Sunday, November 14, 2010

Maumivu ya kuachana wakati bado mnapendana unayajua?

Ni jambo la kumshukuru Mungu kutukutanisha tena kupitia safu hii ambayo lengo lake kuu ni kuelimishana na kukumbushana juu ya mambo mbalimbali yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Wiki iliyopita nilizungumzia mada iliyokuwa inawagusa moja kwa moja wanawake na suala la kujirahisi kwa wanaume. Nilieleza namna ambavyo miili yao ina thamani kubwa kuliko wanavyofikiri.

Hivyo basi, wanaume ambao wanatakiwa kupata fursa ya kuichezea miili yao wawe wale ambao wamewapenda kwa dhati na mioyo yao imeridhia. Wasifanye hivyo kwa tamaa ya pesa ama kitu kingine.

Baada ya kugusia kidogo mada hiyo ya wiki iliyopita, leo nizungumzie jambo moja ambalo limekuwa likiniumiza sana na kujiuliza kwanini huwa linatokea. Wakati najaribu kupitiapitia mtandao, niliona waraka wa barua pepe ambayo dada mmoja alikuwa akimtumia mpenzi wake wa zamani. Naomba niuandike hapa chini kama ulivyo kabla ya kuendelea.

Kwako John, nilikupenda sana mpenzi wangu, nawe ulionesha mapenzi ya dhati kwangu lakini kwa kile kilichotokea ambacho siwezi kukiandika hapa, tuliachana wakati bado nakupenda. Wakati mwingine nahisi sikustahili kukuacha lakini hilo linakuja akilini mwangu nikiwa tayari nimefanya uamuzi.

Kurudi kwako tena nahisi hutanikubalia, nabaki nalia. Nakutakia maisha mema lakini jua nimekuacha wakati nakupenda.
Ni mimi Janeth.

Janeth anaumia kwa uamuzi aliochukua wa kuachana na mpenzi wake wakati bado walikuwa wanapendana. Yawezekana alifanya hivyo kutokana na hasira ama kasoro ambazo alizibaini kwa mpenzi wake. Labda nilizungumzie hili la kasoro za wapenzi wetu kama chanzo cha wengi kuachana wakati bado wanapendana.

Tuelewe kwamba, kila binadamu ana kasoro huku zikitofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Kama ni mfuatiliaji mzuri wa safu hii utakumbuka niliwahi kuandika makala inayosema kuwa, tuvumiliane hasa tunapobaini kuwa wapenzi tulio nao wana kasoro fulani.

Wakati nikiandika hivyo, leo nalazimika kulizungumzia hili la namna ya kukabiliana na kasoro za wapenzi wetu kutokana na ushauri alioomba mmoja wa wasomaji wangu.

“Naitwa Rehema, nina mpenzi wangu ambaye tunapendana sana lakini miongoni mwa vitu ambavyo vinatufanya tusilifurahie penzi letu ni kasoro za kiuanaume alizo nazo. Ananipa kila ninachokitaka lakini tunapokuwa faragha mambo hayaendi.

“Imefika wakati amekuwa akitoa machozi na kunieleza kuwa, tatizo lake la kimaumbile (jogoo kutoamka) analishangaa kwani humjia anapokutana na mimi tu. Mwenyewe anadai aliyemfanyia mchezo huo ni mpenzi wake wa zamani. Nampenda lakini kasoro hiyo aliyo nayo mpenzi wangu inaniweka njia panda.”

Wapo watu wengi walio katika uhusiano usiokuwa na furaha kutokana na kasoro ndogo ndogo ama kubwa walizonazo wapenzi wao. Katika hili kwanza lazima tujue kwamba, hakuna binadamu aliyekamilika!

Leo hii unaweza kumuacha mpenzi wako kutokana na kutokuridhisha katika tendo la ndoa tu lakini ukaingia kwenye uhusiano na mtu mwingine ambaye yeye ni ‘mzuri’ faragha ila ni mlevi na mkorofi.

Ndiyo maana siku zote tumekuwa tukitakiwa kuzifanyia tathmini kasoro walizonazo wapenzi wetu kabla ya kuchukua hatua ya kuwaacha au uamuzi mwingine usiofaa.

Tufahamu kwamba, mapenzi ndiyo yanayotangulia, moyo wako unapompenda fulani hauangalii kasoro alizo nazo kwasababu moyo wenyewe unajua kuwa, kasoro alizonazo mtu haziuzuii kupenda.

Ndiyo maana leo hii unamkuta mwanamke yuko katika uhusiano na mwanaume mkorofi kupita maelezo lakini mwanamke huyo anakueleza kuwa, hawezi kumuacha kwakuwa moyo wake umependa. Anachokifanya ni kumvumilia ili kutokwenda kinyume na matakwa ya moyo wake.

Kwa mfano, mpenzi wako hayajui mapenzi! Hiyo ni kasoro kubwa ambayo wapenzi wengi wamekuwa wakiilalamikia. Mara ooh! Mpenzi wangu hayajui mambo, ni goigoi awapo uwanjani. Mara ooh! Mpenzi wangu akienda mzunguko mmoja tu hoi.

Sawa! Hayo ni mambo yanayokukwaza lakini ndiyo uchukue hatua ya kumuacha kweli? Sidhani kama utakuwa ni uamuzi sahihi na wale wanaowaacha wapenzi wao eti kwasababu wana kasoro fulani wanadhihirisha kutokuwa na mapenzi ya dhati.
Kasoro za wapenzi wetu haziwezi kuwa sababu sahihi za kuwaacha, kama moyo wako umempenda huyo uliye naye na yeye akaonesha kukupenda, kasoro alizo nazo zichukulie kama changamoto kwako.

Tambua kwamba unaweza kubahatika kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hana kasoro kubwa za kukukwaza lakini akawa hana mapenzi ya kweli, matokeo yake akawa mtu wa kukuliza kila siku.

Cha msingi, unapokuwa katika uhusiano na mtu kwa muda fulani ni lazima utabaini kasoro alizo nazo lakini na yeye pia atakuwa amekusoma na kukujua vizuri. Kama kweli mnapendana, mnachotakiwa kufanya ni kuangalia njia sahihi za kukabiliana na kasoro zenu. Zifanyieni kazi, rekebishaneni, yatafutieni ufumbuzi matatizo yenu ili mwisho kasoro hizo zisije zikawafanya mkaachana wakati bado mnapendana kwani inauma sana.

Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena hapa wiki ijayo.

No comments: