Sunday, August 3, 2014

Kuna umuhimu gani wa kuwa na mwenzi wa maisha?

HAPANA shaka mtakuwa wazima wa afya njema na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku kama kawaida. Kwa upande wangu mimi ni mzima wa afya njema kwa uwezo wa Maanani.

Nikukaribishe tena katika mada yetu ya leo baada ya wiki iliyopita kumaliza mada ya kutambua thamani ya mapenzi.
Kabla sijaanza rasmi, niwakumbushe kwamba kitabu changu cha Joseph Shaluwa…Lets Talk About Love kipo katika hatua za mwisho kabisa ya kuingia mitaani.

Ni kitabu chenye mada nyingi za mapenzi pamoja na Love Messages zenye ujumbe murua wa mapenzi kwa ajili ya kumtumia mpenzi wako. Si cha kukosa.

Sasa tuanze mada yetu…hivi umewahi kujiuliza kwanini tunakuwa na wenzi wa maisha? Kwanini mapenzi yakawepo? Kwanini wewe una mpenzi na ikitokea mkawa mmehitilafiana unakosa raha? Sina shaka kuwa katika hili, kila mmoja anaweza kuwa na fikra zake mwenyewe, lakini leo nitafafanua sababu za msingi zaidi zinazowafanya wapenzi kuwa pamoja na hatimaye kuishi katika ndoa.

Lakini kabla ya kufika mbali zaidi hebu jiulize swali moja, mapenzi humaanisha nini hasa? Kimsingi mapenzi ni hisia za watu wawili ambazo hukutana pamoja zikimaanisha upendo wa dhati. Pendo hukamilika ikiwa wawili hao kwa wakati mmoja wakahisi hisia hizo, ingawa wakati mwingine mmoja ndiyo huwa wa kwanza kuanza kuhisi hisia hizo.

Wakati mwingine inawezekana mkajikuta mmependana tangu siku ya kwanza tu mlipokutana, lakini wengine huchukua muda mrefu kidogo kabla hisia hizo hazijachukua nafasi.

Wengine hutumia nafasi hii vibaya, baadhi yao huamini kuwa ngono ndiyo mapenzi yenyewe, jambo ambalo halina ukweli. Hebu fuatilia vipengele vifuatavyo kwa makini bila shaka kuna kitu utajifunza!

KUSAIDIANA MAWAZO
Hili ni jambo la msingi zaidi katika uhusiano, mwanaume kama mwanaume, kwa uwezo wake peke yake, hata kama ana uwezo mkubwa kifedha, siyo rahisi kutimiza mipango yake ya kimaendeleo kwa uwezo wa akili yake peke yake.

Huu ni ukweli ambao wanaume wengi huukwepa kwa kuhofia kale kamsemo ka ‘tulichuma pamoja’, kimsingi unapokuwa katika muunganiko hasa kama mwenzi wako ana hekima chanya, ni wazi kuwa kutakuwa na kitu kinachoongezeka katika maisha yako. Fikra za kuwa mwanamke ni mtu wa kuzaa na kuangalia familia pekee, ni fikra za kizamani zisizo na mantiki.

Waswahili walinena ‘wawili ni wawili’, msemo huu una maana kubwa tena yenye msingi katika maisha yetu ya kila siku. Unapoamua kuingia katika ndoa, urafiki au uchumba ni wazi kuwa utakuwa umeshajiingiza katika ulimwengu wa wawili! Hii ina maana kuwa hata katika mambo yahusuyo maisha yako binafsi, siyo ajabu mwenza wako, akapinga au kukusapoti kulingana na maono yake juu ya jambo husika.

Fahamu kuwa, mwenza wako ana haki ya kutaka kujua kila utarajiacho kukifanya na anaweza kukupinga au kuhitaji pointi za kutosha za wewe kutaka kufanya jambo hilo. Heshimu mchango wa mawazo ya mwezako, bila kujali jinsia, cheo au elimu yake, ukishaamua kuwa naye, mmekuwa kitu kimoja. Hii ni kati ya sababu za msingi sana za kuwa na mwenzi wa maisha.

VIPI KUHUSU KUKUTANA KIMWILI?
Mapenzi ni kitu kingine na ngono ni kitu kingine, ingawa baadhi ya watu hufikiria kuwa ngono ni sehemu ya uhusiano, jambo ambalo sio la kweli hata kidogo. Kimsingi ngono huja baada ya tamaa kuingia kati ya hao wawili wanaopendana!

Hata hivyo kuna uwezekano mkubwa, ukawa na tamaa ya kufanya ngono na mtu hata kama huna mapenzi katika moyo wako. Kimsingi suala la kufanya ngono sio kithibitisho cha kuonyesha mapenzi ya dhati.

Baadhi ya walio katika uhusiano, hudanyanywa na kipengele hiki. Utakuta msichana anaambiwa na boyfriend wake kuwa, ili aonyeshe kuwa anampenda basi lazima akubali kufanya naye ngono, hata hivyo baada ya kumaliza kufanya ngono, kuna uwezekano mkubwa wa penzi hilo kuyeyuka!

Kuwa na msimamo, usikubali kuuza utu wako kwa gharama ya kumpenda mtu! Hebu soma kipengele kinachofuata kwa makini ili uweze kujua ni muda gani hasa ufaao kukutana kimwili na mpenzi wako.

MUDA MUAFAKA KUKUTANA!
Kimsingi suala la kufanya mapenzi halina kanuni, hakuna muda maalum wa kuanza kufanya mapenzi na mpenzi wako. Ngono ni hisia tu, tena basi huwa bora zaidi kama hisia hizo zikaja kwa wakati mmoja kati yako na huyo unayempenda!

Wataalam wa Saikolojia ya Mapenzi, wanashauri wapenzi wasishiriki tendo hilo mpaka pale watapokuwa wamefahamiana kiasi cha kutosha, hasa kupima afya kwakuwa magonjwa ya zinaa na ukimwi yamezagaa. Pamoja na hayo, suala la ngono halikwepeki ikiwa mtaruhusu kukutana sehemu tulivu mkiwa wawili.

Jambo la msingi ni kutulia na kujipanga, msifanye ngono kama sehemu ya mapenzi. Tambua kuwa ngono ni kitu kingine na mapenzi ni kitu kingine, hata kama mtakuwa mmeamua kushiriki katika kitendo hicho, mfahamu kuwa mnasterehesha nafsi zenu na sio kuonyeshana mapenzi ya dhati.

Lakini pia kuna vitu vingi ambavyo mnaweza kuvifanya ili kuepuka kufanya ngono, kama ni kweli mnapendana, mnaweza kutumia muda wenu vizuri kwa ajili ya kupanga maisha yenu yajayo, kucheza ufukweni pamoja na hata kupigana mabusu. Kila kitu kinawezekana ikiwa mtakuwa makini na wenye mipaka. Kwa leo naishia hapa, hadi wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii ambayo sina shaka itakuacha na mafunzo makubwa katika maisha yako ya kimapenzi.source ya mada hii>>>Muandishi Joseph shaluwa

No comments: