Thursday, April 5, 2012

Si wanawake tu, hata wanaume nao huchezewa na kuachwa!


Wanateseka kama wanavyoteseka. Wanapata tabu na matatizo ya moyo sawa na wanawake. Hata hivyo, wengi hawapati nafasi ya kuwaelezea. Leo ni zamu yao.
Kwa utamu wa mada na jinsi nilivyo na haraka, nimesahau hata kuwasalimia...mambo marafiki? Mko poa? Bila shaka mtakuwa wazima wa afya njema na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku. Karibuni tujifunze katika mada yetu ya leo.

Imekuwa ni kawaida sana kusikia wanawake wakilalamika baada ya kuachwa au kuachana na wapenzi wao, kwamba wamepotezewa muda, wamechezewa n.k. Hizi zimekuwa kauli za kawaida kabisa katika jamii, lakini ukitazama kwa upana dhana hii ina matatizo kidogo.

Hebu tujiulize pamoja, kuchezewa ni nini haswa? Kwanini wanawake wamekuwa na tabia ya kulalamika kwamba wamechezewa? Ni kweli kwamba wanaume nao hawawezi kuchezewa na kuachwa? Bila shaka yoyote, majibu ya maswali haya utayapata katika mada hii ambayo itakuongezea jambo fulani kichwani mwako.

DHANA YA KUCHEZEWA
Inawezekana kila mmoja akachambua kwa mtindo wake, lakini mwisho maana inabaki katika mlengo mmoja tu, kupotezewa muda, kutumika kimapenzi! Hiyo ndiyo maana ya moja kwa moja.

Kama ndivyo, mwanaume ana kitu gani cha tofauti katika mwili na moyo wake, ili aondolewe kwenye kipengele cha kuchezewa na kuachwa? Wapo wanaume kadhaa ninaowafahamu ambao maisha yao yamebadilika baada ya kuachana na wapenzi wao waliowapenda.

Hawana furaha tena, hawana uwezo wa kufanya kazi sawasawa, wameathirika kisaikolojia na kila kitu katika maisha yao kimeharibika! Tuwaiteje nao hawa? Si kwamba wamechezewa na kuachwa?
“Maisha yangu yamebadilika kaka Shaluwa, sina mbele wala nyuma, yule mwanamke nilikuwa nampenda sana, lakini ndiyo hivyo nimelazimika kuachana naye kwa sababu nimegundua ni msaliti.

“Siku zote nilikuwa namtegemea yeye, nilimwamini kwa kila hali, nikampa moyo wangu wote, lakini hakuridhika, akanisaliti. Nimedumu naye kwenye mapenzi kwa miaka minne, sikuwahi  kumsaliti hata mara moja.

“Nimefanya naye mambo mengi sana, tulikuwa na mipango mikubwa sana katika maisha yetu, lakini kila kitu kimezimika. Kila mtu yupo kivyake, moyo wangu una simanzi sana.
“Siwezi kufanya kazi vizuri na hivi ninavyokuambia, nina barua mbili za onyo kutoka kwa bosi wangu, akinitaka nibadilike. Nashindwa kumweleza ukweli wa mabadiliko yangu kikazi, maana atanifukuza.

“Sina la kufanya, muda wote namuwaza Betty mwanamke ambaye niliamini angekuwa wangu wa milele, kumbe nilikuwa najidanganya,” alisema Moses, ambaye alifika ofisi kwangu wiki iliyopita kwa ajili ya ushauri.ANORD  ni mfanyakazi katika kampuni moja jijini Arusha. Alikuja kuniomba ushauri baada ya kuachana na mpenzi wake miezi miwili iliyopita. Baada ya tukio hilo, ambalo kimsingi ni yeye aliyeliamua, hivi sasa anaishi maisha ya wasiwasi, akitumia muda mwingi kufikiria jinsi alivyokuwa akiishi na mpenzi wake huyo.

Kwa hakika alikuwa katika hali mbaya sana, nikapata wasaa wa kuzungumza naye kwa muda mrefu sana. Aliondoka akiwa na mahali pa kuanzia, nikiwa na maana kwamba, tatizo lake linahitaji muda, hupona taratibu kulingana na masharti niliyompatia wakati nikimshauri.

Hapo ndipo mada hii ilipozaliwa. Umejifunza nini kupitia Moses? Kwamba hata wanaume nao huteswa, huteseka na hushindwa kufanya mambo mengine, pindi wanapochukua uamuzi mgumu wa kuachana na wale ambao wanawapenda kwa dhati.

HISIA
Rafiki zangu, naomba niwatoe mchanga machoni kuwa, hisia za mapenzi ni zile zile. Haina maana kwamba, mwanamke ana uwezo wa kupenda sana kuliko mwanaume, la hasha! Kikubwa ni hisia kuwa za kweli.
Kwamba mwanamke kama atakuwa hajampenda mwanaume kwa dhati, kadhalika na mwanaume naye akiwa hajampenda mwanamke kwa dhati, itabaki kuwa hivyo, lakini kama wote watakuwa na mapenzi ya kweli, hali hiyo itaendelea kuwa hivyo kwa wote.

KUWEKEZA MAPENZI
Kama ulikuwa hujui, anza sasa kuingiza jambo hili kichwani mwako, kama wafanyabiashara wanavyowekeza katika sehemu mbalimbali, ndivyo ilivyo pia katika mapenzi. Mwanaume kama alivyo mwanamke, akipenda kwa dhati huhifadhi moyo wake kwa mwanamke huyo.

Mapenzi ni kuwekeza na ukishafanya hivyo, inakuwa vigumu sana kuuondoa moyo wako. Hapo sasa ndipo yanapokuja maumivu na dhana ya kuchezewa na kuachwa! Rafiki zangu, natamani sana kuendelea, lakini nafasi yangu ni ndogo. Wiki ijayo nitamalizia sehemu iliyosalia. Nawapenda sana!

No comments: