Wednesday, May 23, 2012

Makosa ambayo hupaswi kuyafanya kwenye uhusiano wa kimapenzi.


KUSHINDWA KUSOMA ALAMA
Zipo alama muhimu ambazo ni vema kuzijua na uzibaini kwa mwenzi wako kabla hujazama kwenye dimbwi la mapenzi. Bahati mbaya wengi hutawaliwa na papara, matokeo yake hushindwa kubaini vitu ambavyo vinaweza kumfanya apate uelekeo wa uhusiano wake.
Katika pointi hii, nashauri watu kwenda kwa mwendo wa kinyonga badala ya kupiga mbizi bila kujua kina cha maji. Kusoma alama muhimu kwa mwenzi wako mapema ni sawa na kutegua kitendawili. Itakusaidia kujua kama kweli uliyenaye ana mapenzi ya kweli au anaweza kuwa laghai.
Wengi wanapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi hueleza kuwa wanapenda, tena huweka wazi kuwa hisia zimeanguka kwa wale wanaowapenda. Hata hivyo, huacha mambo mengi ndani ya uvungu wa nyoyo zao. Wewe utakuwa mshindi, endapo utaweza kumsoma mwenzi wako na kumuelewa kinagaubaga.
Pointi hapa ni kuwa mwanzo kabisa wa uhusiano, yapo mambo mengi ambayo kila mmoja hujitahidi kuyazungumza. Hiyo huita kujiweka wazi lakini imethibitika kitaalam kwamba maelezo ambayo hutolewa ni asilimia 40 tu, zilizobaki hufichwa. Asilimia 60 zilizobaki utazifichua kwa kusoma alama muhimu.
Nyongeza ni kwamba mara nyingi wengi hujitahidi kusema uongo mwanzoni mwa uhusiano. Hata kama mtu anapenda lakini hudanganya hili na lile pengine kwa hofu, tahadhari au kama pointi ya kushinda penzi. Mantiki hapa ni kukutaka uwe makini na umsome mwenzako kwa undani kabisa.
 Katika kipengele cha kusoma alama muhimu, kuna vitu vya msingi vya kuzingatia ambavyo ni hivi vifuatavyo;

1)    Jamii: Mwenzi wako anasimama vipi na jamii yake? Usiingie kichwakichwa kwenye mapenzi na mtu ambaye hata jamii yake inamuona ni tatizo. Vilevile, yule ambaye ni muoga inabidi uanze kumtia wasiwasi mapema. Ni kwa ajili ya maisha yako, hivyo ni vema kuchangamka.
Hutakiwi kugundua muda umeshapita kuwa mwenzi ana tabia usizopenda. Mapema msome na umuelewe. Chunguza msimamo wake kwenye jamii, anavyojiamini, je, anaonesha kuwa na dira ya maisha. Kama hana uelekeo, unatakiwa kuachana naye haraka.

2)    Hisia: Zisome hisia zake, je ni mtu anayejali? Unatakiwa kujua kama hisia zake zipo karibu kwa kiasi gani. Atakapotakiwa kukutimizia haki yako ya faragha, atakuwa tayari kwa wakati? Ni aibu mmeshakuwa na uhusiano kwa muda mrefu ndiyo unaanza kulalamika kwamba mwenzi wako hakutimizii huduma ya uwanja wa wawili.
Lingine kwenye hisia, unatakiwa ujifunze kujua kama mwenzi wako ni mtu wa kulipuka au kinyume chake. Inawezekana ni kweli mwenzi wako anakupenda lakini akawa ni mtu wa jazba, tatizo dogo ‘anapaniki’ utadhani nyoka aina swila, kakanyagwa mkia. Mjue halafu umpime, je, unaweza kumvumilia? Jiridhishe mara mbili, vinginevyo bwaga manyanga.

3)    Muonekano: Ni kipengele kidogo muhimu ndani ya kifungu cha kushindwa kusoma alama kama sehemu mojawapo inayowafanya wengi kufanya makosa kwenye uhusiano. Muonekano si suala la baadaye, inatakiwa mapema sana umtathmini halafu ujiridhishe kama anakufaa au kinyume chake.
Ni aibu umeshaingia kwenye uhusiano, halafu baadaye unamsaliti mwenzi wako na kuanza kuwatolea macho wale ambao unaona ni wazuri zaidi. Hakikisha kwamba mwanzo kabisa kwenye uhusiano wako, unajiridhisha kuwa anao mvuto unaokutosha.

Itaendelea wiki ijayo.

No comments: