Wednesday, June 6, 2012

Mwanamke anayefaa kuolewa ni yupi hasa?

Add caption

NI siku nyingine tena tunakutana katika ukurasa huu kwa lengo la kupeana mawili matatu juu ya mambo ya uhusiano na mapenzi. Nawashukuru wote ambao mmekuwa mkinipa changamoto mbalimbali juu ya uboreshaji wa safu hii.

Rafiki zangu, leo nataka kuzungumzia jambo muhimu sana katika maisha ya mapenzi hasa kwa vijana ambao wanafikiria kuoa. Natambua kwamba wengi huwa wanafikiria sana kuhusu aina ya wanawake wanaofaa kuolewa.

Katika fikra hizo, kuna ambao hufikiria zaidi suala la mazingira mwanamke husika alipozaliwa na kukulia. Yaani wanafikiria kuhusu ubora wa mwanamke aliyezaliwa kijijini au mjini.

Kila mmoja huwa ana wazo lake, akiwa na utetezi wa anachokiamini, lakini ukweli halisi ni yupi? Wewe unaonaje?
“Mimi nimeoa kijijini kwetu huko Saweni Juu, Same naishi na mke wangu mwaka wa tatu huu kwa amani tele. Ananiheshimu, ni mchapakazi na sijawahi kusikia tetesi mbaya kuhusu yeye hata mara moja. Nampenda sana kwa kweli,” Oscar Genesis, mkazi wa Tandale Kwa-Mtogole, Dar alisema alipokuwa katika mahojiano nami.

Wakati Oscar akisema hayo, Francis alikuwa na haya ya kusema: “Kuoa mwanamke kijijini ni hatari sana, unaweza kumleta mjini akiwa hajui kitu, lakini akishaujua mji tu anaanza kukusumbua. Mimi naona ni bora mwanaume akaamua kuoa mwanamke wa mjini ambaye anajua kila kitu, hatamsumbua maana kila kitu anakuwa ameshamaliza.”

Rafiki zangu, ukweli ni upi hapa? Kwanza nitaanza kwa kuwachambua wanawake hawa waliokulia katika mazingira mawili tofauti kabla ya kuendelea na uchambuzi zaidi.

UKWELI KUHUSU MWANAMKE WA KIJIJINI
Hivi ni kweli kwamba mwanamke wa kijijini ni bora zaidi kuliko wa mjini? Wapo wanaofikiria hivyo, lakini hapa nitakupa mazuri na mabaya yake, ambayo bila shaka yatakupa mwanga wa uchaguzi wa mke bora.

Mwanamke huyu anaelezwa kuwa na heshima kupindukia, siyo mkaidi, muelewa na mwenye nidhamu sana kwa mumewe. Hana makuu, hapendi starehe, anajali familia, ndugu wa mumewe na hata marafiki wa karibu na mume wake.
Anajua shughuli za nyumbani kama mke, lakini pia ni mtafutaji mzuri kwani mara zote hujishughulisha na biashara ndogo ndogo au kilimo.

Ni mwepesi kuelewa mambo, hasa kama anakatazwa au kuonywa. Anajua nafasi yake kama mke na ‘anacheza’ ipasavyo katika nafasi hiyo. Anaweza kuishi maisha ya aina yoyote.
Wakati uzuri huo ukianishwa, pia yapo mabaya ambayo yanasemekana mwanamke wa aina hiyo anakuwa nayo. Inaelezwa kwamba, asilimia kubwa ya mwanawake wa kijijini hajaenda shule!
Wengi huishia darasa la saba na kuolewa au kubaki nyumbani. Hili huvumbua kasoro nyingi nyuma yao, lakini kubwa zaidi wanakuwa hawana ufahamu wa mambo mengi.

Hawajui dunia inaendaje, mawazo yao siyo endelevu na siyo mapana. Hawana mipango ya muda mrefu, wanawategemea zaidi waume zao kwa kila kitu.
Baadhi yao huamini kuolewa ndiyo kila kitu na mume ndiyo kila kitu katika nyumba. Kwamba anaweza kufanyiwa kila kitu na mumewe kwa sababu eti ni mume! Siyo mwepesi wa kugundua makosa au matatizo.

Ni rahisi kufanya jambo baya na kung’amua baadaye sana ubaya wa jambo alilolifanya. Siyo mjanja, ni mzito kifikra. Muoga kujifunza. Baadhi yao hupelekwa unyagoni ambapo hufundwa na kuelekezwa anayotakiwa kuyafanya kama mwanamke. Mara nyingi hupelekwa huko akiwa na umri wa kuanzia miaka 13-15, akitoka huko anaamini tayari yeye ni mtu mzima!

Anaanza kufanyia mazoezi aliyofundishwa. Mafunzo yanayotolewa huko yanadaiwa kuwa si mazuri sana, kwani mtoto hufundwa mambo mazito ambayo anapaswa kufundwa mwanamke ambaye anajiandaa kuingia kwenye ndoa. Kuharibikiwa huku mapema, wakati mwingine kunaweza kumuathiri hata anapokuwa mtu mzima na familia yake.

Haya ndiyo baadhi ya mambo yanayodaiwa kuwa mabaya na mazuri ya mwanamke wa kijijini. Kwa leo tuishie hapa, wiki ijayo tutaendelea katika sehemu ya pili ya mada hii.

No comments: