Monday, March 14, 2011

Si kila mtu ni mshauri mzuri katika maisha.

KUMEKUWA na tabia za watu kuingilia matatizo ya watu wakionyesha kutaka kutoa msaada ambao huwa kinyume chake.

Badala ya kutengeneza wanaharibu kabisa. Inakuwaje umekosana na mwenzako pengine kosa lenyewe lipo katika maisha yetu ya kila siku, kwa vile si wote tuliokamilika, lakini watu walishikie kidedea.
Kwa hali hiyo tatizo lolote ndani ya nyumba zetu kwa kulitoa nje laweza kuwa silaha ya kuwaangamiza.

Si wote waliofurahia utulivu wenu, wapo watakaokuvunja moyo kwa kuongeza maneno yao ambayo kwa mtazamo wako wa haraka utaamini kabisa watu wale ni wema lakini mwisho wa siku unagundua ulifanya maamuzi kwa faida yao.

Nasema hivi kwa nini?
Nina mfano hai katika tukio moja siku za nyuma lililotokea Marekani la mwanamuziki Chris Brown kumpiga mpenzi wake Rihanna, jambo lile ni la kawaida kwa wapenzi kukosana hata kufikia kupigana.
Lakini jambo lile lilipofika mbele za watu kuna watu walitaka kujenga umaarufu kupitia tatizo lile. Walilisimamia kidete na mwisho wa siku wawili wale walitengana.

Simamini kama Rihanna baada ya kupigwa na mpenzi wake uamuzi wake ulikuwa kuachana na Brown, pengine baada ya tukio lile hasira zilitawala lakini kama angekaa chini angeweza kutuliza hasira zake na kumsamehe mpenzi wake. Lakini shinikizo la kila mtu ndilo lililomfanya Rihanna kuamua kuachana na Brown.

Sikutaka kisa hiki kiwe mada ya leo, bali nilitaka kutoa mifano hai ambayo huvunja penzi la wawili hata kama mnapendana. Mara nyingi panapotokea tatizo ndani ya uhusiano si wote washauri wazuri ndiyo maana kuna siku nilielezea sababu za mtu kutousemea moyo wa mtu.

Katika uhusiano kuna kitu Uvumilivu:
Huu ndiyo uliobeba mambo mengi katika uhusiano na hadi leo kuna watu wameishi muda marefu katika ndoa zao. Si kwamba katika maisha yao waliishi kama malaika, bali walivumiliana.

Haohao kuna kipindi mazungumzo yao ya ndani yalishindikana lakini wazazi au watu wenye busara walipowakalisha chini waliwasikiliza na kumaliza tofauti zao.

Siamini waliomshauri Rihanna aachane na Brown katika uhusiano wao hakuna migongano, wanaishi kama malaika wasiotendeana makosa. Tumeshauriwa tutenganishe ndoa za watu zilizokosa suluhu ya kuwa kwao pamoja kuna hatari siku za mbele. Lakini tatizo la kawaida ni kupatanisha, hata vitabu vya dini vimemsifu mpatanishaji na si mvunjaji.

Lakini matatizo ya Brown na Rihanna ni ya kawaida si ya watu kuyabebea bango ili kuwatenganisha wawili hao. Nimekuwa nikiendelea kutumia mfano huu baada ya kuona baadhi ya watu wamekuwa wakifurahia kutengana kwa watu na si kuwaunganisha.

Hii imekuwa hasa katika jamii yetu mtu akikueleza tatizo lake badala ya kumpa ushauri wa kujenga wewe unabomoa kabisa.

Nataka nizungumze kitu kimoja, katika maisha yetu kukosana ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, kiumbe mwenye mapungufu. Kama mnapokosana kitu cha kwanza itafute suluhu ndani kwa kuzungumza na mwenzako, pengine alifanya kwa hasira lakini ikitulia uweza kugundua kosa lake.

Pili kama ndani itashindikana basi tumieni wazazi wa pande mbili au watu wazima wenye busara. Na hapo ikishindikana mnaweza kwenda mbele zaidi hata katika mabaraza ya usuluhishi, lakini kwa watu waliokubali mioyoni mwao kuwa kitu kimoja kuvumiliana kwa shida na raha kwa uzima na ugonjwa ni wepesi kurudi katika ubinadamu na kumaliza tatizo lao.

Namalizia kwa kusema, linapotokea kosa lolote usikurupuke kwanza kulipeleka mbele za watu, lipime ni bahati mbaya au makusudi je, wewe upo sahihi kila siku. Ukipata jibu ni rahisi kumsamehe mwenzako.

Jiepushe kulitoa mbele za watu kila tatizo lako la ndani, pia usikubali kila ushauri. Upime kwanza kabla ya kuupokea na kuufanyia kazi.

No comments: