Pokea maneno yangu na uyasome kwa mtindo wa katikati ya mstari, mwisho utajua nini ambacho kinamaanishwa. Siwezi kushadadia utengano kwa maana najua athari na machungu yake.
Upo uhusiano ambao umelengwa kudumu, hasa kwa wanandoa. Kuna wengine hawana sura ya kudumu, wapo kwa muda kwa kuzingatia mazingira pamoja na kile kilichomo ndani ya nafsi zao.
Unaweza kujiuliza; Kwa nini ufike wakati utake kuvunja uhusiano wako na mwenzako? Iwe wa kirafiki au kimapenzi, Ipo wazi kwamba kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuwafanya wahusika kuamua.
Yawezekana uhusiano wako na mpenzi au rafiki yako wa jinsia tofauti unakutia hasara, au unakuharibia biashara, au unakupunguzia heshima katika jamii, au pengine uaminifu wako kazini.
Mathalan, mpenzi wako anafahamika kuwa ni kahaba. Inawezekana uhusiano wako na mwenzako unaidhuru nafsi yako. Mfano, mwenzio ana nguvu sana juu yako kiasi kwamba huwezi kusema “hapana” kwa lolote analokwambia.
Pengine kutokana na hali hiyo umekuwa ukilazimika kufanya mambo ambayo huyapendi na ambayo hayaendani na maadili.
Lakini pia yawezekana umeanza kumchukia mwenzako. Mazingira yamebadilika, kwa hiyo wewe na yeye hampatani tena. Unajitazama na kugundua kwamba ulivyo huendani naye. Ni matokeo ya kuchokana!
Uhusiano wowote unapoyumba, uwe wa kirafiki au kimapenzi, huwaweka wahusika katika wakati mgumu kiasi kwamba ni lazima mmoja achukue hatua ili aweze kuishi kwa amani na furaha ya kweli.
Hata hivyo, ikae akilini kwamba inauma mno kuachana na mtu unayempenda!
Kumaliza uhusiano wa kimapenzi au kirafiki si hatari, lakini la msingi ni kuhakikisha kuwa unamwacha mwenzako akiwa hajaathirika kisaikolojia kwa namna yoyote.
Kwa sababu hiyo unapaswa kujifunza njia sahihi za kumaliza uhusiano wako na mwenzako inapobidi.
Kuna jamii inaweza kuthubutu kusema, unapochoshwa na mtu, mchukue uende naye mahali kisha umueleze kwa uwazi kuwa hutaki tena kujihusisha naye kwa sababu moja, mbili, tatu.
Hata hivyo, hilo si jambo rahisi kwa wengi. Badala ya kukabiliana na mtu ana kwa ana na kumweleza kuwa humhitaji tena, zipo njia za kirafiki ambazo unaweza kuzitumia bila kusababisha matatizo yoyote ya kisaikolojia.
ANDAA SABABU ZAKO!
Unapotaka kumbwaga rafiki yako au mpenzi wako ambaye hujampa ahadi yoyote ya kuishi naye katika ndoa, anza mchakato kwa kuweka bayana sababu zinazokufanya utake kuachana naye.
Hakikisha kuwa sababu unazoziweka ni zile ambazo mpenzi wako huyo hatapata namna ya kuzipinga.
Zitengeneze sababu hizo kwa kuzingatia mtazamo wako mwenyewe, na si wa kwake ili hatimaye kusiwe na mwanya kwamba atajirekebisha na mtaendelea kuwa pamoja.
Namna hii utakuwa unayaangalia zaidi maslahi yako mwenyewe na iwapo utalazimika kumweleza mwenzako ni kwa nini unataka kumaliza uhusiano wako na yeye, sababu zako hazitaonekana kama shambulio kwake wala tabia yake.
USITHUBUTU KUWASILIANA NAYE!
Utakapokuwa umeweka wazi sababu zako na kuziamini, weka mkakati kuwa hutaanzisha tena mawasiliano na mwenzako.
Jiwekee msimamo kuwa hutampigia simu, wala kumtumia ujumbe wa simu, wala barua pepe na kadhalika, ila utajibu tu yeye atakapoanzisha.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment