KARIBU kwa mara nyingine kwenye kona yetu inayozungumzia mapenzi, mada za hapa mara nyingi zinatokana na maoni yenu mnayonitumia, nashukuru kwa hilo.
Ili kuonyesha kona hii inavyowathamini wasomaji wake, mada ambayo ninakuletea kwa kiasi kikubwa ilikula akili yangu baada ya kuiona kutoka kwenu.
Baada ya kupata maswali ya watu mengi yanayoshabihiana, mmoja aliniuliza kujua ni kiasi gani mwenza wake anampenda.
Swali lake lilitokana na kuona kuwa mpenzi wake anajijali mwenyewe zaidi na kutaka matakwa yake yatimizwe bila kujali yale ya laazizi wake.
Pia mpenzi wake huyo amekuwa akiomba fedha na kupewa lakini kila wakipanga wakutane siku hiyo simu anazima, inapotokea wanakutana tena anaomba fedha, asipopewa anakuwa mkali na kutishia kuvunja uhusiano wao.
Swali linakuja, mbona hamuelewi mpenzi wake kwa kujijali yeye na kutoonyesha mapenzi zaidi ya kula vitu alivyonavyo? Tabia zake zimemshinda anaomba ushauri kwani licha ya yote hayo bado anampenda sana.
Nina imani msomaji swali limeelezeka na kinachosubiriwa kwa hamu ni jibu na ufafanuzi wa uhusiano huo. Kwa upeo wangu katika ulimwengu huu wa mahaba ningependa nilijibu swali lake kama ifuatavyo:
Nitafurahi kama msomaji ukiendelea kuwa mfuatiliaji mzuri wa kona hii kwani kuna mengi ya kujifunza na mara kadhaa imetokea maswali kujirudia.
Ukiwa mfuatiliaji utaelewa maana ya penzi la kweli na lile lililopo kwa ajili ya manufaa ya kitu fulani, pia haitokuwa vigumu kwako kutambua penzi limesimama upande upi.
Nataka nieleze kitu kimoja ambacho nimekigundua si kwa wanaume tu bali hata kwa dada zetu. Unapolazimisha penzi wakati ukijua hakuna mapenzi, unakuwa unajitengenezea hali ya hatari katika maisha yako.
Kwa mfano mpenzi wako anakujali kwa ngono tu na anapokosa, mapenzi hupungua hata ukiwa unaumwa. Wakati mwingine inatokea mpenzi wako anakupenda ukiwa na kitu lakini ukiwa huna, mapenzi yanakosekana.
Pia mpenzi wako anakuwa si mkweli, unamkamata na wapenzi zaidi ya watano, lakini anakuwa mkali eti unamfuatilia maisha yake au unakuwa na mpenzi ambaye kila kukicha hutenda makosa na kukuomba msamaha, unamsamehe hata kama kosa lenyewe ni la makusudi eti kwa kuwa unampenda.
Nauliza ni nani aliyepanda mbegu kwenye jiwe likaota? Ninachotaka kukwambia ni kuwa mbolea ya mapenzi ni upendo wa dhati. Kinyume na hapo, hakuna mapenzi zaidi ya wewe kulazimisha wakati ukijua pale hakuna mapenzi.
Unapolazimisha mapenzi kwa kuvumilia vitendo vya udhalilishaji vilivyokosa upendo, utakuwa unajiingiza kwenye mateso ya kujitakia, pia kuonyesha jinsi gani usivyojiamini na kuona huyo asiyekupenda ulimpata kwa bahati.
Ni kosa kubwa kulazimisha mapenzi hata kama umempenda kiasi gani na kuyaonyesha mapenzi kwake kwa kiasi kikubwa, lakini kama haonyeshi kuyajali mapenzi yako, hakufai.
Umeona hakuna mapenzi bado unataka msaada eti huwezi kuachana naye kwa vile unampenda, unakuwa king’ang’anizi, kwani wapenzi wamekwisha? Au umeambiwa huyo ndiye wa mwisho na zaidi yake hakuna mwingine?
Huu ni ulimbukeni wa mapenzi kwa kutoelewa nini maana ya mapenzi ni kumpenda anayekupenda. Zaidi ya hapo unakuwa kila siku mtu wa kuumia.
Thamani ya mtu ni kubwa tofauti na tunavyofikiria, tatizo ni papara ya maisha kwa kulazimisha mambo yasiyowezekana, usiwe ruba kwenye mapenzi, utajitesa bure.
Kila kitu kina wakati, utulivu na kuchagua kwa makini, nina imani utampata mpenzi wa kweli.
No comments:
Post a Comment