Saturday, April 16, 2011

Amekutesa mara nyingi, kwanini unamng’ang’ania?

ILI uendelee kuwa bora katika uhusiano wako ni vizuri kukuza ufahamu kila siku juu ya mbinu mpya za kimapenzi. Yes, ukurasa huu ni muhimu sana kwako, kwani hukuongezea maarifa kila siku, kama ukiwa makini kufuatilia hakika utavuna mengi na kuwa mjanja katika sanaa ya mapenzi.

Leo ni sehemu ya pili ya mada hii kama inavyoonekana hapo juu, tunaangalia mateso ya mapenzi. Ni kweli mapenzi yanatesa? Jibu linaweza kuwa ndiyo na wakati huo huo linaweza kuwa hapana.

Lakini majibu haya mawili tofauti katika swali moja, yanaweza kuelezewa vizuri zaidi na mhusika ambaye amepitia kwenye hatua mojawapo.

Hata hivyo, usiombe uwe umepitia kwenye mateso, maana utasimulia huku ukilia, mapenzi ya mateso yanaumiza sana rafiki zangu.

Kama mnakumbuka wiki jana tulianza na kuona mifano ya rafiki zetu wawili, halafu tukaendelea na kuona mateso yanakuwaje katika maisha ya kimapenzi. Sasa tunaingia katika sehemu ya mwisho, ambayo bila shaka itakujenga.

ANGALIA MWANZO WENU ULIVYOKUWA
Visa vile viwili vya rafiki zetu, ambavyo tuliviona wiki jana, vinatoa mwanga katika maisha yetu ya kimapenzi. Vina mafunzo makubwa sana.

Lakini kuna wengine hukumbwa na mateso ya mapenzi siyo kwa makusudi bali mazingira ndiyo yanayosababisha.

Katika maisha yako ni vyema kuwa makini sana na ahadi za wapenzi, siku zote chunguza sana kauli za mwandani wako, tumieni muda mwingi kuchunguzana.

Matapeli wa mapenzi siku hizi ni wengi, mtu anajifanya anakupenda kumbe hakupendi wewe bali anapenda kitu fulani ulichonacho na siku kikitoweka mwisho wa mapenzi yenu unakuwa umefika.

Kwanini uweke maisha yako rehani? Kwanini ujilaani kuwa eti huna bahati ya kupata mpenzi wa kweli? Nasema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya wasichana huamua kukubali kila mwanaume kwa madai kuwa anaogopa kuacha bahati!

Akitongozwa na mwanaume mchana, jioni wanakutakana beach na usiku wapo kitandani wanafanya mapenzi.

Ukiwauliza wanadai eti wanaonyeshana mapenzi ya dhati! Mapenzi ya dhati ya aina hiyo yameainzia wapi? Kwanini ukubali kumpa mtu uhai wako kwa kukutana kwenu siku moja? Kama uliwahi kupitiwa kwa kufanya hivyo acha kabisa kuanzia leo na kamwe usijaribu kurudia tena.

Mapenzi ya kweli yapo, siku ikifika utakutana na yule maalumu kwa ajili yako na wala hutakuwa na kazi kubwa ya kugundua kuwa anakupenda au anakutamani kwasababu matendo yake yataonekana wazi kuwa anakupenda.

Unapoingia katika uhusiano wa mapenzi lazima uwe umejipanga vilivyo kwa ajili ya kukabilina na kila kitu kilichopo ndani yake. Inawezekana kabisa kuepuka mateso katika maisha yako.

ANGALIA USIWE CHANZO
Inaweza kukushangaza kidogo, lakini nakuambia rafiki yangu, wakati mwingine wewe mwenyewe unaweza kusababisha mateso katika maisha yako mwenyewe. Mateso hayo, utayasababisha kwa kufanya mambo ambayo ni kinyume na utaratibu kwa mpenzi wako.

Wapo baadhi ya watu, huamua kufanya makosa kwa makusudi wakiamini kwamba hawawezi kuachwa kwasababu wapenzi wao wanawapenda sana! Huko nakuita ni uvivu wa kufikiri.

Kamwe usiwe mvivu wa kufikiri mambo, unaweza kumfanyia visa leo, ukamtesa na kumnyanyasa, lakini ipo siku moyo wake utachoshwa na mambo yako, utachoshwa na mateso na mwishowe unaweza kuachwa kwenye mataa.

Kama upo katika uhusiano na mpenzi wako ni vyema ukaonesha mapenzi yako, uoneshe jinsi unavyompenda. Jinsi unavyojali ili penzi lenu lizidi kukua siku hadi siku.

Upo mfano wa wazi kabisa wa kijana mmoja ambaye alikuwa na mpenzi wake aliyempenda kwa miaka kumi kwenye mapenzi. Kila wakati mwanamke huyo alikuwa akimfanyia jamaa visa, kila visa vinazidi.

Leo akifanya hivi, kesho anafanya vile. Lakini kwasababu jamaa alikuwa akimpenda sana mpenzi wake alikuwa akimvumilia. Hakuthubutu kumuacha, lakini ilifika wakati akaona hana sababu ya kuendelea kubaki na maumivu, akafanya maamuzi ambayo yalimuumiza sana yule mchumba wake. Yalimuumiza kwasababu hayakuwa mazuri.

Yalikuwa maamuzi ya kumuacha. Leo hii analia na kuomba msamaha kila kukicha, lakini jamaa ameendelea kushikilia msimamo wake.

Anafanya hivyo si kwasababu hampendi, bali amechoshwa na maumivu!
Kama ni kweli unahitaji furaha katika maisha yako ya kimapenzi, badilika. Chunguza mapito yako, angalia wapi unapokosea kisha anza upya ili furaha iwe sehemu ya maisha yako.

Nashukuru kwa kunisoma na ninaamini mada hii imekubadilisha vya kutosha. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri itakayokuwa mbolea katika penzi lako.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love, mtembelee kwenye mtandao wake.

No comments: