NAAM tumekutana tena katika mwezi mtukufu wa Ramadhani ambapo waumini wa dini ya Kiislamu wapo katika funga, nawatakia mfungo mwema ili wapate malipo mazuri kwa Subhhana Wataala.
Nitakuwa si muungwana kwa kutotanguliza salaam, ni matumaini yangu mu wazima wa afya njema.Tuendelee na mada yetu, kama kawaida tumekutana tena kujuzana mawili matatu kuhusiana na matatizo katika maisha yetu ya uhusiano.
Nimepokea maswali mengi kutoka kwa vijana na wengineo wanaoanza uhusiano wa kimapenzi, ambao wanaona wapenzi wao hawawapendi kutokana na tabia ya kuwazungusha kukutana kimwili.
Moja ya swali linasema hivi:
Kaka, nina mpenzi wangu ambaye tunapendana sana na lengo letu ni kuwa mke na mume, siku moja niitwe baba na mwenzangu mama.
Lakini kuna tatizo moja, nashindwa kumuelewa mwenzangu kwani kila ninapomuomba tufanye mapenzi ananizungusha, mara hivi mara vile, nikimng’ang’ania utasikia eti nisubiri hadi tuoane. Hivi kweli ana mapenzi na mimi? Naomba msaada wako.
Nina imani kila mmoja swali amelisoma, kinachosubiriwa ni jibu langu, nami sina hiyana nitalijibu kama ifuatavyo:
Katika mapenzi ya sasa, ngono imetawala sana, yaani wapenzi wameweka mbele ngono halafu ndiyo mambo mengine yanafuata, pia imeonekana usipopata kuujua mwili wa mwenzio hakuna mapenzi, ni sawa?
Maana ya mapenzi:
Mapenzi ni upendo wa dhati utokao moyoni mwa mtu wala si kuvuliwa nguo na mtu kila unaposhikwa na hashki.
Ngono si upendo wa dhati, bali upendo wa kweli upo moyoni kwa mtu na siku zote apendaye ni mvumilivu wala hatangulizi ngono mbele. Kwa vile anajua yule ni mpenzi wake hana sababu ya kumnyima, mwili wake ni mali yake kwa kuwa hata katika vitabu vitakatifu imeelezwa.
Mwanamke hana mamlaka juu ya mwili wake bali mumewe, vivyo hivyo mwanaume hana mamlaka juu ya mwili wake bali mkewe, pia imetusisitiza pale iliposema tupeane, tusinyimane (Kwa wanaotaka kusoma watazame Wakorintho2 7:1-10).
Nina imani mmeona umuhimu wa kupeana tendo la ndoa ambalo hata Mungu amesisitiza kupitia vitabu vyake vitakatifu.
Lakini kati ya upendo na tendo la ndoa nini kitangulie? Kinachotangulia ni upendo, suala la haki ya ndoa hufuatia baadaye, najua wapo wasiokubaliana nami kwa kuona bila ngono hakuna mapenzi.
Nikikuuliza swali, hivi wanaouza mwili wanawapenda wangapi? Jibu uatakalopata hapo ni kuwa wao wapo kwenye biashara wala hawana mapenzi na mtu, kwa jibu hilo utajua ngono si penzi kamili.
Nachukua fursa hii kuwasifu wasichana wote wanaojua thamani ya miili yao. Kuwajua wanaume wasio wakweli, wanaotanguliza ngono mbele hawana mapenzi ya kweli bali mapenzi yao ni ya kutamani na wakiishaijua miili ya wapenzi wao, mapenzi huisha.Mwisho napenda kuwashauri wote wenye mapenzi ya kweli wasitangulize ngono mbele bali itakuja kwa sababu huyo ni mpenzi wako, kama kweli anakupenda haki yako ya ndoa lazima atakupa.Mapenzi huanza na upendo, sawa na kuandaa shamba lazima utalilima na kupanda mbegu. Ni ajabu kukimbilia kupanda kabla ya kulima. Kama mpo ndani ya ndoa usipopewa haki yako una haki ya kuona hakuna mapenzi, asipokupa wewe mpenzi wake anampa nani?
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment