Saturday, July 2, 2011
Huwezi kulazimisha mtu kupenda asichokipenda
NAAM tumekutana tena kwenye kona ya yetu ili kujuzana machache. Yangu hali buheri wa afya, sijui ninyi wenzangu. Kama ilivyo ada tunaendelea na mada zingine ili tujue tumejikwaa wapi na wapi tuelekee.
Leo nataka kuwaelezea maadui wanaovuruga ndoa za watu, hii inatokana na swali la mmoja wa wafuatiliaji wangu wazuri wa kona hii.
Alikuwa akilalamika kutokana na mchumba wake, ambaye hata familia yake ilimtambua kumgeuka na ujauzito aliompa kupewa mtu mwingine.
Kingine kilichomshangaza kilikuwa kwa mpenzi wake kukana kuwa ujauzito ule si wake, wakati alikuwa naye kipindi chote kabla ya kwenda kwa wazazi wake mkoani kijifungua.
Swali linakuja, kwa nini mchumba wake ambaye walipanga kujenga familia amgeuke ghafla kama kinyonga baada ya kwenda kwa wazazi wake kwa ajili ya kujifungua?
Kwa jibu jepesi najua utasema kuwa mchumba wake hakuwa na mapenzi ya kweli ila alikaa naye kwa ajili ya kutatua matatizo yake au kwa sababu fulani. Kama jibu lako ni hilo, haupo mbali na mada ya leo.
Binafsi ukweli kuhusu suala hilo, niliupata kutokana na maswali niliyomuuliza kwa njia ya simu kwa zaidi ya saa moja tukiwa pamoja na mume mwenzie aliyetaka kubambikiwa mtoto.
Kupitia mazungumzo yetu hayo, nililigundua hili ambalo ndilo limekuwa gonjwa sugu katika mifarakano mingi kwenye ndoa au uhusiano. Najua unataka kujua ni nini.
Tatizo ambalo limekuwa sugu na linalochangia watu kushindwa kuelewana na kuwa na mifarakano ndani ya ndoa au uhusiano, ni wanafamilia.
Mara nyingi mwanamume au mwanamke ambaye anavunja uhusiano ghafla bila maelezo yoyote, wengi huamini ni kukosekana kwa upendo wa kweli kwa mmoja wao, lakini uchunguzi wangu wa ndani ambao nina uhakika nao kwa asilimia mia na hata wewe utaniunga mkono ni kwamba, tatizo kubwa la mifarakano ya ndoa ni hilo ambalo nimelitaja hapo juu. Najua wengine wataniona kama mpiga ramli.
Adui mkubwa wa uhusiano wa wanandoa au wapenzi ni baadhi ya wanafamilia, sichagui ni nani bali wao wanajijua. Hii hutokana na mpenzi wako kutokuwa chaguo lao, kama utakuwa na msimamo wa kukataa wazo lao la kutafuta mwingine, lazima watakutishia kukutenga.
Suluhu yao ni kuachana na mpenzi wako ili uwe na yule ambao wao wamemchagua japo si chaguo lako. Familia imekuwa sumu kubwa kwenye uhusiano mwingi kwa kuingilia matakwa kwa kutumia uwezo wao kuwatenganisha na kukulazimisha kutoa uamuzi wa mdomoni na si wa moyoni kumkataa umpendaye.
Wengi huwa tunaamini uamuzi wa mtu kuvunja penzi ghafla ni pindi anapokosa mapenzi ya kweli, lakini ukichunguza kiundani utakuta uamuzi wa mhusika kuvunja uhusiano si wake bali ni wa wanafamilia.
Kwa walio na msimamo hutengwa na familia hata wazazi hufikia kumtolea radhi. Napenda kurudia, huwezi kuusemea moyo wa mwenzako. Nafasi ya kupenda ni ya mhusika na si mtu wa pembeni au wazazi.
Hata ndugu bado hawana nafasi ya kuingilia uamuzi wa mtu, hata mkiwa mmemzidi umri. Mkiona mwenzenu amejenga ninyi mnatakiwa kuongeza uimara na si kila siku kutafuta njia za kuvunja uhusiano huo.
Kumbuka kumlazimisha mtu ampende asiyempenda ni sawa na kuingilia uhuru wa mtu wa utashi na furaha ya moyo wake. Siku zote uzito wa mzigo aujuae aliyeubeba si mtazamaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment