Thursday, March 29, 2012

Zingatia haya ili usiumizwe tena 2012


TUMEKUTANA tena mwaka 2012, kwanza nawatakia wasomaji wa kona hii heri ya mwaka mpya. Nashukuru kuona kona hii inasomwa na watu wengi na kupata maswali mengi kila kukicha ukiwemo ushauri wa kuiboresha safu hii.
Hali hiyo imenipa moyo sana, leo tuzungumzie penzi linapovunjika nini kinatakiwa kifanywe.
Kumekuwa na utamaduni wa wapenzi wawili wakiachana, mmoja huamua kumuonyesha mwenzake yeye ni zaidi na kumuonyesha mpenzi wake mpya mbele ya macho yake wakiwa katika mikao au matembezi ya kimahaba kwa kushikana hapa na pale.
Wengi huamini kufanya vile ni kumkomoa, lakini mwisho wa mapenzi siyo vita bali ni furaha na upendo:
Lazima tujue mapenzi ya wawili yana muundo gani Mapenzi ya wawili ni mkataba kati ya wawili ambao wote kwa pamoja hutengeneza katiba yao ambayo ndiyo huwa muongozo wa uhusiano wao.
Mnapoanza mapenzi, kila mtu huukubali mkataba huo na kuahidi ataulinda kwa nguvu zake zote.
Ndani ya mkataba wa mapenzi, vitu vikuu huwa uaminifu, tabia nzuri, huruma, upendo na uvumilivu. Nataka tuangalie kitu kimojakimoja:

Uaminifu:
Katika maisha ya uhusiano, mpaka mnaamua kuwa wawili ina maana mmekubali kwa ridhaa yenu. Mmewaacha wengi na kuamua kuwa pamoja, hivyo mnatakiwa kulilinda penzi lenu kwa kuwa waaminifu.

Tabia nzuri:
Hii ndiyo inayobeba uwakilishi wa mwanadamu ndani ya nyumba, ndiyo nguzo imara ambayo itakufanya usimame popote kwa kujiamini.
Katika hili wengi hukosea wanapojiona wana sura na umbile zuri au fedha, basi huanza kuwanyanyasa wenzao kwa kujivunia walivyonavyo na kusahau hakuna kiumbe kilichoumbwa kwa ajili ya kukasirishwa.
Mara nyingi uhusiano wa watu huvunjika kutokana na tabia ya mmoja kuwa mbaya isiyovumilika.

Huruma:
Ndani ya uhusiano, huruma ni kitu muhimu sana, ukiwa nao, huwezi kumuumiza mwenzako.
Nyumba yenye huruma kwa wapendanao hudumu milele na kutenganishwa na kifo. Asiyekuwa na huruma, hufanya jambo lolote bila kujali maumivu ya mwenzake.

Upendo:
Huu ndiyo unaobeba kila kitu kwa vile mwenye upendo ana huruma, ni mvumilivu na tabia njema ndiyo asili yake. Wote mkiwa na upendo hata familia yenu itakuwa yenye tabia nzuri.
Hapa mara nyingi kumekuwa na tatizo kwa baadhi ya watu kuchagua watu hasa wanawake kuchukia ndugu wa mume na mwisho wa siku ndoa huvunjika.

Uvumilivu:
Huu ndiyo muhimu katika maisha yetu ya kila siku, wengi wasio wavumilivu, wamekuwa wakitengana na wenzao. Kuna vitu ambavyo tunatakiwa tuvumiliane kwa vile wanadamu ni viumbe wenye upungufu.
Kukosana ni sehemu ya maisha, lazima mvumiliane, mtangulize kusameheana na kuyasahau yaliyopita. Yapo ya kuvumilia, lakini si yaliyovuka mipaka kwa mtu kushindwa kujirekebisha.

Mwanadamu mwenye akili timamu, hujifunza kutokana na makosa na kuwa tayari kukosolewa na kuomba msamaha anapokosea.

No comments: