NINA furaha sana moyoni mwangu kukutana nanyi tena wapenzi wasomaji wa safu hii namba moja kwa mada za mapenzi na uhusiano nchini. Bila shaka mmekuwa mkijifunza mambo mengi na kubadilika. Karibuni tena katika mwendelezo wa mada yetu iliyoanza wiki ya jana.
Hebu tuendelee kuona vyanzo hivyo kabla ya kwenda katika dawa yenyewe. Tuingie darasani!
Kutetereka kimaisha
Hili nalo huchangia ingawa siyo kwa kiasi kikubwa sana. Kushuka kimaisha ni hali ya kawaida ambayo huweza kumpata mtu yeyote aliye chini ya jua, lakini utafiti wa wanasaikolojia ya Uhusiano wanasema kwamba, kushuka kimaisha ni kati ya sababu zinazosababisha kuporomoka kwa hisia halisi za mapenzi.
Tatizo hili huwakumba zaidi wale ambao wapo katika uhusiano wa karibu zaidi waliooana au hata wanaoishi pamoja kwa muda mrefu.
Mwanasaikojia George K. Pollyns wa Ujerumani katika kitabu chake cha Love Season, anaelezea kushuka kimaisha kama mwanzo wa ugomvi ndani ya nyumba kutokana na furaha iliyokuwepo mwanzo kupunguzwa na ukali wa maisha.
“Lakini hata hivyo, penzi imara haliwezi kuyumbishwa na ukali wa maisha, maisha na mapenzi yanakwenda sanjari, lakini fedha na mapenzi yanatofautiana ingawa pia maisha na fedha ni kama ndugu.
“Umakini ni kitu cha kwanza kabisa kwa walio kwenye uhusiano ukizingatia ukitetereka kidogo tu, unaruhusu mwanya wa kuachana kuingia kati yenu,” ndivyo inavyoeleza sehemu ya nukuu katika kitabu hicho.
Naye Mwanasaikolojia Richard Manyota wa Tanzania, katika kitabu chake cha Saikolojia na Maisha, anaeleza kwamba, pamoja na kuwa ukali wa maisha ni chanzo cha kupungua kwa mapenzi, lakini yeye haamini sana katika hilo, ikiwa wapenzi hao wana mapenzi ya dhati mioyoni mwao.
“Ukiona hayo yanayotokea, basi ujue penzi la awali halikuwa la asili, unajua wengi wanashindwa kutofautisha, penzi la dhati na tamaa ya muda, hili ndiyo tatizo kubwa!” Sehemu ya nukuu katika kitabu chake hicho inaeleza.
Bila shaka, maoni ya Pollyns na Manyota yanaweza kukufanya ujifunze kitu fulani na kuwa na kitu kipya katika ufahamu wako juu ya maisha ya uhusiano, mapenzi na ndoa.
Kutojaliana
Kupungua kwa mapenzi na kutokumjali mwenzi wako, kunatajwa kama moja ya sababu za kuanzisha malumbano. Hili halina ubishi, kwani kama umezoeshwa na mpenzi wako kutoka kila mwishoni mwa wiki, halafu ghafla ratiba zinabadilika, lazima kutakuwa na matatizo.
Tatizo huanza pale mwenzi wako atakapokuuliza sababu za kubadilisha ghafla ratiba ambapo bila shaka hutakuwa na jibu yakinifu, hali itakayozusha ugomvi. Ni vizuri wapenzi wakapendana kwa dhati, kujaliana na kupeana taarifa mapema za mabadiliko yoyote ambayo yametokea.
Mathalani haupo sawa kiakili au umeyumba kidogo kimapato, basi ni vizuri ukamwambia mpenzi wako kwa sauti tamu ya upole: “Sweetie hali mbaya, mifuko imetoboka, wiki hii hatutaenda mahali popote. Itabidi tutulie nyumbani.”
Kauli kama hiyo, lazima mwenzi wako atakuelewa na kwa kiasi kikubwa mtakuwa mmeepusha migogoro ambayo si ya lazima. Lazima wewe uwe wa kwanza kuhakikisha kwamba unalinda uhusiano wako usiingie kirusi cha migogoro. Inawezekana kabisa rafiki zangu.
POKEA, KUBALI TATIZO
Hakuna haja ya papara wala hasira, matatizo katika uhusiano ni jambo la kawaida ambalo kiukweli unatakiwa kujiandaa kukabiliana na changamoto hizo.
Kubali tatizo, kisha tulia na panga jinsi ya kulimaliza kwa njia bora zitakazouacha uhusiano wako katika hali nzuri. Kwanini ubadilishe wapenzi kila kukicha? Unatafuta nini? Upe ubongo wako nafasi ya kufikiri.
Maamuzi ya hasira au kukomoa mwisho wake huwa ni machozi, epuka machozi ambayo hayana sababu. Siku zote, ukikubali kosa na kulipokea, ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye kutafuta njia za utatuzi.
UNATATUAJE?
Hapa ndipo umakini wa kiwango cha juu kabisa unapohitajika. Jinsi gani unamaliza matatizo yako? Unatumia ubabe au utaratibu?
Kama nilivyoeleza awali, wapo ambao wanaamini katika ukali na ukorofi, vitu ambavyo siyo tiba ya kweli.
Baadhi ya watu wanaamini wakitumia ukali sana, wanawapa wapenzi wao nafasi ya kubadilika na kueleza chanzo cha matatizo waliyonayo. Hili halina ukweli hata kidogo.
Kipengele kifuatacho, ikiwa utakipitia kwa umakini litakuwa ni dirisha lako lenye uwazi mkubwa wa kukuelekeza kwenye mafanikio na kukuacha salama kwenye uhusiano wako.
NJIA SALAMA
Pamoja na matatizo niliyoyaeleza hapo juu, wakati mwingine inawezekana kabisa mwenzi wako akawa ndiye mwenye matatizo, lakini kwa kushindwa kwako kuwasilisha vyema hisia zako, ukaharibu! Dondoo hizi zitakufaa sana katika utatuzi wa migogoro katika uhusiano wako.
(i)Zungumza kwa upole
Hii ni hatua ya kwanza kabisa katika kuelekea kuutafuta ukweli. Kwa kutumia upole, hatakuogopa na ataona wewe ndiye kimbilio lake.
Mwulize taratibu kama alikuwa na matatizo yoyote kikazi au kuna mahali ulimkwaza. Tabasamu lako linatakiwa kuwa silaha ya kwanza. Atasema tu!
(ii)Kuwa mdadisi
Kwa kutumia sauti ile ile ya upole kama nilivyoeleza katika kipengele hicho hapo juu, mdadisi! Kuwa mdadisi kwa kutumia ucheshi wa kila aina.
Kama utamdadisi taratibu, kauli yako na upole wako vitakuwa mwanga wa yeye kukueleza ukweli wa kinachomsumbua. Lazima mwisho atakueleza ukweli.
IBUKA MSHINDI
Kwa kuzingatia vijisehemu nilivyoviainisha hapo juu, lazima atasema kinachomsumbua. Kujua tatizo ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye utatuzi.
Jadili tatizo hilo, kisha endeleeni na maisha yenu kama kawaida. Fahamu kwamba, migogoro katika mapenzi ni jambo la kawaida na unachotakiwa kufanya ni kuwa na moyo wa subira na kufuata taratibu zilizopendekezwa bila kukosea hata moja.
No comments:
Post a Comment