Thursday, March 3, 2011

Unamalizaje migogoro na mpenzi wako?-Sehemu ya kwanza.



RAFIKI zangu, ni imani yangu mtakuwa wazima wa afya na mnaendelea na majukumu yenu vyema. Mimi ni mzima wa afya, nipo hapa kwa ajili ya kuwapa kilicho bora zaidi katika uhusiano na wapenzi wetu.

Nawashukuru wote ambao mmekuwa mkiwasiliana nami kwa njia mbalimbali, simu, sms, waraka pepe na katika ukurasa wangu wa Facebook. Ushauri na maoni yenu yananitia nguvu.

Leo tunaangalia mada muhimu sana katika mapenzi, nachambua juu ya migogoro ambayo inaweza kutokea kati yako na mwenzio, je, unaimalizaje? Unajua katika uhusiano wowote, lazima wakati mwingine kutokee kutokuelewana, vivyo hivyo katika uhusiano wa mapenzi lakini tatizo si migogoro, bali ni jinsi gani unavyoweza kutatua migogoro uliyonayo.

Hebu jibu swali hili, umewahi kugombana, kulumbana au kuwa na migogoro na mpenzi wako? Jibu lako litakuwa mwanga wa kuwa na uelewa wa kutosha katika vipengele vinavyofuata. Sasa tuanze moja kwa moja kwa kufahamu maana ya migogoro na malumbano.

Maana yake ni nini hasa?
Naweza kuita mgogoro, malumbano au ugomvi. Ni maneno matatu yenye maana zinazokaribiana, ingawa ukweli ni kwamba yana maana tofauti kidogo! Mnaweza kuwa na mgogoro na mwenzi wako lakini yasiwepo malumbano.

Kwamba inawezekana mpenzi wako amekukosea na ukawa mwanzo wa migogoro katika penzi lenu, lakini kutokana na uelewa wako na kukubali kosa mapema ikiwa ni pamoja na kuomba radhi, kukawa hakuna malumbano na mambo yakawa sawa.

Wakati huo huo, kunaweza kukawa na tatizo linaloweza kusababisha migogoro ambayo huzaa malumbano na mwisho wake ni ugomvi! Naamini tunakwenda sawa!

Kwa nini nimeeleza hayo? Nataka twende sawa, hatua kwa hatua katika mada hii ambayo naamini ni tatizo kwa wengi walio katika uhusiano. Baada ya kuona maana ya maneno matatu muhimu ambayo kwa hakika yanakaribiana, ambayo tunayajadili katika mada yetu ya leo, sasa tuone jinsi matatizo hayo yanavyotokea.

Chanzo cha tatizo
Migogoro ambayo nimeainisha hapo juu, haiwezi kutokea bila kuwa na vyanzo. Lazima kuna mambo ambayo yametokea kwanza, kabla ya tatizo husika kukua na mwisho wake kuanza migogoro, malumbano kabla ya ugomvi.

Kama wahusika hawatakuwa makini, mwanzo wa ugomvi ni mwendelezo wa kuachana hapo baadaye, jambo ambalo mwenye mapenzi na akili timamu hawezi kukubali likachukua nafasi. Hebu sasa pitia mambo hayo.

Penzi kupungua!
Yapo mengi ambayo husababisha migogoro katika mapenzi lakini kubwa zaidi ni kuchuja au kupungua kwa penzi. Unapokuwa na mwenzi wako, halafu kwa sababu ambazo unazijua mwenyewe unajikuta penzi limepungua, huo unaweza kuwa mwanzo wa migogoro.

Kila atakachokiongea utaona kero, kila wakati utakuwa mtu wa kukasirika na usiyependa kufuatwafuatwa! Katika upande mwingine, kama mwenzi wako amejikuta akiingia katika ushawishi na penzi lake kwako kupungua, ni mwanzo wa kuwa na mawasiliano mabaya na wewe, ambayo bila shaka lazima yatasababisha migogoro ambayo huzua malumbano kabla ya ugomvi.

Utashangaa mpenzi wako anakununia bila sababu za msingi, hana raha na wewe, hataki mzungumze chochote kuhusu penzi lenu, hapo ujue ni mwanzo wa migogoro.
Matatizo binafsi...

Hili pia linaweza kuwa chanzo cha ugomvi katika maisha ya wapendanao. Mathalani mwenzi wako ametoka kazini akiwa na matatizo binafsi kichwani, wewe kwa kutokujua unaanza kumuuliza kwa ukali.

Hebu soma mfano ufuatao; “Unakuja nyumbani umenuna, sijui una matatizo gani? Ndiyo yale yale, ugombane na wanawake zako huko nje, halafu unakuja kuninunia hapa nyumbani.” Hii ni moja kati ya kauli mbaya sana kwa mpenzi wako kabla ya kujua sababu ya ukimya na upole aliokuja nao.

Yawezekana ana matatizo binafsi, kwa nini uanze kumhisi vibaya? Tulia, fikiria kwa makini kabla ya kutamka chochote kwa mpenzi wako.

Msongo wa mawazo!
Kipengele kilichopita, hakina tofauti kubwa sana na hiki. Matatizo binafsi ni mwanzo wa kuwa na msongo wa mawazo. Pengine mambo yamemwendea kombo, amegombana na rafiki yake wa karibu, ameharibu kwa bahati mbaya mali ya kampuni n.k.

Mambo haya na mengine yanayofanana na hayo, yanaweza kusababisha mtu kuwa na msongo wa mawazo ambao utasababisha ashindwe kuwa na mawasiliano mazuri na wewe.

Kupungua kwa mawasiliano bora baina ya wapenzi ni mwanzo wa ugomvi, kwani kila mmoja atajiona yupo sahihi kwa sababu mwenye msongo wa mawazo anaamini njia sahihi ni kutulia au kujifungia chumbani akiwaza atakavyotoka katika matatizo yake, wakati anayetengwa na kununuwa ataamini mpenzi wake amepunguza mapenzi kwake.

Majibizano yake ambayo kwa hakika siku zote huwa hasi, ni chachu ya kuruhusu migogoro, malumbano kabla ya ugomvi kutokea. Mwanzo huo kama busara haitachukua nafasi, Kuachana ndiyo kitu pekee ambacho kinaweza kuchukua nafasi kwa wakati huo.

No comments: