Wednesday, May 11, 2011

Kanuni 6 za kukatisha uhusiano wa kimapenzi na mwanaume au mwanamke


Uchunguzi unaonesha kuwa, wanawake/wanaume husumbuka sana kutafuta njia za kukatisha uhusiano wao wa kimapenzi na wanaume/wanawake baada ya kugundua kuwa hawako kwenye chaguo sahihi.

Wengi wao hujikuta wanashindwa kufikia lengo hilo kwa sababu ya kutoeleweka. Dondoo za mahojiano nilizofanya na baadhi ya wanawake zinaonesha kuwa, asilimia 48 kati yao wanaishi kwenye mapenzi ya lazima au yaliyowachosha.

“Sina la kufanya, nimemwambia mara nyingi tuachane lakini hasikii, ananitisha kuwa nikimwacha atanikomesha. Anachofikiri nimepata mwanaume mwingine lakini ukweli tabia zake zimenichosha,” alisema dada (X) wakati akizungumza nami.

Kisaikolojia mapenzi ya kulazimisha nafsi yamekuwa na madhara makubwa kiafya na kiufahamu. Wengi kati ya watu waliotajwa kuua, kujiua au kujeruhi wanatoka katika kundi la maisha ya mapenzi ya lazima. 
Chukua hatua zifuatazo kama umeamua kuachana na mpenzi wako.

1. KUWA MKWELI
Wanawake/wanaume wengi wamekuwa wakificha sababu za kutaka kuachana na wapenzi wao wakihofia kuwaumiza au kujiumbua. Ukweli unamtaka mwanamke amwambie wazi mwanaume kwa nini anataka kukatisha uhusiano.  Mweleze ajue kasoro zake na uweke wazi hali ya kuchoka kumvumilia.

2. MUDA SAHIHI
Usikurupuke kuachana na mpenzi wako. Lazima uhakikishe kuwa uko kwenye wakati sahihi ambao hautakufanya ujutie uamuzi wako. Ikiwa unajua kuna gari umemuazima, pesa, mali na vitu vingine vya thamani tafuta njia za kuzuia visipotee. Ushauri wa kitaalamu kuhusu mali ni muhimu ukauzingatia kabla ya kuamua.

3. SHIRIKISHA WATU
Ukiwa umehakiki mawazo yako usimwambie mhusika mkiwa chumbani. Weka wazi azimio lako mbele ya rafiki na ndugu. Faida za kufanya hivi ni kuweka ushahidi na wakati huo huo kumharibu kisaikolojia asiweze kurudi kwako kwani wanaume wanatajwa kuwa na aibu ya kuonekana wanang’ang’aniza penzi.

4. FANYA MWENYEWE
Suala la kuachana ni binafsi, hivyo unapofikia hatua hiyo lazima uwe ni wewe uliyeamua kufanya hivyo na isiwe shinikizo kutoka kwa watu wengine kwa masilahi yao. Kama ulivyopenda ndivyo uache.

5. UMAANISHE
Kuna wanawake/wanaume ambao hutangaza kuwaacha wapenzi wao, lakini hawamaanishi sawa na uamuzi wao. Utakuta pamoja na hatua hiyo huendelea kuwatumia meseji za mapenzi, kujichekesha chekesha, kujipitisha pitisha na wakati mwingine hata kujipeleka nyumbani. Kufanya hivyo hakuwezi kuleta matokeo sahihi.

6. USIRUDI NYUMA
Uamuzi wa kuachana lazima uwe umeshiba sababu ili isijitokeze hali ya kurudi nyuma na kujuta. Mwanaume ukishamtangazia kumwacha, halafu akaona unajirudisha mwenyewe utamfanya aamini kuwa huna pa kwenda na hivyo kama alikuwa anakutesa na kukudharau ataongeza zaidi. Utakuwa umejirudisha Jehanamu mwenyewe.

No comments: