Monday, March 14, 2011

Nidhamu ya kweli kwenye mapenzi ni tulizo la moyo, uhuru-2


Omba Mungu kila siku akupe maisha yenye dira. Akujalie hekima za kuijadili hasi kabla ya kuiacha ipite. Vivyo hivyo kuitafakari chanya kwa kiwango kinachotosha. Soma kwa mtindo wa katikati ya mstari upate kunielewa.
Mungu ameniwezesha kuanza sehemu ya pili ya makala haya kwa mtindo huo. Ninaposema jadili hasi nakuwa namaanisha kuwa si kila unayemuona mbaya, anaweza kuwa hivyo daima. Kuna leo na kesho!

Inawezekana ulidanganyika kuwa ni mbaya. Usifanye vituko kwanza. Onesha ustaarabu, jiweke katika mazingira ya mtu mwenye hekima zake, acha kichwa kiwe kitupu ili baadaye ufanye uamuzi sahihi baada ya kujiridhisha kwa alama za kila upande.

Tafakari chanya! Hoja kuu ni kwamba aliye mbele yako usidhani ni mwema kabla ya kumchambua. Kuna waliohadaika kwa uzuri wa ukakasi kumbe ndani yake kuna kipande mti. Ukaona anang’aa kumbe yeboyebo. Tobaa!

Siku zote, unatakiwa uishi katika misingi ya adabu! Usithubutu kufanya yasiyofaa kwa kigezo cha kudhani mwenzi wako upo naye kwa kuzugia. Kesho mnaweza kuwa mume na mke, halafu ukakumbushwa uliyofanya ukajisikia vibaya.

Hapa naelekeza nidhamu ya kweli katika mapenzi ili uwe huru daima. Unatakiwa ujiweke salama wakati wote. Usiruhusu maovu yako yajulikane kwa mwenzi wako, kwani mwisho wake ni mbaya.

Ulikuwa mtu wa ‘totoz’, hizo ni ‘faulo’ za zamani, lakini hupaswi kuona ni ufahari, ukasimulia hovyo. Ipo siku utathubutu kumsimulia mkweo, matokeo yake siku unapeleka posa akakutoa mbio.

Ulikuwa mtu wa kuchuna mabuzi, usiku viwanja, ukawa unaruka ‘fensi’ nyumbani kwenu kwenda kulala hotelini, unadhani hiyo ina faida gani kumueleza mwanaume uliyeanza naye uhusiano juzi? Kuficha kucha ni nidhamu ya kimapenzi.

Unatakiwa ujitunze kuanzia mdomoni mpaka matendo hasa unapokuwa na mtu wako. Msome kabla ya kuanza kuzungumza historia ya maisha yako. Lakini kubwa ni wewe mwenyewe kujiuliza kama hilo unalotaka kumwambia lina manufaa yoyote.

Mathalan, mtu wako wa zamani alikuumiza, kwahiyo hakuna ubaya wowote ukimueleza kwa maana ili ajue linalokusumbua na afahamu jukumu lake la kukupa faraja. Ni kosa kumwambia jinsi unavyomkubali.
“Nimeachana naye lakini namkubali sana.” Hii ni kauli ambayo haipaswi kutolewa na mtu mwenye mawazo chanya katika mapenzi. Wakati unaongea hivyo, ni vizuri ukajua kuwa naye neno hilo akilisema kuhusu mtu wake aliyepita litakuchoma, utaumia.

Unashauriwa kisaikolojia kusema mabaya ya mwenzako aliyepita mbele ya mtu wako wa sasa. Hata hivyo, hutakiwi kufanya wimbo kwa maana kwa mwenye uelewa atajua bado unakumbuka penzi lake. Chuja ya kuzungumza.
Pointi hii inatoa mantiki kwamba katika maisha yako, hakikisha yanayomhusu mtu wako wa zamani unayajadili na wengine kama unaona inafaa, Si kuyaweka mezani kwa mpenzi wa sasa. Wengine wana nongwa, atakukumbusha kila siku mpaka utaona kero.

TOA KIPAUMBELEA KWA MWENZI WAKO
Ni kosa kubwa kumuweka mwenzi wako kwenye mzani. Katika hilo unashauriwa kumfanya namba moja kila siku. Wiki iliyopita nilieleza ‘ushpesho’ alionao kwako, kwahiyo ukimdharau aibu iwe kwako.
Tafakari kwamba baada ya kumaliza shughuli za kila siku, wewe na yeye mnalazimika kuwa chumba kimoja, mnalala kitanda kimoja na ikiwezekana mnawekwa kwa ukaribu na shuka moja. Unaamka asubuhi huna kovu, upo salama kabisa.

Mwenzi wako ni mlinzi namba moja wa maisha yako, kwahiyo unatakiwa kumjali wa kwanza kabla ya yeyote yule. Rafiki akisema nawe ukazingatia na kupuuza alichokitamka mwenzako ni kosa kubwa. Fanya mapitio ya tabia yako leo.

Ushauri kuhusu nidhamu yako katika mapenzi, inakutaka uachane na mawazo yenye kuganda. Kwa hali yoyote ile, unatakiwa kumkubali alivyo na umpe thamani inayostahili. Usihadaike na macho, dunia ni ya wawili kwa maana wewe na yeye!

POTEZA KUMBUKUMBU ZA KUUDHI

Iwe ulikosea mwanzoni au kwa namna yoyote ile, fanya juu chini uweze kupoteza kumbukumbu ambazo zinaweza kumuudhi mwenzi wako. Hili ni la lazima kwako ikiwa unataka kusimamia nidhamu ya kweli kwenye mapenzi.
Itaendelea wiki ijayo…by nico trac 0716 276 000

No comments: