Friday, May 20, 2011

Umia mara moja, uupe moyo wako furaha ya kudumu!



MAPENZI ni sanaa marafiki zangu, ili uweze kuwa msanii kamili katika tasnia hiyo ni vyema kutafuta kuwa bora zaidi kila siku. Uwe mshindi siku zote, mwenye kumridhisha mpenzi daima, mwenye kumfanya afurahie kuwa na wewe.

Lakini katika kutafuta ubora, suala la kujiangalia na kuhakikisha unajenga maisha yako yajayo sawasawa ni la lazima. Watu wengi wanafeli maisha kwa sababu ya kukosea katika kuchagua wenzi sahihi.

Kwa wewe kijana ambaye bado hujafunga ndoa, huu ni wakati wako sahihi wa kufanya uchaguzi bora ambao hautakuwa na majuto hapo baadaye. Hapa nazungumzia juu ya kutizama maisha yako yajayo.

Acha kuangalia leo, wakati kesho yako inaonekana wazi kuwa mbaya, yenye majuto ya kila aina. Ieleweke kwamba, maisha utakayoishi kesho ni matokeo ya jinsi unavyoishi leo.
Wakati mwingine mtu anakuwa na mpenzi wake, ana kasoro kibao, kila siku ugomvi, hakuna uelewano, lakini kila anapotaka kuachana naye, hisia kali za mapenzi dhidi yake zinamzidi na kujikuta akiendelea kuwepo kwenye penzi la mateso.

Huu si wakati wa kunyanyasika katika mapenzi, ni muda ambao unatakiwa kuangalia vyema tabia na mwenendo wa mpenzi wako, kama hairidhishi, usijiumize; chukua hatua ya moja kwa moja huku ukizingatia kwamba, maisha yako yatakayofuata yatakuwa bora ukijivunia ujana wako.

Ndiyo maana nikasema ni bora ulie mara moja lakini uishi kwa furaha siku zote katika ulimwengu wa mapenzi. Rafiki zangu, mkikosea kufanya uchaguzi wa wenzi wenu leo, mfahamu kwamba maisha yenu yote yatakuwa yenye machozi. Yenye maumivu. mtalia kila siku mkinyanyasika kwa sababu ya mapenzi.

Sikia, achana na fikra potofu, hata kama unapendwa sana, anajua mapenzi sana, ana faida gani kama kila siku ameendelea kukuumiza? Kukunyanyasa? Kukusimanga? Haoni faida yako, anakudharau waziwazi? Kwa nini uendelee kukaa kifungoni wakati kuna njia?

Mwingine anaweza kusema huyu kaka Shaluwa vipi, leo mbona anafundisha watu kuachana, la hasha! Sina lengo la kufundisha watu kuachana, nataka kuona watu wanatoka katika utumwa wa mapenzi na kuwa na amani siku zote za maisha yao. Ndiyo lengo hasa la mada yetu ya leo.
Rafiki zangu, mwamuzi wa mwisho wa maisha yako ni wewe, hatatokea mtu wa kukupangia maisha bora hapo baadaye, yote hayo unapaswa kufanya peke yako. Chagua maisha uyapendayo na uishi katika msingi huo.

Kwa nini watu wanachanganya mapenzi na mazoea? Mwingine anaweza kabisa kujua kuwa mwenzi wake anamuumiza, anamtesa na kuunyanyasa moyo wake lakini anaamua kuendelea kuwa naye akiamini kwamba eti hatapata mwingine wa kuwa naye.
Hayo ni makosa, ni hisia potofu ambazo kwa hakika zinaweza kukuingiza katika mateso ya kudumu.

Msomaji wangu mpendwa, kupitia mada hii, napenda kukutangazia kwamba, unakwenda kubadilika na utakuwa mwenye uwezo wa kuchukua uamuzi mgumu kwa leo na kuandaa maisha yako yajayo.
Haijalishi kama utaumia kiasi gani? Utalia kwa kiwango kipi, lakini angalau utakuwa umeanza safari ya kutengeneza maisha yako. Hebu sasa twende darasani tukajifunze pamoja.

Unajipangaje?
Ili mada hii ikuingie vizuri, lazima ujiulize umejipangaje kwa ajili ya maisha yako ya baadaye? Rafiki zangu, ninaposema kuangalia maisha yako yanayofuata namaanisha mustakabali wako.

Kwamba maisha yako baada ya leo ni yapi? Unahitaji kuishi maisha gani? Maana kama ukiwa hujui unataka kuishi vipi, utakuwa unakwenda bora siku zisogee na mwishowe, utajikuta ukijuta.

Siku moja inapoondoka, haiwezi kurudi tena, lazima akili yako ifanye kazi zaidi kuhakikisha kwamba kesho yako inakuwa nzuri.

Ili kesho iwe nzuri, leo nayo inatakiwa iwe nzuri zaidi. Ukifanya vibaya leo, basi matokeo ya kesho nayo yatakuwa mabaya. Umeona eeh! Bado kuna mengi ya kujifunza, lakini kutokana na ufinyu wa nafasi, naomba kuweka nukta hapa. Wiki ijayo tutaendelea na sehemu ya pili ambayo ndiyo ya mwisho.

No comments: