Baadhi ya wanaume wanashindwa kuelewana na wanawake zao kwa sababu tu hawajawajua walivyo. Rafiki zangu, wanawake wanatofautiana, lakini si kwa kiasi kikubwa; tabia zao nyingi zinafanana.
Kikubwa ni kuwajua walivyo, basi hapo kazi inakuwa imeisha. Wengine wanaachana na wapenzi wao huku wanawapenda, baadaye wanakuja kujutia, kisa hawakuwajulia. Kwa nini mwanamke akutese? Akulize? Akusumbue kichwa hadi kipasuke? Hakuna sababu.
Sasa hapa katika All About Love, nitaanza kwa kukupa siri za ambazo huzijui kuhusu wanawake. Ukweli ni kwamba, katika uhusiano, kuna mambo ambayo wanawake huyafanya siri au huogopa kuyasema, lakini yakawa yanawaumiza kwa kiwango kikubwa na huenda baadaye yakaharibu uhusiano wenu.
Hebu twende katika hizo sindano tuweze kung’amua pumba na nafaka.
KUHUSU UAMINIFU
Katika Saikolojia ya uhusiano suala la uaminifu ndiyo nguzo ya muhimu. Mwanamke anapenda uwe mwaminifu kwake katika kiwango cha mwisho, hataki kuwa na mashaka na wewe katika kila unachokifanya. Anatamani kuwa salama hata utakapokuwa mbali naye kwa sababu za kikazi au mambo mengine.
Ili uaminifu huu ambao mwanamke anauhitaji kwako uwepo, lazima uwe na penzi la dhati kwake, uwe huna mwanamke mwingine nje. Kwa maana hiyo, wakati mwingine mpenzi wako atakuwa huru na simu yako.
Wengine wanakuwa wakali sana na simu zao. Kuna nini cha siri kimefichwa kwenye simu? Kama ni kweli unampenda na upo huru kwake, huwezi kumzuia kuishika simu yako. Kumbuka wanawake wengi ni dhaifu, huwa hawapo tayari kumpoteza mwanaume wake kwa vitu vidogo lakini ukweli ni kwamba hubaki na siri ya maumivu moyoni mwake, lakini si ajabu akawa anawaza kupata mwanaume mwingine ambaye atamponya madonda ya moyo wake.
‘KILA KITU SAWA’
Wanawake walio wengi, linapokuja suala la kukosea jambo fulani, huwa hawapendi kuwa wasemaji sana. Wakati mwingine atakuwa tayari kutumia lugha za ishara ili uelewe anachokitaka, usipong’amua ananyamza!
Anaweza kujifanya anaridhika na kila kitu, kumbe ndani ananung’unika. Mbaya zaidi, hata mnapokuwa faragha, inawezekana hukufika anapotaka, lakini hawezi kukuambia, lugha ya ishara itatumika, ukishindwa kuelewa atakuacha, lakini moyoni ana maumivu.
Pamoja na kwamba anakupenda, atalazimika kutafuta mwanaume mwingine ambaye anaweza kumpa raha! Hapo utabaki na maumivu. Fumbuka rafiki yangu, msome mwanamke wako ujue anachokitaka.
HATAKI SIRI
Mwanamke anapenda uhuru, anapenda kujisikia wazi mahali popote. Hujisikia vibaya anapokuwa hana uhuru hata wa kumshika mkono mpenzi wako wanapokuwa barabarani. Anapenda penzi la uwazi!
Maana mwingine utakuta akikutana na rafiki yake, badala ya kumtambulisha vizuri kama mpenzi wake, anaanza kupatwa na kigugumizi. Ataishia kusema ni rafiki yake sana...amemaliza! Hayo si mapenzi. Kwa nini unaficha?
Hukosa amani kabisa akifanyiwa hivi, lakini hatasema, atabaki na maumivu akiendelea kufikiria utatuzi, ambao kwa hakika huwa ni kutafuta mwanaume mwingine. Vipi hapo, si utabaki na maumivu mzee?!
UNAJALI?
Rafiki yangu, mwanamke anapenda awe pekee kwako, umsikilize, umjali na umpe kipaumbele katika kila unalolifanya. Wanawake wengi wanapenda kudekezwa, lakini hawapendi kuweka hilo wazi kwa mwanaume.
Wakati mwingine anaweza kukupa mitihani ili kupima kiwango cha penzi lako. Anaweza kukuambia anaumwa au anauguliwa na mtu wake wa karibu, lengo ni kuangalia ni jinsi gani unakuwa makini anapokuwa na matatizo. Vile utakavyochukulia tatizo lake kwa ukaribu, uchungu na kuona kama lako, ndivyo utakavyomfanya aone thamani la penzi lako kwake, ikiwa vingenevyo basi humuacha na machungu moyoni, huku akijutia kuwa na mpenzi wa aina yako.
KATAA MAUMIVU
Siku zote, unatakiwa kuwa mshindi kwa mwanamke wako. Jifunze kusoma hisia zake, kabla ya kufanya kitu, fikiria mara mbili, lakini baada ya kufanya, msome kupitia uso wake. Analifurahia au umemchukiza?
Ni vizuri kugundua hilo ili uweze kufunga hisia za kumfanya aanze kufikiria kukusaliti. Hata mnapokuwa faragha ni vizuri kuwa makini na kila unachokifanya! Chunguza kama anafurahia penzi lako na manjonjo yote unayomfanyia. Kumbuka kwamba ni vigumu sana mwanamke kukueleza moja kwa moja kwamba hujamfurahisha au kuna kitu umekikosea, hii husababishwa na hofu ya kuogopa kukufanya ujisikie vibaya.
No comments:
Post a Comment