Ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba kwa rehema zake Mwenyezi Mungu umzima bukheri wa afya.
Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nataka kuzungumzia kitu ambacho wengi wetu tumekuwa tukikipuuza sana lakini kimethibitika kuwa na nafasi kubwa ya kuliboresha penzi la wawili waliotokea kupendana kwa dhati.
Nazungumzia ishu ya wapenzi kununuliana zawadi. Hapa sizungumzii zawadi ambazo wengi wetu tumekuwa tukinunuliana siku za Sikukuu kama vile Iddi, Krismasi, Valentine na nyinginezo bali namaanisha zawadi nje ya siku hizo.
Kumtumia mwenzi wako zawadi ni kati ya mambo ambayo humfanya afurahie uhusiano wake na wewe. Hata hivyo, hakuna zawadi za moja kwa moja ambazo ni rasmi kwa ajili ya wapenzi lakini ni vyema ukamtumia zawadi kulingana na mapenzi yake zaidi.
Kwa kuwa wewe unamfahamu zaidi mwenzi wako, unaweza kujua zawadi gani ni nzuri zaidi kwake au anayopendelea kuliko aina nyingine.
Wiki hii nimechambua aina kuu za zawadi ambazo ukimtumia mpenzi wako utamteka hisia zake na ataona unamjali.
Mavazi
Mavazi ni kati ya zawadi ambazo zitamfanya mpenzi wako azidi kukupenda na kuwa karibu zaidi na wewe.
Aina ya nguo ambazo unaweza kumtumia mpenzi wako ni zile ambazo unaamini atavutiwa nazo au zile ambazo zitampendeza na kumfanya aonekane nadhifu.Hata hivyo, zipo aina za mavazi ambazo zimependekezwa zaidi kwa ajili ya wenzi kutumiana wanapokuwa mbali na hata wanapokuwa karibu.
Kama wewe ni mwanamke unataka kumtumia mpenzi wako wa kiume, mavazi yafuatayo yanafaa zaidi. Saa nzuri ya mkononi, nguo za ndani, lakini lazima uzingatie rangi ya bluu, bluu bahari au nyeupe kimsingi zisiwe za rangi zinazoficha uchafu.
Zingine ni fulana za ndani ‘singlendi’, fulana, mkanda wa suruali, simu ya mkononi, vitambaa vya jasho n.k. Hakikisha katika zawadi hizo, unaambatanisha na manukato mazuri hasa yale ambayo unajua atayapenda.
Haishauriwi kumtumia suruali au shati kwa sababu inaweza kuwa kubwa au ndogo, hivyo kupunguza ladha ya zawadi hasa kama atakuwa ameipenda sana.
Zawadi za aina hiyo, unaweza kumpa mwenzi wako ofa ya kwenda kuchagua moja kwa moja dukani lakini kama unajua saizi yake na una uhakika akivaa atapendeza, ruksa kumnunulia vitu hivyo na tena utakapopatia saizi yake vizuri ataamini uko makini naye na unampenda kwa dhati.
Kama wewe ni mwanaume na unataka kumtumia mpenzi wako wa kike zawadi, lazima uwe makini sana! Mavazi yaliyopendekezwa hapa ni pamoja na batiki (gauni, blauzi na sketi, blauzi yenyewe n.k), hereni, bangili, mkufu, simu ya mkononi, saa ya mkononi, nguo za ndani (kulingana na mapendekezo yake, kwa jinsi umjuavyo), sidiria, viatu n.k.
Kama umesoma vizuri utaona mwanamke anaweza kununuliwa vitu vingi zaidi (hasa nguo) tofauti na mwanaume. Hii inatokana na aina za mavazi na saizi zao kukaririka kirahisi zaidi au kutokuwa na saizi ya moja kwa moja. Mathalan, batiki, sketi na blauzi na vinginevyo. Kama kawaida, mavazi haya, ambatanisha na manukato mazuri, hasa yale ambayo ndiyo anayopendelea mpenzi wako.
Maua pia ni kati ya zawadi zinazopendekezwa na wataalamu wa mambo ya mapenzi. Maua ni mazuri sana kwa mwezi aliye mbali, lakini ni vyema kuzingatia na umbali uliopo kati yenu, kwani maua huweza kusinyaa kabla ya kumfikia (hasa kama ukimtumia yale halisi, kwani ndiyo haswa mazuri).
Hata hivyo, zipo zawadi nyingine ambazo unaweza kumtumia mpenzi wako kwa kuangalia vitu anavyovipenda sana.
Hii ni njia pekee ya kuonesha ubunifu wako na jinsi unavyomjali hata akiwa mbali kwa kumtumia vitu ambavyo huwa anavipenda lakini alipo hawezi kuvipata!
Mathalan, mpenzi wako anapenda sana zabibu lakini amekwenda mkoa ambao vitu hivyo havipatikani kwa urahisi, hii ni nafasi yako kumtumia.
Mathalan unajua kabisa anapenda sana kusoma vitabu lakini sehemu aliyopo hawezi kupata, basi nunua majarida, magazeti na matoleo yote ambayo hajayapata kisha mtumie, hakika utakuwa umemfurahisha sana na kumfanya afurahi kupata vitu hivyo.
Kwa leo naomba niishie hapo, lengo ni kukufahamisha kwamba zawadi ni kitu muhimu sana katika kuliboresha penzi lenu. Kwanza mpenzi wako aamini kwamba unampenda lakini pia unamjali.
No comments:
Post a Comment