Friday, January 14, 2011

Kama una moyo mdogo, usitake kujua historia ya mpenzi wako...

NAAM kama ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ya mahaba, ili kujuzana machache kuhusiana na maisha yetu ya kila siku ambayo yametawaliwa na mapenzi kwa asilimia kubwa.


Leo nataka tuzungumzie kitu kimoja kuhusiana na jinsi mtu anavyopokea historia ya nyuma ya mwenzake, pale mnapokuwa mmeanzisha uhusiano mpya kila mmoja wenu alikuwa tayari amekwishauanza kwingine.
Ni vizuri kila mmoja kuwa muwazi kwa mwenzake pale anapotaka kujua historia ya nyuma ambayo itamuondoa hofu kwa kujua nini mwenzake alifanya nyuma. Hii husaidia kukufanya usishangae ukijua kitu cha mwenzako ambacho tayari aliishakueleza kama kitajitokeza mbele.
Lakini hapa kuna kitu kimoja ambacho ni muhimu sana watu kujua, kitu hiki humfanya mtu kupoteza imani ya mwenzake pengine kujuta kwa nini alikubali kuwa mwenza wake. Japo katika maisha yetu ya kila siku, kila mtu anatakiwa kuitunza rekodi yake kabla ya kuanzisha uhusiano.
Na hii imekuwa ikiwaelemea sana wanawake pale wanapokuwa wamekutana na wanaume zaidi ya mmoja, akili ya mwanaume atajua wewe ni malaya, Lakini ni tofauti na mwanaume hata akitoa historia yake kuwa alikuwa na wanawake watano bado kwa mwanamke haimsumbui moyoni bali humlinda kwa muda ule aliokuwa nao.
Ila atakuwa na wivu sana kwa kuamini wewe ni mzuri kila mwanamke anakutaka. Nia yangu ni kuelezea uwezo wa mtu kupokea historia ya mwenzake, kama una moyo mdogo si vizuri kutaka kujua historia ya mpenzi wako hasa wanaume ambao huenda ukaelezwa mtu fulani ambaye unamfahamu hata ukimuona moyo unakupasuka japo mpenzio amekuhakikishia hayupo naye tena.
Historia ina faida gani?
Faida ya historia kwa wapendanao ni kuondoa uchafu ambao pengine kama ungeusikia siku za mbele ungekuumiza moyo wako. Na pengine hata kujilaumu kwa nini hukuujua mapema. Faida nyingine ni kumjua mwenzako kiundani pengine ndugu yako wa toka nitoke ambaye mlipotezana mkiwa wadogo.
Unapotaka historia ya mwenzako hakikisha moyo wako jasiri na kuwa tayari kusamehe hata yale yatakaoumiza moyo wako. Na baada ya kupokea historia ni nafasi yako ya kujenga hatua nyingine kwani siku zote mwisho wa penzi la zamani ni mwanzo wa penzi jipya.
Pia pengine mwenzako kabla ya uhusiano wenu ana mtoto lakini amefanya siri kwa wewe kuamini hana motto mwisho wa siku unajua. Lazima moyo utakuuma na kuamini mwenzako si mkweli.
Katika maisha ya leo kina mtu ana makosa yake ambayo yanarekebishika, kama historia ya mwenzako ni mbaya au amekukosesha amani. Tumia makosa yake kujenga penzi imara kwani siku zote mwenye akili timamu hujifunza kutokana na makosa yake.

Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

No comments: