Friday, August 30, 2013

Wivu chandandu ya mapenzi, lakini ikizidi huwa karaha

WOTE tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutufikisha siku hii. Naungana na familia za wote waliopatwa na janga la ajali ya kuzama kwa meli wiki iliyopita. Mungu awape moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu, pia waliotangulia mbele ya haki mwenyezi Mungu awape mapokezi mema.
Kama kawaida tunaendelea mada nyingine jinsi unavyoweza kuudhibiti wivu wako. Hakuna asiyejua wivu ni nini hasa katika suala ya uhusiano. Kila kiumbe chenye akili timamu lazima kiwe katika hali hiyo.
Wivu wa mapenzi unamaanisha nini?
Wivu katika mapenzi unamaanisha mtu kumiliki mpenzi wake peke yake pasipo kuingiliwa na mwingine, kwa maana nyingine kuonyesha unampenda na kumjali ila ukizidi unakuwa sumu.
Kiumbe kisicho na wivu ni sawa na mwili bila roho ambacho lazima kitakuwa ni mfu.

Lakini kwa kiumbe kinachovuta pumzi lazima kiwe katika hali hiyo na kama huna huku bado unavuta pumzi basi hujui nini maana ya kupenda. Lakini kwa yeyote anayeijua thamani ya kupenda lazima atakuwa anajua maana ya wivu.

Wivu katika mapenzi ndiyo chachandu kwa mtu kujua kweli anapendwa. Huwezi kuwa na mke au mume akichelewa au kusimama mazingira yasiyo eleweka ukae kimya, ujue lazima kuna walakini akilini mwako.

Lakini leo nataka kuzungumzia wivu uliovuka mipaka ambao huwa kero kwa wengine. Wapo wanaume au wanawake huwaonea wivu hata dada au kaka yako.

Katika suala hili napenda kulieleza kwa mapana kwa ajili ya kwenda pamoja ili tuweze kupunguza wivu ambao umekuwa kero kwa watu hata kufikia kuvunja uhusiano. Jambo hili niliwahi kulizungumza awali kuwa hakuna kiumbe anayewaza ngono kila, wakati ukiona hivyo ujue ana matatizo.

Pia nilielezea kusomana tabia kabla ya kuanza uhusiano na siyo kukutana kimwili ndiyo msomane, kama wengi wasemavyo.
Kusomana tabia ni pamoja na kujua historia ya nyuma ya mwenza wako, ukizijua tabia zake naamini ukimwonyesha njia utatumia muda kuyarekebisha matatizo yake huku ukimweleza sababu ambazo huenda zitasababisha msiwe pamoja.

Mkirekebisha tatizo hilo ni wakati wenu kuanzisha mapenzi mkiwa mnajuana, kila mmoja anaujua udhaifu wa mwenzie ambao unarekebishika.
Usimpende mtu kwa ajili ya sura au umbile, lakini ikiwa tabia yake ni mbovu huwezi kuibadili kama ilikushinda mkiwa na uhusiano wa juu juu.

Unajikuta unakuwa na wivu wa kijinga hata ukimkuta mpenzi wako amekwenda sokoni dukani au kwenye maji wewe unajua amekwenda kwenye ngono.
Unaweza kuuthibiti wivu wako wa kijinga kwa kuitengeneza tabia ya mwenzi wako ambayo utaijua vizuri kitu kitakacho kufanya umjue vizuri mwenzako na kuweza kumuamini.
Narudia tena hakuna binadamu anayewaza ngono kila wakati, peaneni uhuru ili kujengeana uaminifu.

Pia hata unayetumia mwanya kwa ajili ya kufanya uchafu wako. Jifahamu kuwa wewe si mnyama ni mwanadamu unayetakiwa kujiheshimu, mwili wako anayetakiwa kuujua ni mwenza wako tu.
Uhuru unaopewa usiutumie vibaya na kusababisha kuwaingiza mwenzako kwenye kapu la samaki waliooza na kuwafanya wote waonekane wameoza. Kama bado unataka kufanya uchafu wako usikubali kuingia kwenye uhusiano wa kujenga familia.

No comments: