Monday, April 11, 2011

Nani amekudanganya wewe ni mbaya, huvutii?wewe ni mzuri sana


KESI nyingi ninazokutana nazo kutoka kwa wasomaji wangu wengi wanaowasiliana nami kwa njia mbalimbali wakitaka ushauri, huwa zinahusiana zaidi na kutendwa, kuumizwa, kunyanyaswa, kuachwa, kuachana na matatizo yanayofanana na hayo katika uhusiano.

Katika mazungumzo nao, kutaka kujua kilichopo vichwani mwao, juu ya fikra zao katika kufanya maamuzi sahihi, wengi huonekana wakilalamika kwamba, kuachwa, kuachana, ugomvi na matatizo mengine yote yanatokana ‘eti’ kwa sababu siyo wazuri, hawavutii na hawawatoshelezi wenzi wao!

Matatizo kama hayo niliyoyaeleza hapo juu yamekuwa yakijirudia mara nyingi kutoka kwa wasomaji mbalimbali; naamini yanaweza kuwa matatizo ya wengi zaidi na hivyo kukutana na visa vya namna hiyo kila wakati. Hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nitumie ukurasa huu kuwasaidia watu wengi kwa wakati mmoja!

Katika mazungumzo nami kwa njia ya simu, msomaji mmoja ambaye hapa naomba kutumia jina bandia la Maimuna alisema: “Yaani kaka Shaluwa nateseka sana, kila mwanaume ninayekuwa naye, amekuwa akininyanyasa. Kitu kidogo tu, nimeachwa! Roho inaniuma sana, lakini najua sababu ya haya yote. Unajua mimi sina mvuto kama wanawake wengine, ndiyo maana naachwa.”

Fikra hizo, mimi huwa naziita tope lililoganda kwenye ubongo. Maimuna aliendelea: “Halafu kuna kitu kingine ninachoamini kinaniangusha, kumweleza mwanaume udhaifu wangu. Unajua mwanaume akishajua kwamba uliachwa na wanaume wengine walipita, naye anaona bora akutende, hili suala linaniumiza sana.

“Kama huyu ‘boyfriend’ wangu wa mwisho ndiyo ananiuma zaidi, nilikuwa namuhudumia kwa kila kitu, lakini kumbe alikuwa na mwanamke mwingine, mimi nikitoa fedha na yeye anakwenda kutoa, mwisho wake nilipogundua nikaamua kuachana naye, sikuona sababu ya kuutesa moyo wangu kwa mwanaume ambaye hajui thamani ya mapenzi. Kwa sasa naona ni bora nikae mwenyewe.”

Maelezo ya Maimuna yalikuwa marefu sana, kwa kiasi fulani alikuwa katika maumivu makali sana ya mapenzi, lakini katika kutafuta sababu ya matatizo yote hayo kutokea katika maisha yake ya kimapenzi, kuna makosa ambayo alikuwa akiyafanya; mengine kwa kujua na mengine bila kujua.

Rafiki zangu, inawezekana na wewe una fikra za aina hiyo, unaamini kwamba, huenda wewe si mzuri huna mvuto na ndiyo sababu kubwa inayokufanya ukose/uachwe/ uachane na mpenzi wako. Kama una mawazo ya aina hiyo utakuwa unakosea sana ndugu yangu.

Hapa nimekuandalia dawa ya kupona kabisa tatizo lako. Hilo ni tope limeganda katika ubongo wako ambalo kwa hakika litakusababishia maumivu katika ulimwengu wa mapenzi.  
 
WAPO WASIOVUTIA?
Bila shaka hili ni swali muafaka kabisa la kujiuliza kabla ya kusonga mbele zaidi katika mada hii. Hivi ni kweli kuna mtu ambaye hana mvuto? Mvuto ni nini hasa? Rafiki zangu, suala la mvuto au uzuri lipo katika sehemu kuu mbili zinazotegemeana.

Sehemu ya kwanza kabisa ni wewe mwenyewe, unajitazamaje? Vile unavyojitazama na unavyojichukulia, ndivyo unavyoonekana na jamii inayokuzunguka. Kama unadhani wewe ni mbaya bila shaka utapoteza kujiamini na hapo ndipo hata wanaokutazama watakuona huna mvuto. Kwa nini? Kwa sababu wewe mwenyewe unaamini huna mvuto.

Sehemu ya pili ni mpenzi wako, kwa kuwa anakupenda lazima siku zote atakuona wewe ni mzuri na una mvuto wa aina yake. Kumbuka kwamba, sehemu hizi mbili zinategemeana sana, ndiyo kusema kwamba, hata kama mpenzi wako anakupenda kwa kiwango gani, anakuona mrembo/mtanashati kwa kiwango gani, kama wewe unaamini ni mbaya basi ‘automatically’ naye atakuchukulia wa kawaida.

Kuamini kwamba huna mvuto ni tatizo kubwa, maana utasafiri nalo miaka yote ya maisha yako, hata ukikutana na nani, bado utakuwa mtu wa kujitoa makosa. Mmenipata marafiki zangu? Sasa twende tukaone katika kipengele kinachofuata.

HAKUNA MZURI KAMA WEWE
Kitu cha kwanza kabisa ambacho unatakiwa kufanya rafiki yangu mpendwa ni kuamini kwamba hakuna mzuri kama wewe. Hakuna anayevutia kama wewe...hiyo ndiyo dawa kubwa kuliko zote.

Kuna jamaa yangu mmoja aliwahi kuniambia kwamba, yeye huwa hasubiri kusifiwa, anajiamini kwamba yupo bora katika kile anachokifanya! Bila shaka anaamini sawa kabisa, kutambua, kuthamani na kuamini unachokiweza ni vizuri, maana utaendelea kuwa bora kila siku.

Hata katika mapenzi ni hivyo hivyo, lazima ujiamini kwamba hakuna mzuri kama wewe. Kuna watu huwa hawaishi kujitoa makosa, mara mimi mweusi sana, mweupe sana, nina macho makubwa/madogo, macho yangu yana rangi mbaya, sina nywele nyingi nk.

Rafiki zangu huo ni ulimbukeni, amini umeumbwa hivyo ulivyo kwa makusudi na siyo bahati mbaya. Kujiamini kutakuongezea mambo mengi sana; ukijiamini hata tembea yako itakuwa inadhihirisha kwamba unajijua kwamba wewe ni mzuri, utatembea kwa maringo na uso wako utakuwa angavu.

Sura yako kujaa tabasamu kazini kwako, kutawavutia wengi na kukufanya uwe na marafiki wengi ambao mara zote watakuwa wanakusifia kwamba UNAVUTIA SANA! Unajua kwa nini hayo yote yatatokea? Kwa sababu umeamua kujikubali kwamba una mvuto!

Bado kuna mengi ya kujifunza rafiki zangu, lakini kutokana na ufinyu wa nafasi, kwa leo naomba niweke kituo kikubwa hapa, wiki ijayo tutaingia katika sehemu ya pili, ni imani yangu itakubadilisha! USIKOSE.

No comments: