Sunday, April 15, 2012

Diamond ang’ata tuzo za muziki za Kilimanjaro…ashindwa kuvunja rekodi ya 20%




Khadija Kopa, ambaye hii ni mara yake ya kwanza kunyakua tuzo za KTMAHatimaye baada ya tambo za hapa na pale, pamoja na shauku kubwa toka kwa mashabiki wa burudani ya muziki nchini, Watanzania leo hii wameweza kuwajua vinara wa muziki nchini baada ya washindi wa tuzo mbalimbali kutangazwa katika shoa kali iliyofanyika jijini Dar es salaam, maeneo ya Mlimani City.Tuzo hizo ambazo hudhaminiwa na kampuni ya bia ya Kilimanjaro, zimeshuhudia msanii mkongwe bi Khadija Kopa, akinyakua tuzo yake ya kwanza baada ya kushiriki kwenye kinyang’anyiro hicho miaka kadhaa huku akiambulia patupu.
Msanii anayewika kwa sasa Diamond, aliweza kung’ara kama ilivyotarajiwa baada ya kunyakua tuzo tatu, japo alishindwa kuvunja rekodi ya kunyakua tuzo nyingi kwa pamoja, kama ilivyowekwa na msanii 20% msimu uliopita. Mshindi huyo wa mwaka jana, naye yalimtokea yaliyomtokea Diamond mwaka jana, baada ya kuambulia patupu katika tuzo zote.
Tuzo ambazo zilitolewa katika shindano la msimu huu, washindi na waliokuwa washindani ni kama ifuatavyo:-
Tuzo ya muziki wa Reggae – Arusha Gold:
Tuzo ya kwanza kutolewa katika usiku huu, ambayo ilikwenda kwa Arusha Gold, kupitia wimbo wao wa Arusha Gold, baada ya kuwabwaga wakali wengine waliokuwa wakiiwania akiwemo mshindi wa tuzo tano wa mwaka jana 20%, Manfred ft Fire na Nakaaya.
Tuzo ya wimbo bora wa Ragga – Maneno Maneno
Ilitwaliwa na mwanadada Queen darling kupitia wimbo wa Maneno Maneno, baada ya kuwabwaga washindani wengine wane, ambao ni pamoja na mkali AY, kupitia wimbo wake wa Good Look, aliomshirikisha mwanadada Miss Trinity. Wengine walioshindwa walikuwa ni Manfred na Double.
Tuzo ya wimbo wenye mahadhi ya Zouk Rhumba – Dushelele
Ally Kiba, aliitwaa tuzo hii baada ya kuwapiga kumbo Barnaba, Dyina, Lady JD na Rachel.
Tuzo ya wimbo bora wenye vionjo vya asili – Vifutundu
Vifutundu, ni wimbo ambao umekuwa masikioni mwa watu ukitamba sana hivi sasa, na ukamuwezesha AT kuitwaa tuzo hii, akiwabwaga Offside Trick kupitia wimbo wao wa Kidudu Mtu, Ashimba kupitia wimbo wa Mwanadamu, na Young D katika wimbo aliomshirikisha Kitokololo.
Tuzo ya wimbo bora wa taarab – Nani kama mama
Bilashaka jina la wimbo lilitosha kumbeba, lakini pia nani anabisha kuwa Isha Mashauzi amekuwa juu sana msimu huu? Aliinyakua tuzo hii baada ya kura zake kuwa nyingi zaidi ya wakali wengine katika miondoko hiyo akiwemo mkongwe Khadija Kopa kupitia wimbo wa Full Stop, Jahazi na nyimbo wa Hakuna Mkamilifu na Nilijua Mtasema
Tuzo ya wimbo bora wa Kiswahili kwa upande wa bendi – Dunia Daraja
African Stars, ilikuwa bendi ya kwanza kutajwa katika bendi zilizokuwa zikiwania tuzo hii na ikaishia kuwa ya kwanza pia kutangazwa kwa walioshinda tuzo yenyewe kupitia wimbo wao wa Dunia daraja. Hii ilikuwa baada ya kuwabwaga Mapacha watatu na wimbo wao Usia wa babu, na Mashujaa kwa wimbo wao wa Hukumu ya mnafiki.
Tuzo ya wimbo bora wa Afro Pop – Hakunaga
Kuna ambaye ana swali juu ya tuzo hii kumshukia Suma Lee? Bila shaka Hakunaga, maana hakunaga ambaye hakubambwa na wimbo huu. Mkali huyo ambaye alipotea katika anga za muziki kabla ya kurejeshwa kwa kasi na Hakunaga, aliwashinda Diamond aliyekuwa anaiwania kupitia Moyo wangu na Mawazo, Tunda Man na wimbo wa Starehe, pamoja na Ommy Dimples aliyeingiza Nai Nai ambayo imemshirikisha Ally Kiba
Tuzo ya wimbo bora wa RnB – My number 1 fan
Ben Paul, akiwa kaingiza nyimbo mbili katika tuzo hii, alifanikiwa kuitwaa kupitia wimbo wa my number one fan, huku akiwashinda Belle 9 na Nilipe Nisepe, Hemed na Usiniache, pamoja na msanii Jux.

Roma Mkatoliki, aliyepeleka tuzo za Hip Hop jijini Tanga
Tuzo ya wimbo bora wa Hip Hop – Mathematics
Ufalme wa A Town unaanza kuvunjwa au unazidi kusambaza makali yake katika ukanda wa Kaskazini? Moja wapo hapo bilashaka linaweza kuwa na ukweli ndani yake, baada ya msanii toka Tanga, Roma, kuinyakua tuzo hii kupitia wimbo wa Mathematics. Roma, aliwabwaga mpinzani wake mkuu Izzo B (Rizzy One), Jay Mo ft P. Funk kupitia wimbo wa Famous, Godzilla ft Chally kupitia wimbo wa King zilla, na Joe Makini akishirikiana na Lady JD.
Tuzo ya msanii bora anayechipukia – Ommy Dimples
Usiku mzuri kwa chipukizi Ommy Dimpo, ulianzia hapa, baada ya wimbo wake kumuwezesha kutwaa tuzo ya msanii chipukizi, kupitia wimbo wake wa Nai Nai, aliomshirikisha Ally Kiba, ambapo aliwabwaga Darasa na wimbo wa Darasa, Rachel kupitia wimbo wa Kizunguzungu, Abdul Kiba na wimbo wa Sio demu na Beatrice kwa wimbo wa Nabisha
Tuzo ya repa bora wa mwaka kwa upande wa bendi – Kitokololo
Aliinyakua tuzo hii baada ya kuwashinda wapinzani wake ambao walikuwa ni Khalid Chokoraa, Ferguson, Msafiri Diouf na Totoo ze Bingwa.
Tuzo ya Msanii bora wa Hip Hop – Roma.
Roma, alinyakua tuzo yake ya pili baada ya ile ya awali ya wimbo bora wa mwaka aliyoichukua kupitia wimbo wa Mathematics, wimbo ambao pia ulimuibua kidedea katika kinyang’anyiro cha msanii bora wa Hip Hop. Aliwashinda Godzilla na wimbo wake wa King Zilla, Izzo B, Joe Makini na Fid Q.
Tuzo ya wimbo bora wa kushirikiana – Nai Nai.
Ommy Dimples naye akanyakua tuzo yake ya pili baada ya wimbo wake wa Nai nai kuzishinda nyimbo za Famous wa Jay Mo na P. Funk, Godzilla na Marco challi kwa wimbo wa King Zilla, Lady jay Dee na Mr. Blue walioshiriki kupitia wimbo wa Wangu. Pamoja na Chege, Temba na Feruzi walioingiza wimbo wa Gangsta au Sharoballo
Tuzo ya wimbo bora wa Afrika Mashariki – Kigeugeu
Hakukuwa na wasanii toka nchi za jirani, lakini kazi zao zilishirikishwa na tuzo ya wimbo bora wa ukanda wa Afrika Mashariki ambao uliwabamba Watanzania, ikanyakuliwa na msanii Jaguar kupitia wimbo wa Kigeugeu.
Tuzo ya Mtumbuizaji bora wa kike wa mwaka – Khadija Kopa.
“Nimekuwa nikishiriki tuzo hizi kwa muda mrefu sana lakini sijawahi kushinda tuzo hii, hivyo nawashukuru kwa safari hii kunipatia ushindi huu” Hiki ndicho alichotamka bi. Khadija Kopa, pindi alipotangazwa mshindi wa tuzo hii, baada ya kuwashinda Isha Mashauzi, Queen Darling, Dyina na Shaa.
Tuzo ya Mtumbuizaji bora wa kiume wa mwaka – Diamond.
Kijua kikiwa kinaelekea kuonekana kinazama, huku wengi wakianza kudhania kuwa nuksi ya mwaka jana inaelekea kumnyemelea mkali huyu, hatimaye akatajwa kama mtumbuizaji bora wa mwaka kwa upande wa wasanii wanaume, baada ya kuwabwaga Ally Kiba, Bob Junior, H baba na mkali wa taarab, Mzee Yusup.
Tuzo ya Mtunzi bora wa mwaka – Diamond.
Na nyota ikazidi kumng’aria baada ya kufululiza tuzo ya pili ya utunzi bora wa mwaka kupitia wimbo wake wa Mawazo, huku akiwabwaga Ally Kiba na dushelele, Mzee Yusuph na Juma dede, Barnaba na Milele daima, pamoja na Bele 9, kupitia Wewe ni wangu.
Tuzo ya mtayarishaji bora wa mwaka – Maneke
Mkali huyu ambaye ametengeneza wimbo wa starehe gharama, aliwabwaga Marco Chali, Pancho, Bob Junior na Man Walter.
Tuzo ya video bora ya muziki ya mwaka – Diamond
Naam, nani anakataa kuwa hakustahili? Baada ya kuanguka vibaya mwaka jana, ambapo hakuambulia kitu, bilashaka alijipanga uzuri mno na akarejea msimu huu kivingine kabisa. Haikushangaza basi alipojiongezea tuzo ya tatu katika usiku huu baada ya kutwaa tuzo ya video bora ya mwaka kupitia wimbo wa moyo wangu. Alishindanishwa na Suma Lee aliyekuwa kaingiza wimbo wa Hakunaga, Kassim, Lady JD na wimbo wa Wangu.
Tuzo ya wimbo bora wa mwaka – Hakunaga
Ndio. Kona gani ambayo ungeweza kupita na usisikie wakiimba wimbo huu? Bila shaka Suma Lee, hakukosewa kupata tuzo hii licha ya kuwa alikuwa akipambana na nyimbo zingine zilizokuwa kali pia kwa mwaka uliopita za Dushelele, Moyo wangu, Mathematics, Nilipe nisepe, na Rizzy One.
Tuzo ya mwaka ya Taasisi iliyotoa mchango mkubwa katika sekta ya muziki nchini
JKT kupitia bendi yao ya JKT Taarab. Moja ya bendi kongwe za muziki wa taarab au mwambao, ambazo zimekuwa zikifanya vyema kwa miaka mingi hadi sasa huku nyimbo zao zikiwa zinaendelea kusikika masikioni mwa wapenzi wa burudani ya muziki.
Tuzo ya mtu binafsi aliyechangia kukuza fani ya muziki wa dansi nchini
Ilinyakuliwa na mzee mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpangu, maarufu kwa jina la kisanii la King Kikii, ambaye licha ya umri wake mkubwa, hadi hivi sasa angali akijishughulisha na muziki.
Tuzo ya mtu binafsi aliyechangia kukuza fani ya muziki wa dansi nchini
Tuzo hii ikanyakuliwa na marehemu Remmy Ongala. Licha ya kuwa hatunaye duniani, bado kazi zake zimeendelea kuwa na athari kubwa katika muziki nchini. Sifa yake kubwa ni kwamba, alipenda sana kuimba nyimbo ambazo zilikuwa zimeegemea zaidi katika uhalisia.
Tuzo ya mwimbaji bora wa kiume – Barnaba
Mshindi aliwashinda Diamond, Ally Kiba, Belle 9 na mkali wa miondoko ya mwambao, mzee Yusuph.

No comments: