KAMA ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba na kupeana mawili matatu kuhusiana na mambo ya uhusiano ambayo yamekuwa yakiwatatiza watu kila kukicha. Kwa uwezo wa mola nina imani wote mu wazima wa afya njema, yangu hali sijambo.
Leo nilitaka tuzungumzie kuhusu mtu kuanzisha penzi jipya wakati bado penzi la zamani halijamtoka akilini. Hii inatokana na swali la ndugu yangu mmoja kusema kuwa alikuwa na mpenzi wake ambaye alikuwa ameachana na mpenzi wake.
Walipendana sana na kuahidiana kufunga ndoa, lakini hivi majuzi mpenzi wake alikuja na kumueleza wamerudiana na mpenzi wake wa zamani ambaye walitengana na kuamua kuanzisha penzi jipya.
Kwa hiyo mipango yao ilivurugika na kuamua kulivunja penzi lao, lakini ajabu yule mpenzi wake bado amesema kuwa bado anampenda na wataendelea kuwa wapenzi bila malengo ya kuoana kwa vile mpenzi wake wa zamani kajirudi kwa makosa yote yaliyosababisha kuachana.
Jamaa alitaka ushauri juu ya yule mwanamke na kuuliza ana mapenzi ya kweli na yeye? Jibu nafikiri lipo wazi kwa kuwa mpaka amevunja uhusiano na wewe hana mapenzi nawe tena. Lakini nataka kulipanua zaidi ili kila mtu alielewe matatizo ya kuanzisha uhusiano mpya wakati wa zamani hayajakutoka moyoni mwako.
Kuendelea kufanya mapenzi na mwanamke ambaye tayari ameshakueleza kuwa amerudiana na mpenzi wake wa zamani, na mpango wenu wa kuendelea kuwa pamoja umekufa.
Hapa nataka wote twende pamoja, kumekuwa na maamuzi ya pupa ambayo hulenga kukomoana pale mtu na mpenzi wake wanapokorofishana na mmoja kuamua kuanzisha mapenzi mapya bila kufikia kikomo cha penzi la zamani.
Siku zote watu mnapokorofishana lazima muangalie tatizo lenu lina ukubwa gani, ambalo haliwezi kupata suluhu na kuamua kuachana. Panapotokea tatizo si busara kutoa maamuzi ya kukurupuka, kwani wagombanao bado wana nafasi ya kupatana.
Hivyo si busara kuanzisha uhusiano mpya na baadaye kuvunja penzi jipya ghafla baada ya kumaliza tofauti zenu na mpenzi wako wa zamani.
Pia si vizuri unaporudisha penzi la zamani kuendelea na penzi jipya sawa na kumtafutia matatizo mpenzi wako mpya. Kutembea na mtu ambaye ameshakueleza kuwa amerudiana na mpenzi wake wa zamani lakini bado anakupenda, ni sawa na kutembea na mke wa mtu kwa vile unajua kabisa ana mtu.
Kutembea na mtu ukijua kabisa anamilikiwa na mtu ni kujihatarishia maisha, kama alikuahidi kuwa utakuwa naye siku zote za maisha yenu na baadaye kamrudia mpenzi wake waliyetengana. Lazima uwe na moyo wa kijasiri kukubaliana na uamuzi huo kwa vile, waliotengana wamerudiana.Source ya mada hii ni kutoka kwa >>Muandishi Joseph shaluwa
No comments:
Post a Comment