Monday, July 4, 2011

Mapenzi ni mateso kwa kila asiye na heshima kwa mwenzi wake.


Na Luqman Maloto
Siku zinakwenda, tunapata matoleo mapya ya watu kufeli katika mapenzi. Wengine ‘Alhamdulillah’ wanapiga simu na kukiri kupata ukombozi kutokana na yale ninayoandika. Ni maisha yetu kwa sababu wote tunaingia kwenye uhusiano, hivyo hatuna budi kuheshimu.

Jamii inakabiliwa na tatizo la kutotambua thamani ya wenzi wao. Mwanamume anaweza kudhani mke au mwenzi wake ni sawa na mtu yeyote anayekutana naye barabarani. Aina hii ya watu ndiyo  ambao mara nyingi wanajikuta wakipata sifuri kila kukicha.

Leo atalia, “mapenzi yananitesa”, siku zitapita ataangukia kwa mwingine. Asili yake haoni mbali, kwa hiyo atatangaza kuwa amepata tiba, “aah, huyu wa sasa ni safi sana. Simuachi na ndiye wangu wa maisha”, baada ya neno hilo, kaa uone matokeo.

Kabla ya wiki mbili hazijapita, usishangae akaja na kilio kingine, “jamani mimi nina mkosi, kila mtu ananitenda.” Si kweli kuwa anatendwa, ila ukosefu wake wa nidhamu kuhusu mapenzi ndiyo tatizo. Hanyenyekei pale inapohitajika, unategemea nini?

Nimewahi kueleza hili; Sanaa ya busara katika maisha inajumuisha vitu vinne: Nia na malengo, Mungu ana nafasi yake, hatua chanya na mafanikio endelevu. Ukikaribisha busara kama kanuni yako ya kuishi, maana yake unahitaji amani na furaha.

Ukitaka kuishi kwa busara ni lazima uwe na mtazamo wenye furaha. Lazima uingalie dunia kwa fikra na macho. Angalia jinsi watu wengine wanavyosononeka kwa kuikosa, halafu chukua mfano wa wanaoishi kwa amani na furaha.

Unapoitazama dunia kwa fikra, hapo unapaswa kubeba ufahamu wa uchafu mgumu uliopo. Fikra zinakuja kutokana na kumbukumbu ambazo hutafsiri uzoefu wa nyuma ambao utakupa mwanga wa hali ya sasa. Hatua hizo zinatakiwa kutoa muongozo katika kuandaa furaha.

Je, umewahi kumtazama mwenzi wako kwa mtazamo chanya? Upungufu wake unauchukuliaje? Kasoro zake unazipokea kama changamoto ili umrekebishe mkae kwa amani? Ukiona vyaelea ujue vimeundwa. Usitarajie kupata malaika ambaye atakidhi kila unachohitaji.

Vingine inakubidi uvifanyie kazi. Utumie namna ya upole kumfanya aelewe kile ambacho unakihitaji kutoka kwake. Kama ni mgumu kufuata muongozo, tambua kwamba hiyo ni kasoro yake. Nenda naye taratibu. Si kuwa na jazba na kujilundikia msongo wa mawazo.

Napenda sana kutumia nukuu ya Mwandishi wa saikolojia, Swami Sukhabodhanda ambaye katika makala yake yenye kichwa  kisemacho “Love and Happiness: Art of Wise Living Brings Great Joy” ameandika:
“Mtu sahihi ni yule anayejifunza kupunguza msongo wa mawazo, anayejifunza kuongeza furaha na kupanua uwezo wake.”

Hii ina maana kuwa kutafuta furaha ni wajibu wako, lakini swali la kujiuliza ni hili, mwenzi wako akiwa hana amani wewe utaipata wapi furaha? Akiwa amekasirika utaweza kucheka? Jibu ni kwamba haiwezekani na endapo moyo wako una amani wakati mwenzako umejikunja, ni wazi kwamba penzi lenu limejaa mashaka.

Heshima ambayo naizungumzia, kitovu chake ni furaha ya kila mmoja. Kama mwenzako hana amani lakini kwako imejaa tele na hali hiyo haikukereketi, maana yake ni kwamba humheshimu mwenzi wako. Matokeo yake ni kuwahi kuchokana. Utasema una mkosi, kumbe unajitakia.

Hivyo basi, naungana na Swami kushauri kwamba ni lazima kila mtu ajifunze kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza furaha. Ukifanikiwa kuiweka chanya furaha ya mwenzi wako na yako itapatikana. Zingatia msemo kuwa ninyi ni kitu kimoja wewe ni yeye!
Watu wengi wamekuwa wakishindwa kustawisha uhusiano wao kwa sababu wanashindwa kuishi ndani ya wenzao. Wanatenda mambo ambayo yanawaumiza wenzi wao bila kujiuliza. Hawana malengo chanya!

Mtu mwenye malengo mazuri katika mapenzi ni yule anayejiuliza kabla ya kuzungumza au kutenda. Anatafakari kauli au kitendo na matokeo yake. Pointi kuu ni mapokeo ya mwenzi wake. Ni kosa kufanya tukio lolote au kutoa matamshi yanayoweza kumuudhi mwenzako.
Ni lazima uwe na angalizo ambalo kwako linaweza kuwa dogo lakini kwa mwenzako lakiwa kubwa.

Itaendelea wiki ijayo.

No comments: