Saturday, June 18, 2011

Jinsi ya kuishi na mwanamke nyakati za shida


Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wanaume ambayo yanaonesha kuwa nyakati za shida hukumbana na mitafaruku mikubwa kutoka kwa wake/wapenzi wao na taarifa kuwekwa wazi kwamba mapenzi huvunjika nyakati za shida.

“Tulikuwa tunaishi vizuri tu na mke/mpenzi wangu, lakini mambo yangu yalipoyumba alibadilika tabia, akaanza visa na kuamua kuondoka.” Ukisikiliza kauli hii na kuitafakari kwa kina unaweza kuamini kwamba wanawake ni watu wanaopenda kuishi na wanaume ‘mambo safi, jambo ambalo si sahihi kabisa.

Ukweli ni kwamba, tatizo kubwa linalochangia uhusiano kutetereka si umasikini wala utajiri, bali ni ufahamu wa mtu husika wa kimaisha ambao utamfanya mwenza wake apate furaha, matumaini na ajiamini kwenye uhusiano wake.

Hivyo basi ukiwa na fedha au shida jambo kubwa la kufanya na kuzingatia ni kumjengea mpenzi wako mambo matatu ambayo ni FURAHA, MATUMANI, IMANI. Maana yake nini? Ukiwa na fedha au utajiri lakini ukashindwa kumpa mwanamke mambo hayo matatu atakuacha na fedha zako na kwenda kwa mtu masikini atakayempatia vitu hivyo. Vivyo hivyo kwa mwanamume masikini. Njia za kufuata ili kuishi kwa usalama ni hizi:

KUWA MKWELI
Tatizo kubwa la wanaume huwa hawataki kuonekana kwa wapenzi wao kuwa ‘wamefuria’ na hivyo kujifanya kama wako safi kimaisha. Ifahamike kwamba kumficha mwanamke shida na umasikini wako kutamfanya aone kwamba unashindwa kumtimizia mahitaji yake kwa ubahili wako na hivyo kuvunjika moyo. Mwambie ukweli kwamba hali yako kimaisha si nzuri. Akishafahamu hivyo atakuvumilia.

MPE MATUMAINI
Kila mara unapokuwa na mpenzi wako hakikisha kwamba hali ya kukata tamaa kimaisha haimshambulii kiasi cha kuanza kutafuta njia za kujiokoa. Hakikisha unamtia moyo kwa kumuahidi kuwa hali hiyo itapita. “Nivumilie mpenzi wangu, tatizo langu la kukosa kazi litakwisha, wakati huo nitakufurahisha.”

JENGA IMANI
Kitu kikubwa kabisa wanachohitaji wanawake ni imani, wajiamini kuwa wako peke yao, wamuamini mwanamume, waamini kuwa watafanikiwa, waone wako salama kimaisha, imani zote hizo zikiwemo za dini ni jukumu la mwanamume kuhakikisha kwamba mpenzi wake anakuwa nazo. Ni mwiko kabisa mwanaume kulalamikia maisha magumu huku nje vimada kibao, anasa na mitoko isiyoisha.

FURAHIA MAISHA
Hakikisha kwamba unamfanya mkeo awe na furaha na maisha mnayoishi kwenye chumba kimoja, afurahi kupika dagaa, afurahiye kuvaa nguo moja, apuuze kejeli na azione shida ni kitu cha kupita tu.

Aidha, mfurahishe mkeo kwa vitu vidogo vidogo vinavyoendana na hali yenu ya kimaisha, bila kusahau furaha ya tendo la ndoa, kuwa pamoja, kusaidiana na kushirikiana kwa kila jambo.

ISHI SAWA NA HALI
Ndugu, kumbuka kwamba, maisha siku zote hayawezi ‘kukaba’ moja kwa moja kuna wakati yanalegeza. Inapotokea uchumi wa familia umeimarika kutoka kwenye kula mchicha hadi dagaa, mfanye mwenza wako aone mabadiliko hayo kwa vitendo usimwache aendelee kupika majani ya maboga wakati ipo nyongeza ya kununua nyama utamkatisha tamaa.

No comments: