Na Luqmani Maloto
KILA
mtu angeyaheshimu mapenzi, angejua jinsi ya kulinda hisia za mwenzi
wake. Angeelewa maana ya kupenda, asigekuwa na shaka pale anapopendwa.
Angeishi ndani ya mwenzake, hivyo kuumizana kusingekuwepo, migogoro
mikubwa na kuachana isingetokea.
Migogoro mingi inatokea kwa sababu
wengi wameyageuza mapenzi kama mchezo (game), hawajui kuwa saikolojia
inaonya vitendo vya kuucheza shere moyo wa mtu. Kumfanyia hivyo mtu
mwenye hisia za ndani na za kweli katika kupenda unaweza kuua bila
kukusudia.
Katika sehemu ya kwanza ya makala haya wiki iliyopita,
nilieleza kuwa kama hujawa tayari kupenda, kunyenyekea na kuheshimu ni
vizuri ukakaa pembeni kwa sababu unaruhusiwa kucheza game na mtu lakini
ni kosa kubwa kucheza game na moyo wa mtu.
Hata hivyo, nilitaka kila
mtu awe makini anapokuwa anaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu.
Anapaswa kujihakikishia upendo kutoka moyoni badala ya kujaribu. Wengi
walioingia kwa mtindo wa kupima kina cha maji, walilia kwa kusaga meno.
Lipo
tabaka ambalo linakuwa limejitosheleza kuwa mapenzi hamna lakini
wanang’ang’ania, matokeo yake wanauguza jeraha la moyo kwa muda mrefu.
Wengine wakajipa ugonjwa wa moyo. Ni vizuri kuwa makini mno ikiwa
unahitaji kupata thamani halisi ya penzi.
Pigania kuhifadhi moyo
wako. Uweke katika himaya salama. Usijidanganye kwa penzi lisilo na
uelekeo. Lenye sura ya upande mmoja. Wewe unapenda, yeye anakuchora,
presha inakupanda na kushuka mwenzako hana habari hata kidogo, tena
ikiwezekana atakucheka kama katuni.
Kuna watu hawaoni umuhimu wa
hili, mpenzi maana yake ni msiri wa maisha yako. Unapokuwa umelala
fofofo hujitambui, ubavuni kwako yupo yeye. Anaweza kukufanya lolote
wakati wewe unaogelea ndotoni. Mpende akupendaye, vinginevyo utakumbana
na maumivu yafuatayo;
HATOKUSIKILIZA IPASAVYO
Mapenzi ni
hisia. Ni rahisi kwako kujua kwamba uliyenaye anakupenda kwa dhati
mnapokuwa mnazungumza. Je, anakusikiliza kiasi gani?
Mtu ambaye hana
mapenzi na wewe, hata umwambie kwa lugha gani hawezi kukuelewa. Tena
inawezekana ulizungumza naye jana kwa herufi kubwa, lakini leo jua
limechomoza anarudia yale yale.
Inawezekana ulimuonya kuhusu tabia
ambazo zinakufanya heshima yake ipotee. Hakatazwi kuwa na marafiki wa
jinsi nyingine, lakini mazoea yake siyo mazuri kiasi kwamba wanaweza
kutembea barabarani wameshikana viuno. Ikiwa unamueleza habadiliki, huyo
hakupendi.
Hakusikilizi kwa sababu hana hisia na wewe.
ATAPENDA KUKUFANANISHA
Haamini
kama wewe ni mwanamke au mwanaume mwenye mvuto kamili. Akiona wengine
barabarani ni rahisi kushawishika. Atajiuliza hivi huyu na wangu vipi?
Huyu anaonekana ni mzuri zaidi. Anajiuliza maswali hayo kwa sababu
hajakukubali. Shtuka mapema.
Mwanasaikolojia Brandon King katika
makala yake: “Be aware with ones heart!” anasema kuwa ni rahisi mtu
kujidanganya kwamba aliyenaye siyo chaguo sahihi kwa sababu yupo naye
lakini hiyo hutokea kwa mtu ambaye mapenzi yake si asimilia 100.
Anasema:
“Vitu vya thamani yeye huvichukulia ni rahisi. Hajui kama mpenzio wake
ni wa gharama kubwa. Mtu wa barabarani labda kwa sababu tu amevaa
kapendeza, yeye ataanza kumfananisha na mwenzi wake nyumbani na
ikiwezekana kumuona bora.
“Wengine hawana uvumilivu, kwahiyo wanaweza
kujikuta wakimwaga sifa kwa watu wa pembeni. Wakiendelea huharibu
kabisa kwa sababu hujikuta wakiwaeleza hata wapenzi wao, kitu ambacho
taaluma ya saikolojia katika eneo la mapenzi inakataza.”
Brandon
anaonya: “Ni kosa kubwa kumsifia mtu wa jinsi inayofanana na mwenzi wako
mbele yake. Mfano unamwambia mwenzi wako wa kiume kwamba ‘yule kaka
mzuri jamani’! Hata kama huna hisia za ndani ya moyo wako lakini haiwezi
kumpa picha nzuri, atajiona hayupo salama kwamba unavutiwa na mwingine.
“Fikiria
na wewe upande wako. Mwenzi wako anamuona mwanamke na yeye anamwagia
sifa, ‘dah yule manzi mrembo, wewe ungekuwa mrembo kama yeye ningejidai
sana’! Bila shaka utaumia sana, kwahiyo na yeye ndivyo anavyoweza kupata
maumivu.”
Anashauri: “Kila mmoja aridhike kwa jinsi mwenzi wake
alivyo. Haikusaidii kitu kumuona bora wa jirani kwani kuna wenzako
wanajiuliza huyo wako watampataje? Mheshimu na mtukuze mbele za watu.
Ukijenga imani kwamba mpenzi wako ni bora kuliko wote duniani, itakuwa
na moyo wako utakubali.
No comments:
Post a Comment