Sunday, March 27, 2011

Mpenzi wako amepoteza msisimko na wewe, nini cha kufanya?

SINA shaka kwa wiki mbili zilizopita wakati nazungumzia mada hii utakuwa umejifunza kitu kipya katika maisha yako ya kimapenzi. Inawezekana kabisa, ulikuwa unahisi mpenzi wako hana msisimko na wewe, lakini bado ulikuwa huna uhakika hasa!

Ni mada ambayo sina shaka itakuwa imekutoa mchanga na kukuingiza katika ulimwengu mpya wa fikra.
Rafiki zangu, kubwa zaidi ambalo mnatakiwa kufahamu ni kwamba, mpenzi wako si kwamba hakupendi, bali amepoteza ule msisimko wa kimapenzi na wewe. Si tatizo geni katika ulimwengu wa mapenzi.

Ni tatizo lililowaumiza wengi na wakati mwingine husambaratisha uhusiano wa wenzi mbalimbali kutokana na tatizo hili. Umewahi kujiuliza, mpenzi wako unampenda kwa moyo wako wote, lakini anafanya mambo yanayoonesha wazi kuwa hana msisimko tena na wewe, nini cha kufanya?
Utaachana naye au utaendelea naye kama kawaida? Hebu tuone kipengele kifuatacho...

SI SABABU YA KUMWACHA
Rafiki zangu, kuna tofauti kubwa kati ya usaliti na kupoteza msisimko. Aliyepoteza msisiko siyo kwamba amepoteza kwa hiyari yake, bali ni kwa bahati mbaya.

Yamkini hata yeye anatambua kuwa anaumwa, lakini hana jinsi, hawezi kusema, anajikuta anaishia kufanya vituko, si kwa kupenda mwenyewe bali kwa bahati mbaya. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, anapokea huwa anagundua baadaye, anaweza kulia sana kutokana na kitendo kile, akawa anazidi kujiumiza mwenyewe, lakini suluhusho akawa hana.

Wakati napokea simu na ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa wachangiaji wa mada hii wiki iliyopita, nilipata ujumbe kutoka kwa dada mmoja ambaye ni msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye hakutaja jina lake.
Ujumbe wake ulisomeka hivi; “Ahsante sana kaka Shaluwa kwa mada yako, imenigusa sana kwakweli.

Nasubiri kwa hamu sana hiyo wiki ijayo niweze kujua tiba yake. Nimeishi katika utumwa kwa muda mrefu sasa.”
Msomaji huyo anaweza kuwawakilisha wengine wengi wenye tatizo kama lake.

ALIYEATHIRIKA AFANYEJE?
Nimeona ni vyema nianze kwa kuzungumza na waathirika wenyewe wa tatizo hili. Kama maelezo yote hapo juu yanakuhusu na unajijua una tatizo hilo, ni vizuri kuwa makini na kipengele hiki.

Kwanza kabisa, kubali tatizo lako, halafu amini kwamba mwenzi wako hana tatizo isipokuwa wewe. Ukishajiweka katika hali hii ni rahisi kubadilika. Kama unahisi huwezi kubadilika au ni vugumu kurudi katika hali yako ya kawaida, zungumza na mpenzi wako na umweleze kila kitu kuhusu tatizo lako.

Tumia nafasi hiyo pia kuomba msamaha kwa mpenzi wako juu ya yote ambayo umeyafanya kwake na unahisi yalikwenda kinyume. Kuwa mkweli kwa kiwango hicho, kutampa nafuu kubwa mpenzi wako ya kukuweka sawa, maana atajua ulikuwa hufanyi makusudi bali unaumwa!
Fanya jitihada za pekee kwa ajili ya kurudisha msisimko wa kimapenzi kwa mwenza wako. Simu, sms, waraka pepe ni kati ya njia zinazoweza kukurejeshea msisimmo uliokuwa umepotea.

Kuwa naye karibu, cheza naye michezo ya kimapenzi, pendelea kushikana mikono mnapokuwa mmetoka pamoja n.k, hizo ni njia nzuri zaidi za kukufanya uwe na msisimko kama zamani.

JINSI YA KUMTIBU MUATHIRIKA
Hapa sasa tunaangalia pale ambapo wewe umegundua mwenza wako ana tatizo hili. Yapo mambo ya kitaalam unayopaswa kufanya ili kuweka mambo sawa hatimaye mpenzi wako arudi kwenye hali yake ya zamani.
Unajua cha kufanya? Twende tukaone...

Jiachie kwake
Akili na hisia zako zitambue kuwa huyo ndiye mpenzi wako wa kweli, kama hisia zako zitasema hivyo kwa kumaanisha, basi bila ya shaka utajiachia kwake kisawa-sawa!
Kujiachia kwake, kutamfanya aone jinsi unavyompenda na kuthamini penzi lake. Hapo utampa sababu ya kuanza kubadilika taratibu.

Mpe uhuru
Usimbane, mfanye awe huru kwa kila kitu. Wewe ni wake, kwahiyo huna sababu ya kumuwekea mipaka katika maeneo fulani. Uhuru huo utazidi kumsogeza kwako na kumfanya aanze kupuuza na kusahau kabisa aliyokuwa anawaza au kukuambia awali.

Mfundishe kwa kauli njema
Katika mapenzi kuna kukosea, kumbuka kwamba huyu ana matatizo, kwahiyo wakati mwingine anaweza akafanya kosa kubwa sana ambalo litakuudhi lakini ukishatambua kwamba mpenzi wako anaumwa, ni rahisi zaidi kumfariji!
Tumia ulimi wako vyema kwa ajili ya kumwelekeza na siyo kumfokea au kumtukana.

Mweleze alivyo na thamani
Thamani yake kwako ni kitu ambacho kinamuumiza kichwa kila siku, yawezekana hata machozi yake husababishwa na jinsi asivyoamini kama yeye ni wa thamani wako.
Hapa ni chaguo lako, kufanya chochote ambacho kitamfanya ajione wa thamani kwako. Kumshirikisha katika mambo yako hata yale ya siri sana, kutamfanya aione thamani yako bila hata kumwambia!

Mtengenezee furaha
Usikubali kuyaona machozi yake hovyo, siku kuwa mpigania furaha yake. Kama kuna kitu ameudhika ni vyema kumtuliza haraka.
Inawezekana kabisa siku moja ukawa umemuudhi, fanya haraka sana kumuomba msamaha ili mambo yaende sawa. Hakikisha anakuwa na furaha muda wote.

Thamini chozi lake
Anapokuwa katika matatizo ya kiafya au kifamilia, kiasi cha kulazimika kumwaga machozi, unatakiwa kuyathamini na kuyafuta. Kuwa naye karibu, mfariji na kumfanya asijihisi yupo peke yake.
Asione kwamba tatizo ni lake mwenyewe, mfanye atambe na aone kabisa kwamba hayupo peke yake, nyuma yake yupo mtu anayempenda ambaye atamthamini siku zote. Hii itamsaidia kwa kiwango kikubwa sana kumaliza tatizo lake.

Sasa ibuka mshindi
Unapofanya kitu kizuri na kufanikiwa, lazima ushangilie maana tayari unakuwa mshindi. Hii ni nafasi yako ya kushangilia na kujiona mshindi kwa kurejesha msisimko wa mwenza wako.
Nina imani umebadilika na utaendelea kufurahia mapenzi na mwenza wako.

No comments: