Monday, March 28, 2011

Unavyoweza kuitumia simu yako kulinogesha penzi lenu


Kuwasiliana kwa njia ya simu za mkononi ni moja kati ya njia bora za mawasiliano ya kuboresha uhusiano kwa wapenzi. Mwenzi wako anapokuwa mbali na wewe, kwa kutumia njia hii, unaweza kumsogeza karibu yako na kufurahia sana uwepo wake.

Unapompigia simu mpenzi wako hakikisha maneno yako yanakuwa laini, zungumza naye kwa unyenyekevu na kumtia hamasa ya kuzidi kuzungumza na wewe. Kadhalika unapomwandikia meseji, kaa chini na utunge, siyo unamwandikia ‘sema mtu wangu, uko shwari? Umeshakula?’ Hii ni meseji isiyo na hamasa yoyote ya kimahaba.

Unapaswa kumtumia sms za mapenzi, tungo za mahaba, maneno ya utani na vichekesho. Unaweza kumtumia meseji nyingi kadri uwezavyo kulingana na uwezo wako kifedha, ingawa mitandao mingi ya simu za mkononi siku hizi huwa na ofa maalum ya kutuma sms nyingi kwa gharama ndogo! Unaweza kujisajili kila siku kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano na mpenzi wako.

Pamoja na kwamba uwezo wako kifedha, muda na majukumu vinaweza kukufanya uamue idadi ya sms utakazomtumia mpenzi wako, lakini ni lazima umtumie angalau sms tano kwa siku.

Meseji hizo hutumwa kwa muda maalum, mathalani baada ya kuamka asubuhi unapaswa kumtumia ujumbe mzuri wa kumtakia asubuhi njema na mafanikio katika kazi zake za kutwa hiyo.

Mchana, mtakie mlo mwema na kazi njema, alasiri mtumie ujumbe wa kichekesho. Usiku, mtumie ujumbe wa kumpa pole kwa kazi, kisha malizia kwa kumtumia ujumbe mwanana wakati wa kulala.
Kama nilivyoeleza awali, unaweza kutuma meseji nyingi zaidi kulingana na uwezo wako na muda huku ukizingatia majukumu yako ya kazi.

Inawezekana mpenzi wako huko aliko ana kazi nyingi na ratiba zake zinambana sana, kama ndivyo unapaswa kuhakikisha humtumii meseji nyingi sana, kwani unaweza kumkera kwa milio ya simu kila wakati, muda ambao yeye hutumia kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuboresha maisha yenu ya baadaye.

Ni vyema kuangalia sana ratiba yake ya mchana, kwa suala la kumpigia simu na kumwandikia sms. Unaweza kumpigia simu angalau mara mbili kwa siku, baada ya hapo ukamwachia muda wa kufanya kazi, kwani si busara kumsumbua mwenzi wako anapokuwa ana majukumu kazini.

Hata sms zako, zisiwe nyingi sana kama nilivyoeleza awali. Usiku, ni muda mzuri sana kwako, kumfanya mwenzi wako awe karibu na wewe zaidi kimapenzi. Kwa kutumia simu mnaweza kuchati kwa muda mrefu mkitumia lugha laini za mapenzi, pia mnaweza hata kukutana faragha kwa kutumia simu zenu.

Mnaweza kufanya kila kitu kwa sauti laini zitakazoamsha hisia zenu na kujikuta kila mmoja akiwa anaridhika kwa kusikia tu, sauti ya mwenzi wake.tu kama inavyosomeka , kumekuwa na matatizo mengi katika matumizi ya simu kwa wapendanao. Tangu simu za mkononi ziingie, naweza kusema zimevunja ndoa zaidi ya milioni moja.

No comments: