyatafsiri mapenzi kama hisia ambazo zipo moyoni mwa mtu kwenda kwa mwingine. Hisia hizi ili ziweze kuwa mapenzi ni lazima ziwe na ukweli na za dhati huku moyo ukiwa na nafasi kubwa katika hilo.

Hii ndiyo maana ya haraka haraka ya mapenzi. Kwamba unapoingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu uliyetokea kumpenda, hupaswi kuwa na mtu mwingine kwakuwa, kufanya hivyo ni kuunyima haki moyo wako.

Pamoja na ukweli huo juu ya mapenzi, lakini hivi sasa maana halisi ya mapenzi imepotoshwa kabisa, imebadilishwa huku kila mmoja akiyachukulia kama anavyoona yeye na kujiona yuko sahihi. Mapenzi ya siku hizi yamejaa usanii mtupu, hayana ukweli, kila siku ni maumivu juu ya maumivu. Kwanini watu wanaharibu maana halisi ya mapenzi?

Tunajua matatizo mengi yanaweza kutukumba iwapo tutakuwa siyo waaminifu kwa wale tuliowaeleza kwamba tunawapenda. Tunajua kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja ni kujitafutia matatizo ambayo mwisho wa siku tunaweza kujikuta tunajuta na kutoa machozi lakini bado tunaendelea kufanya hivyo.

Tunaelewa wazi inavyouma kusikia mpenzi wako ana mtu mwingine lakini sisi mbona tunawafanyia wenzetu hivyo? Hatuoni kwamba kwa kufanya hivyo tunakwenda kinyume kabisa na maana halisi ya mapenzi?

Unaweza kujifanya mjanja sana kwa kuunganisha wapenzi zaidi ya kumi huko gizani ukiamini huonekani na hakuna matatizo yoyote ambayo unaweza kuyapata, kumbe unajidanganya maana kuna siku utakuja kuumbuka kwa kuonekana kwako si muaminifu!

Ila sasa kitu ambacho kimekuwa kikinisikitisha ni pale mtu anapoona dalili za wazi wazi kwa mpenzi wake kwamba si muaminifu lakini bado anaendelea kumng’ang’ania eti kwa maelezo kwamba anampenda sana na hayuko tayari kumkosa katika maisha yake. Jamani inakuwaje mtu ameshabaini yuko ndani ya penzi la kitapeli lakini bado haambiwi wala hasikii?

Najua wapo walio katika penzi la kitapeli kwa kuhisi wanapendwa kutokana na kuitwa majina ya kimahaba lakini hawajui. Ila kuna hawa ambao kutokana na ulimbukeni wao wanajua kabisa wameingia ‘choo cha kike’ lakini hawataki kutoka.

Naomba niseme tu kwamba, wapo watu ambao utapeli ndiyo asili yao, yaani mapenzi yao wanayaendesha kiujanja ujanja. Ni walaghai ambao inafika wakati hujifanyisha kuwa wana mapenzi ya kweli lakini ukichunguza sana unakuta hamna kitu.

Ukiwa na bahati mbaya ya kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu wa aina hii ni vigumu sana kudumu naye na hata kama mtadumu, hamuwezi kufurahia maisha yenu.

Unamkuta mwanamke ni mwepesi sana kukuita majina mazuri ya kimapenzi kama vile sweetie, honey na mengineyo ya aina hii lakini ungebahatika kuingia kwenye moyo wake ungekutana na hali tofauti, yaani hakupendi kama unavyodhani. Hawa wapo wengi lakini ni vigumu sana kuwabaini.

Yaani wao kuwasaliti wapenzi wao ndiyo maisha yao ya kila siku lakini ngoja nikuulize wewe unayemsaliti mpenzi wako. Hivi unavyomfanyia mwenzako hivyo unadhani yeye hana moyo? Hivi hujui kuwa mwenzako anakupenda kwa mapenzi yake yote na amekuchagua wewe uwe wa kumpa furaha? Siku akijiua kwa sababu yako utakuwa katika hali gani? Hebu acha utapeli wako!

Kuwa muwazi, dhihirisha kile kilichomo moyoni mwako. Acha kujifanyisha, kama unampenda kiukweli mfanye mwenza wako aamini hivyo lakini kama humpendi basi mwache huru atafute mwingine mwenye msimamo na uendelee na maisha yako.

No comments: