Saturday, April 28, 2012

Uliyemkusudia hukumpata, mvumilie uliye naye


NAAM, kama ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu ili kuendelea kukumbushana na kufundishana mambo machache yahusuyo maisha yetu ya kila siku.

Nina imani kila mtu ana hamu kujua kile nilichowaandalia. Leo tuzungumzie maisha ya mapenzi.
Mtakubaliana nami kuwa, siyo wote wamepata kile walichokikusudia, nikiwa na maana kuwa, kila mtu huwa na matamanio yake apate mpenzi wa aina gani ambaye ndiye chaguo la moyo wake.

Wengi wameangukia kweli mapenzi waliyoyaota katika maisha yao, kutokana na kupima kwa macho au pupa ya penzi. Ili kumpata mpenzi aliye bora, kuna vitu ambavyo kila mmoja huvihitaji kwa mwenzake. Zaidi ya sura na umbile zuri ambavyo huonekana, kikubwa ni tabia ambayo haionekani kwa macho.

Lakini wengi tumejikuta tukipata kimoja kati ya hivyo, umbile la nje lenye siri kubwa ndani. Wapo waliopata wapenzi ambao huamini ndiyo chaguo la mioyo yao lakini hujikuta wakijutia uchaguzi wao.

Ni ukweli ulio wazi kwamba, kila mtu huangalia sana mtu alivyo, kama sura umbile na umaridadi wake.
Mtakubaliana nami kila mmoja huvutiwa na mwenzake kwa kumuangalia na kuvutwa kama sumaku.

Hata mnapoanza uhusiano kila mmoja huwa na matumaini ya kupata penzi la kweli. Kupata mpenzi mzuri mwenye tabia nzuri ni bahati nasibu kwa vile pale ni sawa na kufunua karata yako ambayo tayari umeishailamba.

Hapo kuna mambo mawili ule au uliwe. Ukila utakuwa umepata kile ulichokikusudia kumpata yule uliyemkusudia, lakini ukiliwa ujue karata uliyofunua siyo.

Hapa ndipo watu huanza kujiuliza; mbona mpenzi wangu au mwenzangu simuelewi? Nilivyomfikiria na nilivyomuona sivyo alivyo.

Ni kwa nini?
Ni vigumu kuijua tabia ya mtu mara moja, wapo wenye tabia mbaya ya asili ambayo hujitahidi kuishi kutokana na mafundisho aliyoyapata ya uhusiano.

Kwa vile aliishi kwa kufuata maelekezo na si asili yake lazima atarudia uhalisia wake na kukufanya ujiulize; ni kweli huyu ndiye yule niliyemuona na kutamani awe mpenzi wangu?

Kibaya zaidi tayari umeishajitia kitanzi hivyo huna jinsi ni kuvumilia huku ukitafuta msaada nje ya uhusiano ambao si tiba kamili kama kumeza dawa za kupunguza maumivu wakati baadaye tatizo hujirudia kwa vile ugonjwa bado unaendelea kuwepo.

Siyo wote ambayo matatizo yao huwa hayapati ufumbuzi. Kuna wengine ambao kwa kumcha Mungu, huongozwa na muongozo wa maisha wa kuujua umuhimu wa uhusiano na kujirudi.

Wapo ambao huolewa au kuoa watu wasiowajua vizuri, lakini nyumba zao hujaa upendo kuliko zile ambazo zilitumia muda mwingi kuchunguzana tabia.

Hapo lazima ukubali ndoa au kumpata mpenzi wa kweli ni bahati nasibu hakuna mwenye uhakika wa 100%. Napenda kuwauliza kitu kimoja: Je, ni kweli wazee wetu walikuwa na ujuzi wa kumjua mpenzi wa kweli?

Jibu; si kweli, bali mafunzo ya wazazi kabla ya ndoa na nidhamu ya mwanamke ndiyo iliyolinda ndoa nyingi hata kama uliyemuoa au kuolewa naye humpendi kwa vile wazazi wamempenda basi utaishi naye.

Siri kubwa ilikuwa wazazi kuzisimamia ndoa za watoto wao, kuhakikisha zinadumu, zinakuwa na uvumilivu na usiri ambao ndiyo njia pekee ya kuokoa ndoa. Lakini za sasa hivi ambazo nyingi zinakwenda na wakati, miaka 10, wapenzi 20, watoto 10 na kila mtoto ana mzazi wake.

Hata kama hukumpata yule uliyemkusudia, kwa vile ameishakuwa wako, jengeni tabia ya kutatua matatizo yenu wenyewe hata yale ya ndani yawe siri yenu.

Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

No comments: