"NI lazima niolewe kwa sababu wadogo zangu wameshaolewa, aaah hapana bwana wadogo zangu wameshaoa kwa hiyo ni lazima na mimi nitafute mtu wa kuoana naye,”ndivyo wanavyojisemea baadhi ya watu.
Kuna wengine wanaoa kwa sababu wameshinikizwa. Lakini ukweli ni kwamba ndoa yoyote ambayo haina upendo wa dhati, ni kosa kubwa.
Katika hali kama hii baadhi ya watu huwa tayari kuoana na yeyote anayepita mbele yake hata bila kuangalia kwa makini kama kweli mtu huyu ni mzuri kwake au la.
Hali hii ya kukubali kuolewa kwa sababu wadogo zako wameolewa, huchangia kasi ya ndoa kuvunjika, kwa sababu watu wanaoana pasipo kupendana kwa dhati.
Ndoa ni nzuri, lakini lazima uelewe kuwa unapaswa kuoana na mtu kwa sababu umemuona anakufaa hasa baada ya kumchunguza kwa makini na kuamini kweli anakufaa.
Usiingie katika mapenzi kwa unafiki, unafiki wa kusema aaah kwa vile baba amesema nikikataa ataniona sina adabu....kumbuka ndoa ni maisha yako si ya baba yako wala mama yako. Ukipata shida utakayeumia kimaisha ni wewe, si mwingine.
Uongo pia ni suala baya katika uhusiano…mwingine ni mnywaji mzuri wa bia na aina nyingine ya vileo lakini ukimuuliza anakwambia mimi simwi wala sivuti, naye anakwambia aaah hata mimi bwana, yaani sipendi kabisa kunywa.
Kama wewe ni mnywaji, sema mimi nakunywa ili mwenzi wako ajue aina ya mke au mume ambaye atakuwa naye. Ingawa ni hatari zaidi kwa mwanamke kulewa, kuliko mwanaume hasa katika suala la uaminifu wa ndoa, lakini maisha ni makubaliano.
Ni rahisi mwanaume mlevi kubaki mwaminifu, lakini ni vigumu kwa mwanamke mzuri mlevi kubaki mwaminifu kwa ndoa yake, kama unabisha shauri yako.
Ninachotaka kusisitiza hapa ni umuhimu wa mtu kuwa muwazi hasa pale wanapoanzisha urafiki, hii itakusaidia hata katika siku za baadaye za uhusiano wenu kuishi kwa amani.
Eeeh bwana maana mumeo atakuwa anajua kwamba nimeoa mke mlevi, nimekubali, hakutakuwa na ugomvi, maana ulishamwambia kwamba mimi bila kunywa usingizi haupandi...siku ukifungwa jela au ukiumwa sijui utalalaje ? Mimi sijui, lakini ninachotaka kusema kwenye kipengele hiki ni kwamba wapo watu wanasema hivyo kwamba eti asipokunywa hajisikii vizuri, kitu ambacho si kweli.
Unafiki mwingine ni wa tabia katika mazungumzo nk, ndugu yangu kama unaelekea kuoa au kuolewa, ni vizuri siku moja tafuta uwezekano wa kugombana na mwenzi wako, uone kauli zake zikoje, anajibu vipi malalamiko.
Kuna wengine wanajifanya wakimya, lakini wana lugha chafu kana kwamba wametoka kwenye shimo la choo. Ni wiki mbili tu zilizopita kuna mama mmoja alimchukua binti kanisani awe mfanyakazi wake wa ndani.
Huyo binti alikwenda kanisani, kweli walikuwa wakimsifia kuwa ni mzuri kwa namna alivyokuwa akionekana....siku moja kwa bahati mbaya bosi wake alipata safari ghafla kiasi kwamba aliacha fedha kidogo nyumbani.
Akiwa huko mbali na nyumbani akapata ujumbe mfupi kutoka kwa mfanyakazi huyo wa ndani ??ndio fedha gani hiyo umeniachia, mimi huwa sinywi maji ya bomba, nitumie fedha ya kutosha ninunue maji ya dukani, nikinwa ya bomba tumbo linauma?
Huo ni ujumbe wa kutoka kwa binti ambaye kanisani anaonekana ni mtakatifu. Kama hiyo haitoshi wakati bosi wake yuko mbali ikabainika akawa analala na kijana mmoja wa mtaani hapo, bosi akalazimika kumfukuza kwa sababu ya kuona anakwenda kinyume na alivyokuwa akimtarajia.
Unafiki hauko tu katika mapenzi, bali hata maofisini, mwingine anaweza kukuchekea na ukaamini ni rafiki, kumbe anakuchimba...eeeh bwana wengine ni maarufu wa kutangaza mabaya ya wenzao, huku wao wakijiona ni watu safi, wajuaji wa mambo nk.
Katika maisha ni vizuri kuwa kama ulivyo, simamia kwenye ukweli wala usikubali kuingia kwenye uongo ili upate hiki na kile, maisha tunayoishi ni mafupi, uko leo, hujui kama kesho utafika, yanini kuwa mnafiki? Yanini kusengenya wengine? Yanini kuwa mtu wa majungu, badala ya kuangalia mambo yako ambayo yatakusaidia uwe na maisha bora zaidi kuliko ulivyo sasa?
Tangu mwaka uanze umeshateta watu wangapi? Umeshafanya unafiki mara ngapi? Je, kati ya maneno unayozungumza kwa siku, mengi ni ya aina gani....unafiki, uongo au heri kwa wengine? Mimi sijui, lakini wewe unalo jibu, lakini kwa vyovyote itakavyokuwa ni vizuri katika maisha pendelea kuachana na tabia za kinafiki.
No comments:
Post a Comment