Friday, April 6, 2012

MAPENZI YANA WIGO MPANA YATIZAMWE KWA JICHO LA TATU



KAMA ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona yetu, kwa uwezo wa Karima nina imani mu wazima wa afya njema. Siku zote sitaki kupiga porojo zaidi ya kuweka mada mezani ili kila mmoja aisome.

Kumekuwa na uwezo mdogo wa watu kufikiri mapenzi ni nini na muonekano wa mapenzi uko vipi. Leo nimelenga kwenye upungufu mkubwa katika utengenezaji wa filamu zetu zinazohusu mapenzi.

Wengi wanaamini kunyonya midomo ndiyo kuwakilisha mapenzi, mtu kukaa nusu utupu kitandani au bafuni, watakuwa wametimiza lengo lao hilo.

Ndiyo maana maandalizi ya mapenzi au muonekano wa mwanamke kwa mpenzi wake huwa jambo la siri lisilotakiwa mwingine alione. Naweza nisiwalaumu waandaaji kwa vile ni uwezo wa ufahamu kuhusu mapenzi yana mtazamo gani mbele ya jamii.

Nimekuwa mfuatiliaji wa filamu nyingi za mapenzi, ndani na nje ya nchi na kuangalia maigizo ya maudhui hayo yanawakilishwaje. Je, haya mapenzi tunayoigiza ndiyo tunapaswa kuishi ndani ya familia zetu?

Inawezekana wengi hawaelewi maigizo yanayoonekana mbele ya jamii huwa kivuli cha maisha tunayoishi, mengi yakiwa yanalenga kuelimisha jamii na si kupotosha.
Pia yanazingatia utamaduni wa nchi yetu husika, lakini kwa baadhi ya waigizaji wetu nina imani kabisa ni uwezo mdogo wa kukifahamu kile unachokifanya kwa kuamini wapo sahihi na hawataki kujifunza.

Siku zote usipotaka kujifunza na kubadilika utajiona unakwenda mbele na mwisho wake utakuwa unapiga ‘maktaimu’ na kupoteza nguvu zako.
Sitaki kuhamia sana katika uwezo wa waandaaji wa maigizo ila nataka nitoe elimu ya mapenzi ambayo huenda itakufumbua macho zaidi na kuvaa uhusika ambao utaangaliwa na rika zote.

Katika maigizo hayo kuna aina nyingi ya kuwakilisha mapenzi ya wawili na si lazima mlale kitandani mkiwa nusu utupu, kunyonyana ndimi au kushikana maeneo ya aibu ambayo anatakiwa kuyagusa mtu wako tena mkiwa faragha.

Kumbuka mwanadamu ameumbwa kwa matamanio hasa kiumbe wa kike, kuna sehemu anatakiwa kuguswa na mpenzi wake tena kumuandaa kwa ajili ya tendo wkiwa faragha.

Unapocheza filamu ya mapenzi halafu mnyonyanye ndimi tena kwa kurudia zaidi ya mara tatu, inakuwa si sawa kwa vile kuna siku mzazi wa mmoja ama wahusika wote ataona mchezo ule pengine na akiwa na familia, kisha amuone mwanaye katika tukio lile.

Nasema haya kutokana na baadhi ya watu kushindwa kuwapa ruhusa wake au marafiki zao wa kike kwenda kushiriki kwenye tasnia hiyo kutokana na kile kinachofanyika huko.

Hebu tuangalie picha za nje za mapenzi hata za Kinigeria kama My love, True Love, Real Love, na za nje kama La Muja, Timeless nyingine kadhaa za Kihindi ambazo zinatazamwa kwenye ulimwengu wa filamu za mapenzi, huwezi kuona uchafu kama unaofanywa na baadhi ya waigizaji wa Tanzania na kwingineko.

No comments: