Saturday, July 2, 2011

Unawezaje kujiepusha na upweke moyoni mwako?


Leo nitazungumzia juu ya kuweza kuushinda upweke katika moyo wako.   Natambua kuna baadhi ya wanawake au wanaume wanakaa kipindi kirefu bila ya kutamkiwa na wengine kuwa wanapedwa, kutokana na hali hiyo wanakuwa wapweke na wakati mwingine kufikiria kuwa wao ni wabaya na wasiostahili kabisa kuwa na wapenzi.

Wengine huanza kujiona hawafai kutokana na sababu ambazo kwa kiasi kikubwa huwa ni za kujikosoa mwenyewe.
Wakati mwingine huanza kufikiria kuwa huenda kwa sababu wapo katika hali fulani ndiyo maana hawapati mtu wa kuwapenda na fikra nyingine mbaya juu yao ambazo huwa ni za kujikatisha tamaa.

Tambua kitu kimoja, kuna wasichana warembo na wavulana watanashati wengi ambao hawajapata pumziko la kweli katika mioyo yao kwa muda mrefu sasa, wamekuwa wakitafuta watu wenye mapenzi ya kweli bila ya mafanikio na sasa wamekata tamaa na badala yake wamegeuka vyombo vya starehe.

Wavulana watanashati au wasichana warembo mara nyingi watu wa upande wa pili huwatamani zaidi kuliko kuwa na mapenzi ya kweli,kwa maana hiyo baada ya kushiriki nao ngono mara kadhaa huamua kuachana nao na kuwaacha wahusika wakiwa na sononeko katika mioyo yao.

Watu wa aina hii huachwa na dhiki ya moyo na wakati mwingine hukata tamaa na kuamua kutokuwa na uhusiano mwingine kabisa na wapenzi wapya. Jaribu kufikiria kama kuna mtu wa aina hii ambaye amekuwa akitoneshwa mara kadhaa na wapenzi na wewe ambaye una miezi karibu sita sasa hujapata akupendaye nani mwenye matatizo zaidi? Nadhani jibu yakinifu utakuwa nalo.

Inawezekana wewe ni mmoja kati ya hao ambao wana sononeko la moyo kwa kutopata faraja ya kweli kwa wapenzi wao. Hakika hizi ni mada mbili tofauti lakini leo nitaanza na hili la kutopata mpenzi kwa muda mrefu na sasa umekata tamaa ya kupendwa, kuoa au kuolewa katika siku zote za maisha yako.

Wakati mwingine inawezekana hujafahamu chanzo cha wewe kutopata mpenzi, lakini kuna mambo mengi ya kuzingatia ili uweze kupata mpenzi na hivyo kuepuka upweke katika moyo wako.

UNAJIJALI?
Inawezekana ukawa na maswali lukuki kutokana na ninavyouliza, unajijali? Nataka utambue kitu kimoja, kuwa kuna baadhi ya watu hawajipendi! Hivi unadhani kama wewe  hujipendi, hujithamini nani atakupenda?

Ninaposema ujipende namaanisha ujipe upendo ule wa kawaida wewe mwenyewe kabla ya kuhitaji upendo wa mtu mwingine. Mwingine inawezekana hajitunzi, anavaa nguo chafu, hapigi pasi, nywele zipo timtim nani atakupenda kwa misingi hiyo?

Hakuna anayependa kuwa na mtu ambaye hana desturi ya usafi kwanza hata kama ni mzuri kisi gani unapokuwa upo ‘rafu’ sana hakuna mtu ambaye atausumbua moyo wake kuanza eti kukufikiria wewe usiyejipenda.

Siyo lazima wakati wote uwe ‘smart’, kwa kuwa inawezekana wengine wanafanya kazi ngumu ambazo mazingira yake lazima anakuwa mchafu, lakini baada ya kazi unapaswa kuwa msafi mbele za watu.

Upande wa wasichana siyo lazima uweke nywele zako dawa au usuke rasta wakati vitu hivyo huna uwezo navyo, unaweza ukasuka nywele zako vizuri au wakati mwingine ukanyoa mtindo mzuri unaokubalika ambao hautakuweka katika mtazamo mbaya kwa jamii.

Anza kujipenda kabla ya kuhitaji upendo kutoka kwa mtu mwingine, hiyo itakusaidia kuwa na mvuto na mwonekano mzuri kiasi cha kuweza kumpagawisha mtu mwingine kuanza kuhisi cheche za moto wa mapenzi katika moyo wake.

UNAJIAMINI?                                          
Hili ni tatizo lingine ambalo kwa kweli ni la kisaikolojia zaidi kwa sababu kuna baadhi ya watu wanakosa kujiamini. Kuna mwingine anaweza akakaa kwenye kioo kwa saa kadhaa na kuanza kujitoa kasoro katika mwili wake.

Hujiona mbaya asiyevutia na ambaye hana thamani kabisa katika ulimwengu wa mapenzi, hujiona hawezi kupata mpenzi katika maisha yake yote baada ya kujitoa kasoro hizo. Mwingine hujiona kuwa ana matiti makubwa, mfupi sana, mrefu sana ana matege, ana makengeza na kasoro nyingine zozote ambazo huhisi ni kosa kuwa nazo.

Nani amekuambia kuwa una kasoro? Mshukuru Mungu kwa kukuumba jinsi ulivyo amini kuwa Mungu ana makusudi yake kukuumba kama ulivyo. Kuna watu wengine wanaweza kukupenda kutokana na hizo kasoro unazoziona katika mwili wako!

Kujitoa kasoro na kutojiamini ni kosa kwa kuwa unakuwa unajiathiri kisaikolojia na kujiona hufai kupendwa mwisho wa yote unakuja kumparamia mtu yeyote kwa nia ya kujiondolea mkosi na akishakutumia anakuacha solemba unabaki na machungu moyoni na kujiongezea matatizo zaidi.

Naamini baada ya kujipenda wewe na kujiamini kuwa unavutia, utakuwa katika hali ya kawaida kisaikolojia na wakati mwingine anaweza akajitokeza akupendaye na kukuomba hifadhi ya moyo wake kwako.

Sababu ya kukaa muda mrefu bila mpenzi au kutamkiwa kuwa unapendwa isiwe chanzo cha kupata maumivu mapya ya moyo. Acha papara, tulia, pata wasaa wa kumchunguza huyo anayedai anakupenda kwa muda wa kutosha kwa kuwa inawezekana naye akawa ni mmoja kati ya wale wanaotaka kukufanya chombo cha starehe!

Kwa dada zangu, baada ya mwanaume kukuomba uwe naye pamoja unatakiwa kumchunguza kwanza na usiruhusu aujue mwili wako kabla ya kuelewa nia yake hasa kwako ni ipi, starehe ya muda mfupi au anakuhitaji kimaisha.

Usifanye mambo kwa papara, unahitaji utulivu wa kutosha ili uweze kumpata yule ambaye ni muhimu kwa ajili yako. Ukijiamini na kuwa makini ni wazi kuwa utampata yule anayekupenda kwa dhati. Bila shaka tumeelewa.

No comments: