Friday, March 18, 2011

Uvumilivu, unyenyekevu sifa zinazowashinda wengi!


INANIPASA nimshukuru Muumba wangu kwa kuwa yeye ndiye mlinzi na kiongozi wa maisha yangu, naamini bila yeye mimi na wewe tusingekuwepo, hivyo basi tuna wajibu wa kumshukuru kila wakati.

Bila shaka utakuwa mzima wa siha njema na macho na akili yako vimejiandaa kupata darasa hili murua kwa ajili ya maisha yako ya kimapenzi.

Yap! Leo nazungumzia mambo muhimu sana kwa wapenzi ambayo yanawachanganya wengi; uvumilivu na unyenyekevu! Kwa hakika ni maneno mepesi kuyatamka, lakini yana maana pana sana katika ulimwengu wa mapenzi.
Labda niweke wazi jambo muhimu, katika mada hii nitazungumza zaidi na rafiki zangu ambao wapo kwenye ndoa. Nazungumzia unyenyekevu na uvumilivu katika ndoa bila kujali jinsia, je ni utumwa? Hapa kila mmoja atakuwa na jibu lake, lakini leo nataka kuwapa ukweli wa kitaalamu.
Kuna usemi usemao ukitaka kujua uhondo wa ngoma uingie ucheze, wengine pia husema ukitaka kujua utamu na uchungu wa ndoa basi uwe mwanandoa.
Semi hizi zina ukweli ndani yake, wewe ambaye hujaingia kwenye ndoa naamini si rahisi kujua shida ama starehe apatazo mume ama mke ndani ya ndoa, pengine kama utazijua ni kwa kuzisikia kwa wanandoa ambao wanaeleza maisha yao.

Hata kama utayasikia hutajua ukweli yampatayo mwenzio mpaka yakukute mwenyewe kwani mengi huwa ya siri za ndoa. Kuna matatizo mengi wapatayo wanandoa, ukiniambia nitaje matatizo yaliyopo katika ndoa za watu  nitaeleza mengi sana kutokana na uzoefu wangu pamoja na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa mambo ya mapenzi.
Lakini wakati nikizitaja kero za ndoa pia kuna upande wa pili ambao ni furaha, kuna mengi mazuri wayapatayo wanandoa wanapokuwa katika ndoa zao.

NDOA NI NINI HASA?
Ndoa ina maana kubwa sana katika maisha ya binadamu, hata hivyo ina tafsiri nyingi kulingana na imani au mahali ndoa ilipofungwa! Kwa Wanasaikolojia wa Mapenzi ndoa ni ukamilifu wa makubaliano ya muungano wa mwanamke na mwanaume wenye kupendana kwa lengo la  kuishi pamoja kama mume na mke kulingana na sheria ya  dini,  mila au desturi za sehemu fulani wakiwa chini ya sheria ya nchi.

Pamoja na tafsiri hiyo ambayo hutambuliwa na wataalamu wa mambo ya mapenzi, hawashauri wanandoa kuachana, maana kama waliungana kwa upendo basi wanapaswa kuishi kwa upendo na kusikilizana siku zote, huo ndiyo upendo wa kweli ambao Wanasaikolojia wa Mapenzi wanautambua.

NDOA INALINDWAJE?
Hapa ndipo kwenye msingi wa mada yetu, unapoingia kwenye ndoa kitu cha kwanza unatakiwa kufikiria jinsi ya kuilinda ndoa hiyo kwa gharama yoyote! Kuingia kwenye ndoa na kutoka baada ya muda mfupi ni kujitafutia laana ambayo haina ulazima wowote.

Hapa unatakiwa kufikiria mpaka mwisho wa uwezo wako wa kufikiri ili ndoa yako idumu na usije ukajikuta umeingia katika laana hiyo. Linapokuja suala la ulinzi wa ndoa yako, utashindwa kumnyenyekea mpenzi wako?

Unatashindwa kumvumilia mpenzi wako kwa sababu utajihisi wewe ni mtumwa wa mapenzi? Wapi imeandikwa hii? Mathalan mkeo anaumwa na kwa bahati mbaya hamna msichana wa kazi, je utashindwa kumsaidia kazi kama kupika, kufua, kuosha vyombo na kazi nyinginezo kwa sababu tu, wewe ni mwananume? Haingii akilini hata kidogo.

Rafiki zangu, hii ni mada ambayo inahitaji umakini wa kutosha kuweza kuelewa ninachokizungumzia. Ninaposema uvumilivu namaanisha nini hasa? Twende tukaone hapa chini.

UVUMILIVU
Katika maisha anayohitaji kuyavumilia mwanadamu ni maisha ya ndoa. Ndoa inakuwa na mambo mengi sana, kutunza familia, kupeana haki za nyumba, kusaidiana na kuvumiliana katika vipindi vya dhiki na faraja na mengineyo.

Ukarimu, uaminifu, upendo wa kweli ni kati ya chachu za kudumisha penzi na kamwe halitaweza kuchuja. Unapooa au kuolewa lazima ufahamu kuwa unakuwa umejenga undugu baina ya familia yako na ya mwenzio.
Katika kuishi kwenu huko utakutana na matabaka mengi, watu hutofautiana tabia, mfano wewe mwanamke umeolewa, mumeo akaleta ndugu, yaani wifi zako. Unatakiwa kuwasoma wifi zako tabia ili uweze kuendana nao.

Katika hili, ili uweze kufanikiwa unapaswa uwe na busara, mvumilivu, mnyenyekevu, na kuonesha kuwajali, hii inaweza kukusaidia sana kwani watakapokutendea mambo ya ajabu nawe ukaanza kuwaropokea matusi, utakuwa unajingiza kwenye migogoro ambayo mwisho wake huweza kuwa mbaya zaidi kwako kuliko kwao.

Kumbuka kuwa Mungu ametuumba kila mtu na udhaifu wake, ndiyo maana unaona wanandoa wengi wanajikuta wakizikimbia ndoa zao kwa kutendwa na wandani ama ndugu wa wandani wao, wakati mwingine mume anaweza kuwa hajui, unayepaswa kumweleza ni wewe.

Wakati unamweleza lazima uzingatie heshima na busara ambayo haitaonesha kwamba umedharau ukoo wao. Siyo unaanza kusema: “Nyoo! Umeniletea ukoo wenu hapa, chakula hakitoshi! Nitawafukuza!”

Kwa kauli hiyo utaonekana limbukeni, kaa naye chini zungumza naye kwa ukarimu mweleze ni jambo gani  linalokunyima uhuru wewe kama mkewe wa ndoa. Usimfiche, mwambie kwa upendo: “Mume wangu, kuna jambo wifi amenitendea sijui kama anaona ni kosa lakini miye naona amenikosea, mweleze asirudie tena.”

Kauli hiyo hapo juu ni tiba tosha kwa mumeo. Tena hakikisha wakati unamweleza haya mpo peke yenu chumbani na huenda ni baada ya kumpa haki yake. Ni kauli nzuri ambayo itamjenga na kwa hakika atalifanyia kazi jambo hilo.

Huo ndiyo uvumilivu ninaouzungumzia, siku zote wewe ndiye unayetakiwa kuwa na uchungu na ndoa yako. Kabla ya kuzungumza jambo lolote fikiria mara mbili, halitasababisha matatizo kwako? Ukipata matatizo au kuachika huyo wifi yako atakuwepo? Jibu ni hapana! Utakaporudishwa kwenu, utawaangaliaje wazazi wako ambao walikulea katika malezi mazuri na kukufunda vyema? Ni nini kama siyo aibu mtoto wa kike utakuwa umewapelekea wazee wako?

Kaa chini, fikiria kwa makini kabla ya kuamua jambo lolote linalohusu ndoa yako. Kumbuka kuwa kuingia kwenye ndoa ni kazi ngumu lakini kazi ngumu zaidi ni kuhakikisha unailinda ndoa hiyo iendelee kuwa hai siku zote.

Hapana shaka siku mnasherehekea miaka 10 au jubilee ya ndoa yenu, utakuwa ukijimiminia sifa kwamba kama siyo uvumilivu wako usingeweza kufikia hatua hiyo. Rafiki zangu, napenda sana kuendelea lakini nafasi yangu haitoshi, hadi wiki ijayo tena katika sehemu ya mwisho ya mada hii. USIKOSE!

No comments: