Monday, April 11, 2011

NJIA SAHIHI ZA KUACHANA NAMWENZI WAKO...

Unapotaka kupeleka ujumbe kwa mpenzi wako kuwa hayuko tena moyoni mwako, lazima tu ujitolee kupata hasara katika baadhi ya mambo. Kumbuka kuwa huhitaji tena uhusiano na mwenzako.
PUNGUZA MWITIKIO WAKE
Kuna wakati ambapo rafiki au mpenzi wako atafanya au kusema jambo na wewe utatakiwa kuonesha mwitikio. Kama umeshadhamiria kuachana naye, onesha mwitikio wa shingo upande.
Kama mhusika atabaini jinsi ulivyoitikia shingo upande, utakuwa umepeleka ujumbe maridhawa, kuwa huna tena furaha na uhusiano wenu na kwamba unahisi ni wakati muafaka wa kumaliza mambo.

Kuna mazingira ambayo hutaepuka kumwitikia mpenzi au rafiki unayetaka ‘kumpiga chini’. Kwa sababu hiyo, ndiyo maana unapaswa kumwitikia lakini katika hali ambayo inaonesha kwamba huna habari naye tena.

Unapomwitikia mpenzi wako kwa shingo upande, unamwonesha kuwa yeye siyo kipaumbele kwako, jambo ambalo litamfanya kuona kuwa yamkini ni wakati muafaka wa kupunguza moto wake kwako.

PUNGUZA UKARIBU NAYE
Kama umekuwa na mazoea ya kuwa karibu na mpenzi wako kama ilivyo kawaida, anza kujenga mazingira ya kujitenga naye mnapokuwa mbele za watu ili aweze kuhisi mabadiliko katika mwenendo wako.
Haina maana kuwa usizungumze naye, kaa naye karibu na uzungumze naye kama kawaida, lakini majibu yako yawe ya mkato.  Pia usikae karibu naye sana, maana namna hiyo utalazimika kuzungumza naye na kukaribisha lugha yake ya matendo.

Lakini kama itawezekana, jishughulishe zaidi kuzungumza na watu wengine ili kwa kiasi fulani huyo mwenzako aweze kuona kuwa hukumpa kipaumbele cha kwanza.
ONESHA WATU KWAMBA HAUPO NAYE
Bila kulazimika kumfedhehesha mwenzako, chukua hatua za kuuonesha umma unaowazunguka kuwa yeye si tena mdau muhimu katika maisha yako, mathalani kwa kutomwalika kwenye shughuli muhimu ambazo ulizoea kumwalika. 
Unapolazimika kumwalika, weka mipaka katika mazungumzo yako na yeye. Hata hivyo, haishauriwi kuwatangazia marafiki zako wengine kuwa unataka kumtenga mpenzi au rafiki yako huyo, maana namna hiyo watajiwa na fikra kuwa yamkini ana matatizo kumbe kwa hakika kama kuna mwenye matatizo basi ni wewe (au unavyopaswa kuwafanya watu waamini).
Kama unataka kuwa mstaarabu, hakikisha kuwa hakuna mtu mwingine anayeingia katika mchakato huu wa kumbwaga mpenzi au rafki yako, kwani hii ni suala lako binafsi.

USIJIBEBESHE MZIGO
Hakuna haja ya kubeba mzigo wa uhusiano ambao huna maslahi nao. Japo baadhi ya wanawake huwalalamikia wanaume ambao huwachezea kisha wakawaacha, ukweli ni kwamba hupaswi kuendelea na uhusiano ambao haukupi kile ukitakacho.
Watu wengi walishafanya hivi na kufanikiwa kumaliza vema uhusiano wao na wapenzi wao. Hakuna ubaya wowote kufanya hivi pale unapoona kuwa mwenzako anakupeleka kule ambako usingependa kwenda kwa sasa.
Iwapo utatokea mgogoro wowote au mpenzi wako akawa na malalamiko, bahati nzuri tayari unazo sababu zako ambazo umetakiwa kuziweka bayana mawazoni. 
Hapo ndipo utakapozianika mbele yake na kumweleza msimamo wako mpya. Hata hivyo, utaratibu huu wa kumaliza uhusiano unafaa zaidi kwa wapenzi ambao mahusiano yao hayajajenga mizizi au wale ambao ni marafiki wa kawaida.
Kama uhusiano wako na mwenzako umeshaota mizizi, zipo tahadhari nyingi zaidi za kuchukua, maana ulishampotezea mwenzio muda mwingi.

No comments: